KANISA KATOLIKI KUBORESHA HUDUMA ZA AFYA NCHINI
IDARA ya
Afya ya Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania (TEC) imefanya mkutano wa Mwaka
ili kutathmini utendaji kazi pamoja na kujadili mbinu za kuboresha utoaji
huduma za Afya katika hospitali na vituo vya Afya vinavyomilikiwa na Kanisa
Katoliki nchini.
Mkutano huo umefanyia hivi karibuni katika Baraza
la Maaskofu Katoliki Tanzania Kurasini jijini Dar es Salaam ukijumuisha
Makatibu wa Afya Jimbo, madaktari wa hospitali zinazomilikiwa na Kanisa Katoliki, wasimamizi na Wakuu wa Vituo
vya Afya vya Kanisa Katoliki.
Akifungua mkutano huo Mwenyekiti wa Kamati ya Afya
TEC Askofu Mkuu Jude Thadeus Ruwaich amesema kuwa anatumaini mkutano huo
utaleta matokeo yenye tija katika kuboresha utoaji wa huduma ya afya kwa
hospitali na vituo vya afya chini ya Kanisa Katoliki kwa wananchi.
Ajenda kuu ya mkutano huo ni "Kuimarisha
uwezo wa Vifaa vya Afya katika hospitali na vituo vya Afya vya Kanisa Katoliki
kutoa huduma bora: Kutathmini uwezo,
fursa, udhaifu, changamoto na kuangalia suluhisho" kwa lengo maalum la kubaini
njia za ubunifu juu ya utoaji wa huduma za afya, upatikanaji wa huduma za afya
bora, fedha ambazo ni moja ya mikakati ya kuendeleza mifumo ya utoaji wa huduma
za afya na kuboresha mawasiliano kati ya TEC na taasisi za afya katika majimbo.
“Ni matumaini yangu kuwa majadiliano yetu
yatatusaidia kufikiria kwa kiasi kikubwa juu ya kile tunachokifanya, jinsi
tunavyofanya ili mwishowe tupate matokeo yaliyokusudiwa ambayo yanaboresha upatikanaji
na ubora wa huduma za afya tunayozitoa.
Wakati wa mkutano wa mwaka jana, tulijitolea
kuboresha upatikanaji wa huduma za afya bora katika taasisi za afya za
Kikatoliki. Mkutano huu pia utajadili hali ya utekelezaji wa hatua za vitendo
ambazo tulikubaliana wakati wa mkutano wa mwisho.
Nimeambiwa kuwa wakati wa mkutano wa mwaka huu, Tanzania
Christian Madical Associations (TCMA) ilijadili pia changamoto ambazo
tunakabiliwa nazo katika kutoa huduma za afya kwa jamii kama vile masuala
yanayohusiana na rasilimali za afya, fedha, mikataba ya watumishi na ubora wa
huduma. Pia ulipendekeza baadhi ya njia za kutatua.
Hivyo ninawahimiza kujadili kwa kina na kuzipitia
ili kuhakikisha kuwa watu wote wanapata huduma bora za afya zinazotolewa katika
Taasisi za Afya Katoliki.”
Mkutano huo umewashirikisha wakurugenzi wa afya
majimboni, wakuu wa vitengo pamoja na wadau mbalimbali wa sekta ya afya
wakiwemo wakurugenzi na wakuu wa Idara mbalimbali za Baraza la Maaskofu
Katoliki Tanzania (TEC).
Baadhi ya maadhimio ya mkutano huo ni pamoja na
kutumia teknolojia katika kukusanya mapato ya hospitali, kuzingatia maadili ya
Kanisa Katoliki katika utoaji huduma, kuhamasisha wananchi kuwa na bima ya afya
ili kuwa na uhakika wa kupata matibabu.
Aidha kuibua mikakati itakayohakikisha utoaji wa
huduma za afya utakuwa endelevu na kuwa na majadiliano na serikali ili mpango
wa kutoa huduma za afya bure kwa makundi
maalumu yasiathiri Hospitali za Kanisa
na vituo vyake kuendelea kutoa huduma za Afya kwa wananchi.
Comments
Post a Comment