MAPADRI WENYE TAMAA WAONYWA
ASKOFU Mkuu wa Jimbo Kuu Katoliki Tabora Mhashamu Paulo
Ruzoka amewaasa mapadri kukaa chonjo na mali za ulimwengu huu unaopita ili
wasiingie matatani na kuipoteza imani yao safi.
Rai hiyo ameitoa hivi karibuni katika adhimisho la Misa
Takatifu na kutoa Sakramenti ya Daraja Takatifu ya Upadri kwa Shemasi Peter
Fabian Kulwa hivi karibuni.
Akitoa mahubiri yake katika Kanisa la Mtakatifu Yosefu Mfanyakazi
Kipalapala Tabora, Askofu Mkuu Ruzoka amewataka mapadri kupeleka upendo wa
Kristo kwa watu wote bila ya ubaguzi wowote.
Amesema Mtakatifu Matayo mtume na mwinjili alikubali kuacha
kazi yake nzuri ya mshahara akakubali kumfuata Kristo, vivyo hivyo na padri
anapoitwa hana budi kuacha yale yote yasiyoendana na wito mtakatifu wa upadri
na kumsikiliza Kristo anachomtaka akifanye kwa watu wake.
Pia Askofu Mkuu Ruzoka amesema wito wa upadri ni zawadi toka
kwa Baba Mungu ambayo padri anazawadiwa bila mastahili yake mwenyewe. Na kama
mtu atasema nataka kuwa padri bila kuitwa na Kristo mwisho wa padri huyo huwa
ni kukata tamaa.
“Padri anaitwa kuadhimisha makuu ya Mungu na si vinginevyo,
hivyo ni vyema ajikabidhi kwa Kristo, na awe tayari kuadhimisha Sakramenti ya
Upatanisho ambayo ndio Kristo alionesha kwa Mtakatifu Matayo na kumwambia
amfuate.”
Aidha katika mahubiri yake Askofu Mkuu Ruzoka amesema sisi
binadamu ni dhaifu hivyo ni vyema tuwe tayari kuhurumiana na kusameheana ili
upendo wa Kristo umfikie kila mwanadamu na kuachana na moyo wa kulipiza kisasi.
Padri
Peter Fabiani Kulwa anakuwa padri wa tatu tangu kuanzishwa kwa parokia ya
Mtakatifu Yosefu Kipalapala. Pamoja na mambo mengine parokia ya
Kipalapala imemzawadia padri mpya gari dogo aina ya Tayota Lav 4 kwa ajili ya
uchungaji.
Comments
Post a Comment