WAAMINI OMBEENI TAASISI ZA KANISA- ASK. MSONGANZILA
WAAMINI wa Kanisa Katoliki Jimbo Katoliki
Musoma wamekumbushwa kuombea taasisi
zote za Kanisa zinazotoa huduma katika jamii ili ziweze kuendelea kutoa huduma
hizo kwa jamii kiroho, kielimu na kiafya kwa kuwa lengo la taasisi hizo ni
kumuhudumia mwanadamu bila ubaguzi.
Hayo yamesemwa hivi karibuni na Askofu wa Jimbo Katoliki
Musoma Mhashamu Michael Msonganzila wakati wa ibada ya kumshukuru Mungu kwa
Parokia ya Kiabakari kwa kutimiza miaka 25 tangu kuzinduliwa rasmi mwaka 1992.
Askofu Msonganzila amewakumbusha
waamini wa Jimbo hilo kuwa wanaposherehekea miaka 25 ya kuzaliwa kwa parokia
yao wasisahau kuziombea taasisi zote zilizopo chini ya Jimbo na Parokia hiyo ya
kiabakari ikiwemo shule, Zahanati na huduma zote za kuroho kwa kuwa kituo cha
Kiabakari ni kituo cha kikanda cha Lango
la huruma ambacho mahujaji mbalimbali wanafika kwa ajili ya kusali na
kutoa shukurani kwa Mwenyezi Mungu.
“Huduma zinazotolewa na taasisi zetu zilizopo
chini ya Jimbo letu la Musoma zina lengo la kumuhudumia mwanadamu, na ndiyo maana
taasisi hizi zinahudumia bila ubaguzi na zinaitwa kumbakumba, hivyo nawaomba
sana waamini tuweke mikakati wa kuwaombea watu wa mataifa ili waendelee
kuziombea taasisi zetu” amesema Askofu Msonganzila.
Askofu Msonganzila amewaomba waamini
kuhakikisha wanasimama imara katika imani yao, na kutokubali majaribu waliyokumbana nayo ndani ya miaka 25
kuwakatisha tamaa katika kuitetea imani yao, kwa kuwa kila penye mafanikio kuna
changamoto pia.
Amesema kuwa atajitahidi kuhakikisha
ifikapo 2018 kituo cha hija cha Kiabakari
kinatangazwa kuwa kituo cha hija cha Kitaifa, baada ya kupata baraka zote kutoka kwenye kikao cha
Maaskofu kitakachofanyika hivi karibuni Jijini Dar Es Saalam.
Kwa uapande wake Paroko wa Parokia ya
Kiabakari Padri Wojciech Koscielniak amesema kuwa wanamshukuru Mungu kwa zawadi
ya uhai kwa kusherehekea miaka 25 ya Parokia hiyo baada ya kutangazwa rasmi na
Hayati Askofu Justine Samba Agosti 21
mwaka 1992, ambapo katika risala yake aliomba siku moja kituo hicho cha hija
kiweze kutangazwa kituo cha Hija cha Kitaifa kwa kuwa watu wa Mataifa
mbalimbali wanafika katika kituo hicho kwa ajili ya kuhiji.
Comments
Post a Comment