"JIKITENI KATIKA MALEZI YA KIKRISTO"
Baba Mtakatifu Francisko kama sehemu ya mwendelezo wa Katekesi kuhusu “Matumaini ya Kikristo”, Jumatano tarehe 20 Septemba 2017, kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican, amejikita zaidi katika umuhimu wa “Malezi ya matumaini” kwa kujiaminisha kwa walezi na watu wenye dhamana kama hii ili kujifunza matumaini ya kikristo, ili hatimaye, kukuza ile mbegu ya matumaini iliyopandwa ndani mwao na Mwenyezi Mungu.
Adui wa kwanza ambaye waamini wanapaswa kumwogopa yuko ndani mwao anayejitokeza kwa njia ya mawazo machafu. Mwenyezi Mungu mwingi wa huruma na mapendo, amewawekea waja wake, fadhila ya imani na matumaini ambayo ni sawa na chanda na pete, kwani zinahitajiana na kukamilishana, ili kuweza kufikia ukweli mkamilifu. Mwenyezi Mungu, daima anawasubiri waja wake, ili waweze kupiga hatua ya kwanza, kwa kumwamini yeye ambaye ni Muumba na Roho Mtakatifu anayeongoza mambo yote kadiri ya mpango wa Mungu. Ulimwengu unasonga mbele kutokana na mchango wa watu mbali mbali ambao wanathubutu kujenga madaraja; watu ambao wanaota ndoto hata pale wanapoonekana kukwama na kutaka kukata tamaa!
Baba Mtakatifu anapenda kuwatia shime waamini kupambana kufa na kupona pasi na kujikatia wala kukatishwa tamaa, kwani iko siku Mwenyezi Mungu ataweza kuwatekelezea ndoto zao, kwani kamwe Mwenyezi Mungu hawezi kumhadaa mja wake, kwani amepandikiza katika sakafu ya moyo wa mwanadamu matumaini yanayomwezesha mwamini kusonga mbele, kwa kujiaminisha mbele ya Mwenyezi Mungu. Katika shida na mahangaiko ya binadamu, Baba Mtakatifu anawaalika watu kusimama na kuendelea mbele, kamwe wasikubali kulalama hapo chini walikobagwa. Wawe ni vyombo vya huruma na upendo wa Mungu, ili kuondokana na mchoko unaoweza kuwaletea madhara makubwa katika maisha, hasa pale wanapojisikia wakavu kutoka katika undani wa maisha yao!
Baba Mtakatifu katika mazingira ya kukata tamaa, anawataka waamini wajitahidi kuwa kweli ni vyombo na wajenzi wa amani; kwa kuachana na sauti zinazowataka kulipiza kisasi na kusababisha utengano katika maisha ya watu ndani ya jamii. Binadamu hata katika utofauti wao, wameumbwa ili kukaa pamoja kwani binadamu ni kiumbe jamii. Kukosa na kukoseana ni sehemu ya ubinadamu; hali inayowalazimisha kuchukuliana kwa upole na uvumilivu, kwani iko siku watagundua kwamba, kila mmoja wao, alikuwa ana mbegu ya ukweli ndani mwake. Baba Mtakatifu anawahamasisha wakristo kujikita katika Injili ya upendo kwa kutambua kwamba, kila mtu anayo historia anayoweza kusimulia na kuwashirikisha wengine. Kila mtoto anayezaliwa ni alama ya uhai dhidi ya kifo na kwamba, kila upendo unaochipua katika moyo wa mwanadamu ni nguvu ya mabadiliko katika furaha.
Baba Mtakatifu anawataka waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema kuendelea kuota ndoto na kamwe wasikubali ndoto yao ipotee kama umande wa asubuhi, kwani matumaini yanawawezesha waamini kutambua kwamba, iko siku, kutakuwa na utimilifu wa kazi ya uumbaji; mwanga utang’aa zaidi na giza na uvuli wa mauti kutoweka kabisa. Matumaini yamewawezesha watu kupiga hatua kubwa katika maendeleo ya sayansi na teknolojia; wamesafiri baharini na hata kufika kwenye anga za mbali ambazo zilikuwa hazijaguswa na binadamu. Matumaini yamewawezesha binadamu kuvunjilia mbali utumwa na hatimaye kuboresha hali ya maisha ya watu wengi duniani.
Matumaini yamewawezesha viongozi wa Jumuiya ya Kimataifa kusimama kidete dhidi ya ukosefu wa haki msingi za binadamu zinazonyanyasa utu na heshima ya binadamu. Waamini wakumbuke kwamba, Kristo Yesu ameshinda woga kwa niaba yao na kwa njia ya Sakramenti ya Ubatizo, maisha yao yanafumbatwa katika Fumbo la Utatu Mtakatifu na kwamba, wao sasa ni mali ya Kristo Yesu anayeishi ndani mwao na kwamba, anataka kuwaweka adui zao chini ya miguu yao kama soli ya kiatu! Baba Mtakatifu anakaza kusema, adui wa binadamu ni dhambi, vita, ghasia na kisasi, lakini adui hawa wote iko siku, watapigishwa magoti!
Katika shida na mahangaiko ya ndani waamini wawe na ujasiri wa kuyatolea yote mbele ya Mwenyezi Mungu, huku wakiendelea kudumu katika uaminifu. Wanapotenda na kuanguka dhambini, wajipe moyo wa kusimama na kuanza tena, kwani Kristo Yesu, Mwana wa Mungu amekuja hapa duniani ili kumkomboa mwanadamu kutoka katika lindi la dhambi na mauti na kwamba, Mwenyezi Mungu anataka kujenga na kudumisha urafiki na binadamu wote. Mwishoni Baba Mtakatifu anawataka waamini kuishi, kupenda na kumwamini Mungu, neema zinazomwezesha mwamini kusonga mbele katika imani na matumaini bila ya kukata tamaa katika maisha!
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.
Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.
Comments
Post a Comment