Kanisa linawashukuru watawa wa Moyo Mtakatifu wa Yesu kwa huduma

Mama Kanisa anaadhimisha Jubilei ya Miaka 100 tangu alipofariki dunia Mtakatifu Franciska Xavier Cabrini, Msimamizi wa wakimbizi na wahamiaji ambaye katika maisha na utume wake, ameliachia Kanisa na ulimwengu katika ujumla wake, amana kubwa ya ujumbe wa upendo na mshikamano kwa ajili ya wahamiaji na wakimbizi, ambao leo hii wanaonekana kuwa ni kero kubwa kwa Jumuiya ya Kimataifa. Mtakatifu Franciska Xavier Cabrini alitambua wito wake wa kimisionari kutoka kwa Mwenyezi Mungu, akawaandaa watawa na kuwatuma sehemu mbali mbali za dunia ili kusaidia huduma kwa wakimbizi na wahamiaji, kwa kushirikiana na watawa wa mashirika mbali mbali pamoja na viongozi wa Makanisa Mahalia.
Hii ni sehemu ya ujumbe wa Baba Mtakatifu Francisko aliomwandikia Sr. Barbara Louse Staley, Mama Mkuu wa Shirika la Wamissionari wa Moyo Mtakatifu wa Yesu, ambao kuanzia tarehe 17 hadi tarehe 23 Septemba, 2017 wanaadhimisha mkutano mkuu wa Shirika, huko Chicago, nchini Marekani karibia sana na Madhabahu ya Taifa ya Mtakatifu Franciska Xavier Cabrin, msimamizi wa wahamiaji. Huu ni wito na wakfu unaobubujika kutoka katika sakafu ya Moyo Mtakatifu wa Yesu, kiini cha umisionari unaofumbatwa katika huruma isiyokuwa na kifani. Huyu ni mwanamke wa shoka aliyepandikiza ndani ya watawa wenzake ari na moyo mkuu wa kuganga na kuponya madonda ya walimwengu, kwa kutiwa nguvu na Kristo mwenyewe.
Hii ni kauli mbiu ilimsaidia sana Mtakatifu Franciska Xavier Cabrini kutekeleza dhamana na wajibu wake nchini Italia, Ufaransa, Hispania, Uingereza, Marekani, Amerika ya Kati, Argentina na Brazil. Utume wake uliwaka moto wa huruma na mapendo kwa watu wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii, kwa kujenga nyumba ya wahamiaji huko New Orleans, Louisiana, mwaka mmoja, baada ya baadhi ya wananchi wa Italia kushutumiwa kwa mauaji ya Kamanda mkuu wa Polisi wa mkoa. Utume wa Wacabrini umefumbatwa tangu mwanzo na huduma makini kwa wahamiaji waliotoka Italia, ili kutafuta maisha bora zaidi huko ughaibuni na kama kielelezo cha utii kwa Papa Leo XIII.
Leo hii, utume kama huu unakabiliwa na changamoto pevu, lakini Mtakatifu Franciska Xavier Cabrini alijikita zaidi katika huduma kwa maskini, kwa watoto yatima na wale waliokuwa wanaishi katika mazingira magumu na hatarishi. Akasaidia kulinda na kudumisha Mapokeo ya Kikristo na Ibada sanjari na kuwapatia nafasi ya kushiriki katika maisha ya wananchi wa Amerika kwa kuwa Wamarekani halisi pamoja na kuendelea kubaki kuwa Waitaliani. Wananchi hawa wakawa ni zawadi kwa Kanisa na watu waliowakarimu. Upendo na akili ni mambo makuu mawili yanayofumbata karama ya shirika hili; mambo ambayo yamesaidia sana kukuza na kudumisha umoja na majadiliano na hivyo kuondoa utengano na uadui kati ya watu na kwamba, waamini wote wanayo dhamana ya kuwa kweli ni wafuasi wa Kristo Yesu kwa njia ya ushuhuda wa maisha yao.
Baba Mtakatifu Francisko anakaza kusema, maadhimisho ya Jubilei hii iwe ni fursa ya kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa zawadi hii kubwa ambayo amelijalia Kanisa. Baba Mtakatifu anawaombea ili kweli Shirika hili liweze kupata nguvu ya Roho Mtakatifu ili kuimarisha imani ya kumfuasa Kristo Yesu mintarafu karama ya shirika. Waamini walei waendelee kushiriki na kuwaunga mkono katika dhamana ya uinjilishaji katika mazingira ya jamii ya nyakati hizi. Baba Mtakatifu anawaomba wamkumbuke katika sala na sadaka yao kwa ajili ya maisha na utume wake kama Khalifa wa Mtakatifu Petro, hasa kwa kujisadaka kwa ajili ya ustawi, maendeleo na hatima ya wakimbizi na wahamiaji duniani.
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.
Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.

Comments

Popular posts from this blog

SALA YA ASUBUHI:SALI HIVI..

Ujio wa Wamisionari wa Kwanza Tanzania Bara (2)

MJUE MTAKATIFU MARIA GORETTI