KUTUKUKA KWA MSALABA WA BWANA WETU YESU KRISTO
KAnisa
huadhimisha Sikukuu ya Kutukuka kwa Msalaba wa Bwana wetu Yesu Kristo tarehe 14
Septemba kila mwaka. Katika Kanisa la Mashariki Sikukuu hiyo inatukuzwa sana na
huadhimishwa kama sherehe. Tumeona vema kueleza kifupi historia ya Sikukuu
hiyo.
Kifo cha Msalaba
Adhabu ya kumsulubisha mhalifu kufa msalabani ilikuwa
ya kikatili sana na yenye maumivu makali sana. Mhalifu alikufa polepole kwa
mateso na aibu kubwa sana kutokana na kusulibiwa akiwa uchi. Adhabu hiyo iliyoanzia sehemu za Asia-ndogo ilienea
hata kufika magharibi. Wagiriki au Wayunani hawakuitumia sana adhabu hiyo
kwaniilidhalilisha na kuwapa mateso sana waliopata; lakini Warumi waliitumia
mara nyingi kwa watumwa katika mataifa
ambayo yalikuwa chini ya dola yao. Wahalifu waliokuwa magaidi, wevi sugu na
waliopinga serikali walipata adhabu hiyo bila huruma.
Kwa kawaida wahalifu waliopata adhabu ya kutundikwa
msalabani walipigwa kisha walibebeshwa
gogo la msalaba mpaka walipofika mahali waliposulubiwa. Hapo kulikuwa
limesimikwa tayari gogo la kumsimamisha mhalifu. Wahalifu walivuliwa nguo zao
na kutundikwa msalabani. Waliachwa vile katika mateso makali wakiteseka kwa
baridi hasa wakati wa majira ya baridi. Wakati wa joto kali waliteseka kwa joto
kali, kiu na njaa. Pengine waliopita kando, waliwachekelea na kuwatukana
wahalifu hao.
Ingawa Bwana Yesu hakuwa na kosa lolote, alipata
adhabu hiyo kwa sababu Wayahudi walidai asulubiwe. Wayahudi wenyewe walikiona
kifo cha kutundikwa msalabani kuwa kifo cha laana kama ilivyoandikwa na Mose
katika Kumbukumbu la Torati
kwamba “aliyetundikwa amelaaniwa na Mungu”.
Kwa hiyo alitakiwa kuzikwa siku hiyohiyo alipokufa bila kuchelewa; la sivyo
alisababisha unajisi katika nchi(Rej Kumb 21:22-23).
Msalaba wa Kristo
Aliposulubiwa Yesu, msalaba wake haukufikiriwa kuwa
mti wa maana, bali kama gogo au mti
uliotumika kama adhabu kwake, ingawa Mitume na wengine walifahamu kwamba
hakustahili adhabu ile; hakuwa na kosa. Mti wa msalaba wa Yesu uliachwa tu.
Hata hivi kifo chake Yesu msalabani kilipata kuwa
ishara ya sadaka na ukombozi wa watu tangu wakati wa Mitume. Mtume Paulo
aliweza kufundisha na kuandika: “Kwa sababu Wayahudi
wanataka ishara, na Wayunani wanatafuta hekima; bali sisi tunamhubiri Kristo,
aliyesulubiwa; kwa Wayahudi ni kikwazo, na kwa Wayunani ni upuzi; bali kwao
waitwao, Wayahudi kwa Wayunani, ni Kristo nguvu ya Mungu, na hekima ya Mungu”(1Kor
1:22-24).
Tena Mtume Paulo katika waraka wake kwa Wakaristo wa
Galatia aliweza kuandika kwa imani na uhakika: “Lakini mimi, hasha,
nisione fahari juu ya kitu chochote ila Msalaba wa Bwana wetu Yesu Kristo,
ambao kwa huo ulimwengu umesulibishwa kwangu, na mimi kwa ulimwengu. Kwa sababu
kutahiriwa si kitu wala kutokutahiriwa, bali kiumbe kipya” (Gal
6:14-15).
Basi, kifo cha Yesu Kristo Msalabani ni kifo cha
sadaka ya kuwakomboa wanadamu; wote wanaomsadiki wanakuwa viumbe vipya. Kwa
hiyo mti wa Msalaba wake umekuwa na
thamani kubwa katika imani ya Kikristo tangu wakati wa Mitume.
Kutukuka kwa Msalaba
Kadiri ya mapokeo ya Alexandria ni kwamba Mtakatifu
malkia Helena alipokwenda kuhiji Yerusalemu aliubaini na kuuvumbua Msalaba wa
Yesu Kristo tarehe 14 Septemba 320. Kumbe wakati huo huo makanisa makubwa
yakawa yanajengwa juu ya kilima cha Golgotha. Kanisa moja lilijengwa pale
aliposulubiwa Yesu na jingine pale alipozikwa. Kanisa lililojengwa pale
aliposulibiwa huitwa Kanisa la Msalaba
na lile lililojengwa pale alipozikwa
huitwa Kanisa la Ufufuo. Makanisa hayo yote
mawili yalitabarukiwa siku moja, tarehe 13 Septemba, 335 kwa vile yalivyokuwa
jirani. Siku iliyofuata, tarehe 14 Septemba 335, Msalaba wa Yesu, ambao
Mtakatifu malkia Helena alikuwa ameuvumbua, uliletwa kwa heshima na fahari
kubwa na kuwekwa mahali pa heshima ili waamini waweze kuutukuza kwa ibada
kubwa.
Matukuio hayo ndiyo chanzo cha Sikukuu ya Kutukuka kwa Msalaba kwani kila mwaka
tendo la kuutukuza msalaba liliadhimishwa mjini Yerusalemu na baadaye limeenea
sehemu nyingine. Tayari katika karne ya tano Sikukuu hiyo ilikuwa inaadhimishwa
katika kanisa kuu la Konstantinopoli. Mwishoni mwa karne ya saba Sikukuu hiyo
ilikuwa imepokewa na kuadhimishwa pia katika kanisa la Roma. Katika makanisa
makuu hayo ya Yerusalemu, Konstantinopoli na Roma walikuwa na vipande vikubwa
vya Msalaba wa Yesu. Tarehe 14 Septemba
ilikuwa kawaida katika makanisa hayo kuvitoa kwa ibada vipande hivyo vya mti wa
Msalaba wa Bwana ili waamini waweze kuviheshimu na kuutukuza kwa ibada.
Adhimisho hilo liliitwa kutuzwa au kutukuka
kwa Msalaba.
Misa ya Sikukuu
Wazo kuu la Sikukuu ya Kutukuka kwa Msalaba ni kifo
chake Yesu Kristo ambacho kimewaletea ukombozi watu wote. Wimbo wa mwanzo ni
maneno ya Mtume Paulo kwa Wagalatia ambayo tumeyanukuu hapo juu. Kifo cha Yesu
juu ya Msalaba kimeleta wokovu, maisha halisi ya neema na ufufuo wetu.
Katika sehemu ya mwanzo ya Sala ya Ekaristi, yaani Utangulizi, tunaona ukuu wa mti wa Msalaba wa Yesu Kristo
ambao ni kinyume cha mti wa bustani ya Aden. Mti ule wa bustani ya Adeni
ulikuwa chanzo cha dhambi kwa wazee wetu Adamu na Hawa, wakapoteza uzima wa
kimungu waliokuwa nao. Kumbe kwa njia ya
mti wa Msalaba Yesu, Kristo ametuletea neema yaani uzima wa Kimungu ndani yetu;
tukombolewa.
Pale yalipoanzia mauti yaani dhambi, na uzima uanzie
hapo hapo katika mti, na yule aliyeshinda katika mti, ashindwe pia katika mti
wa Msalaba. Shetani alifautu kuleta mauti kwa kupitia mti wa bustani, kumbe kwa
njia ya mti wa Msalaba uzima na ufufuko umepatikana. Mti wa Msalaba umekuwa mti
wa ushindi kwa njia ya Yesu Kristo.
Tuutukuze msalaba
Kila tunapoadhimisha Liturujia tunaanza kwa kupiga Ishara ya Msalaba. Kwa ishara hiyo tunaumbuka
ukombozi wetu. Kwa kawaida hata katika Sala za kila siku, Mkristo inampasa
kuanza kwa Ishara ya Msalaba na kumaliza kwa ishara hiyo.
Hapana budi kufanya ishara hiyo vizuri na kwa ibada, isije ikawa tu mazoea.
Tena ni vema kuwahimiza Wakristo kuwa na msalaba
angalau msalaba moja katika kila nyumba. Nyumba ya Mkristo inayokosa msalaba
inakosa kitu muhimu sana. Msalaba ulio na sanamu ya Bwana Yesu ubarikiwe na
kuhani na uwekwe barazani au sebuleni ili kuwa ishara ya imani yetu na uwakinge
katika mabaa na kuwaletea Baraka wote. Baraka iwafikie siyo tu wanaoishi katika nyumba, bali hata
wageni na wote waingiao katika nyumba hiyo. Kila Mkristo asiuonee aibu Msalaba
wa Kristo bali aone fahari kuwa nao.
Comments
Post a Comment