UBINAFSI NA TAMAA VINAITESA DUNIA
Misingi ya ukweli imefichwa
BAada ya dunia kuendelea kukumbwa na machafuko ya
mauaji, utekaji, vita, kuumizana, na kunyanyasa watoto, Kiongozi wa Kanisa
Katoliki Duniani Papa Fransisko amesema viongozi wasiishie tu kuona huruma juu
ya mateso ya watu bali watafute chanzo na suluhisho ili dunia iwe mahali salama
pa kuishi.
Papa Fransisko amezungumza hayo wakati alipohutubia waamini kwenye sala ya
malaika wa Bwana Septemba 20 mwaka huu katika Viwanja vya Kanisa Kuu la
Mtakatifu Petro Vatikani.
“Waamini na viongozi wasiwe watazamaji, wanaosikitishwa na matukio
mbalimbali yanayotendeka sehemu mbalimbali za dunia, bila kujishughulisha hata
kidogo kutafuta chanzo na suluhisho ili kusaidia unyanyasaji wa mwanadamu
duniani kukoma.
Ni vyema, ikiwa kama waamini watajiuliza swali la msingi, ikiwa kama kweli
wana huruma, wanaweza kusali na kujishughulisha kadiri ya nafasi na uwezo wao
yale wanayoyaona yakitangazwa kwenye vyombo vya mawasiliano ya jamii. Haitoshi
kuwaonea watu huruma, bali kuchukua hatua madhubuti ili kuwasaidia.”
Kufuatia rai hiyo iliyotolewa na Baba Mtakatifu, baadhi ya Maskofu wa
Kanisa Katoliki Tanzania wamesema kuwa, dunia inateswa na ubinafsi, madaraka ya
mali na utawala usiojali wengine.
Akizungumza na Gazeti Kiongozi, Askofu wa Jimbo Katoliki Geita Mhashamu
Flavian Kassala amesema kuwa ubinafsi umewasababisha watu hususani viongozi
kujiona wanastahili kuliko wengine.
“Ndiyo maana wanasahau sura ya Mungu ndani wa watu wengine, wanasahau utu
wa mwanadamu wenye thamani isiyopimika. Wanajihesabia haki hata kama wamekosea,
ubinafsi unawasahaulisha kuwa wana mapungufu, wanahitaji kusamehe na
kusamehewa.
Kuanzia mtu binafsi kuelekea kwenye taasisi inakuwa mbaya zaidi pale
taasisi inapogubikwa na ubinafsi unaosababisha isahau mahitaji msingi na haki
za wengine.
Anayeongoza taasisi anachochea dhuluma, uonevu na kunyanyasa wengine kwa
sababu tu ana nguvu. Hajali utu wa watu wake, anashirikiana na wengine
kunyanyasa watu kwa kujihesabia haki ya madaraka na mali. Hicho ndicho chanzo
cha mateso na maumivu ya watu duniani,” amesema Askofu Kassala.
Aidha ameeleza kuwa, ubinafsi unaanzia kwa mtu binafsi, taasisi ndipo
uende kwenye mataifa ambapo wachache wanapewa dhamana ya kuongoza wengi. Watu
hao wakiwa na ubinafsi, wanapitisha sera zilizo na ubinafsi.
“Tunateseka kwa sababu watawala na viongozi wamekataa ukweli kwamba kuna masikini
wanahitaji kusaidiwa, wanatunga sera zilizo na ubinafsi ndiyo maana kuna
biashara za unyonyaji na maamuzi yaliyogubikwa na ubinafsi wa kupendelea upande
mmoja.
Tumekataa misingi ya kweli (Fundamenta truth) unaotupa miongozo ya namna
ya kuishi ambayo kwa asili Mungu alishaiweka.
Msingi wa ukweli kuwa huyu ni mama, baba, mzazi wangu ama mtu mwingine
mwenye utu ni ukweli.
Tumefuta ukweli huo, ndiyo maana
tunawafanyia mambo ambayo hayastahili
kwa sababu tumekataa watoto na tunawaona watoto sawa na watu wazima,
tunawafanyia ukatili, tunawanyanyasa wazazi wetu, tunaumizana kwa sababu
tumefuta misingi ya kweli. Aliye na utu anafahamu utu wa mwingine hawezi
kumuumiza na hili halihitaji mtu awe na dini Fulani,” Amefafanua Askofu
Kassala.
Hata hivyo amesema ukweli, utu na kuthamini ubinadamu unajengwa na
kuimarishwa zaidi na chachu ya imani hususani chachu ya Injili. Ndiyo maana
anasisitiza jamii hususani dini kuwekeza kwenye imani, malezi na maadili kwa
watoto.
“Katika imani kuanzia kwa watoto wetu, tutapoteza imani, kujua ukweli
(Fundamental truth).Inaweza ikaenda kwenye mataifa, na mtu huyu ana madaraka
makubwa. Wao kama viongozi kwa pamoja wanaweza kupitisha sera za kibaguzi, za
unyonyaji na kusahau wengine. Tumebaki tunapiga kelele juu ya haki za binadamu,
kusaidia masikini, lakini, je, tunatenda? Kama mtu binafsi ninatenda? kama
taasisi inatenda? kama mataifa yanatenda?.
Tukitenda tutashinda, lakini tukibaki tunaongea tu, kunyoosha vidole, sera
zitakuwa nzuri sana lakini hazina watendaji. Na sera zitakuwa zimetawaliwa na
ubinafsi uleule kama vile mwanadamu alivyoumbwa kwa sura na mfano wa Mungu
lakini akaamua kufunga macho akaisahau ile sura ya Mungu ndani mwake na kwa
wengine.
Ubinafsi unaleta biashara zisizo na usawa, wizi, mauaji, vita, umiliki wa
silaha.
Kabla ya imani iko miongozo ambayo Mungu ametuwekea ndani mwetu. Mfano
kuelewa kuwa kuua ni dhambi haihitaji uongoke katika imani, kuelewa kwamba
wahitaji wanahitaji msaada, kuelewa haki za binadamu maana binadamu na haki na
mahitaji msingi, huhitaji dini! Dini inatupa mwelekeo na hatua nyingine ya hayo
ambayo ni ya kawaida. Hata Tamko la haki za Binadamu la Umoja wa Mataifa halina
itikadi za dini, kabila wala taifa.
Ni la haki za msingi za binadamu kwani kwa asili anahitaji mavazi,
chakula, anahitaji kuishi. Hayo hayasubiri mtu awe na dini, ni fundamental
truth. Tuache ubinafsi, tusafishe dhamiri, tuwe na utu,” Amesema.
Askofu Niwemugizi; Mtu asiyemwamini Mungu ni hatari,
anafanya lolote
Kwa upande wake Askofu wa Jimbo Katoliki Rulenge-Ngara Mhashamu Severine
Niwemugizi amesema kuwa, ni kweli hata katika taifa letu kuna matatizo ya
utekaji nyara hususani watoto, kuua watu, dhuluma, kuteswa n.k. lakini yote
amesema ni kukubali kutawaliwa na ubinadamu, tamaa na kumuacha Mungu.
“Ukisoma Wagalatia 5 Mtume Paulo anaeleza vizuri sana akisema kuwa mwili
hushindana na roho. Mwanadamu akiruhusu tamaa ya mwili kushinda tunda la roho
anakuwa na vurugu nyingi.
Anakuwa na uchu wa madaraka yasiyojali wengine, anakuwa na tamaa ya mali,
umaarufu kwa kunyanyasa na kuumiza wengine.
Tunda la Roho ni upendo, furaha, amani, uadilifu, utu wema, fadhili na
uaminifu. Kumbe tunahitaji watu (waamini, wananchi) pamoja na viongozi
wanaoongozwa na Roho ya Mungu. Ukikosa matunda ya Roho wa Mungu lazima ufanye
mambo kinyume na Amri za Mungu na kuficha dhamiri kwani unatawaliwa na tamaa
zako binafsi kwa kutesa wengine,” Amesema Askofu Niwemugizi.
Amesema kuwa, ingawa yapo mataifa yasiyomwamini Mungu (secular) lakini
yanathamini utu wa mwanadamu. Pia yapo mataifa kama Tanzania yanayo mwamini
Mungu lakini halijaweka maadili kikatiba hivyo haki inaweza kuvunjwa na kubakia kusema taifa hili linamwamini
Mungu wa maneno.
Tuweke vipaumbele vyetu vya kujenga taifa lenye amani kikatiba kwamba
hakuna mtu anaweza kukiuka.
Taifa letu lifundishe maadili kuanzia shule za awali ili kulea dhamiri
zinazoheshimu utu wa mwanadamu. Dhamiri nyoofu inaheshimu utu, haki, usawa,
inajali wanyonge, inasikiliza, inakosoa na kukubali kukosolewa, inakubali
msamaha na kumheshimu Mungu. Anayeenda kinyume na hayo anaweza kufanya mambo ya
ajabu,” Amesisitiza Askofu Niwemugizi.
Askofu Banzi- Uvuguvugu wa imani chanzo cha matatizo
Akizungumzia juu ya umwagaji damu duniani, Askofu wa Jimbo Katoliki Tanga
Mhashamu Anthony Banzi amesema kuwa,
uvuguvugu wa imani ndiyo chanzo cha yote kwani mwenye imani ana hekima,
anamuogopa Mungu.
“Inaelekea hatujainjilisha vya kutosha. Tufanye uinjilishaji wa kina ili
watu wawe na hofu ya Mungu, wajali utu wa mwanadamu pamoja na thamani yake.
Wakristo waliobatizwa leo hii wanaacha imani yao inayofundisha msamaha,
kusikiliza dhamiri, kuheshimu uhai. Wapo waliobatizwa na leo hii wanajiita
wakristo tena wa Kanisa Katoliki lakini wapo vuguvugu, mguu mmoja ndani ya
imani mwingine nje.
Ni wabinafsi wa kujilimbikizia mali na madaraka. Chako ni changu , changu
ni chetu. Hapana tuendelee kuwapa mafundisho ya imani ili waachane na ubinafsi
uliopindukia ambao ndicho chanzo cha umwagaji damu duniani.
Tusisitize uinjilishaji mpya kwa kila mtu. Hakuna mtu asiyehitaji
Katekisimu endelevu. Tuwe na mikakati mbalimbali ya kuwekeza kwenye imani ili
tutengeneze taifa linalomcha Mungu. Watu wenye huruma wanaoguswa na mahangaiko
ya jirani zao. Hiyo ndiyo kazi yetu
viongozi wa dini,” Amesisitiza Askofu Banzi.
Comments
Post a Comment