“DINI INAYOHUBIRI FEDHA KULIKO HUDUMA HAIFAI”
MKUTANO Mkuu wa 17 wa Shirikisho la Masista
Wakatoliki nchi za Afrika Mashariki na Kati (ACWECA) umefunguliwa hivi karibuni
jijini Dar es salaam na kuandika historia nchini, ambapo ufunguzi huo
umehudhuriwa na Rais wa Baraza la Kipapa la Maisha ya waliowekwa wakfu Mwadhama
Joao Kardinali Braz de Aviz kutoka Vatikani.
Katika Misa Takatifu ya ufunguzi wa
mkutano huo Kardinali Joao amewaasa watawa wanaounda shirikisho hilo kutomezwa
na tama ya fedha katika utume wao na badala yake wajikite katika kutoa huduma
bila kutegemeamalipo ya hapa duniani.
Amesema kuwa watawa wanapaswa kuwa
kimbilio la watu hasa wale wanaoteseka na kutengwa katika jamii, kwa kuwa
mamlaka waliyonayo watawa ni mamlaka ya kuhudumia wanyonge kwa kuliishi Neno la
Mungu.
“Fedha inaamrisha kilakitu. Fedha ina
nguvu na msukumo mkubwa katika ulimwengu wa leo. Fedha inasababisha vifo,
silaha, hofu na vita. Hatupaswi kuitumikia fedha, bali tunapaswa kumtumikia
Mungu” ameeleza.
Aidha amesema kuwa dini inayohubiri
fedha kuliko huduma haiwezi kuwa dini ya kweli,na kusema kuwa hiyo ni
changamoto kubwa katika ulimwengu wa leo. Pia amesema kuwa haitoshi kwa mtawa
kuishia katika kusoma Biblia tu bali mtawa anapaswa aishi mtindo wa maisha kama
mkristo, kama walivyoishi wafuasi wa Kristo.
Pia amewakumbusha watawa kuishi fadhila
na karisma za waasisi na waanzilishi wa mashirika yao badala ya kujikita katika
mambo mapya yasiyoendana na uhalisia wa maisha ya utawa.
Wakati huo huo Waziri wa Sera, Bunge,
Kazi, Vijana, Ajira na Walemavu Jenister Mhagama amesema kuwa uwepo wa Umoja wa
Masista Afrika Mashariki na Kati umesaidia maendeleo ya nchi hizo na kuwa
sehemu muhimu ya kuimarisha Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC).
Amesema kuwa kupitia mashirika hayo ya
kitawa, miradi mbalimbali nahuduma za kijamii imetekelezwa na hivyo kuharakisha
maendeleo ya nchi zaukanda huo, huku huduma hizo zikitolewa bila kujali tofauti
za dini, rangi na hali za maisha.
Pia
ameziomba Taasisi mbalimbali za dini za Kanisa Katoliki nchini ziendelee
kukuza maadili na utawala bora ili kuliepusha taifa dhidi ya rushwa, dawa za
kulevya, ukimwi na viongozi wasiokuwa waadilifu.
“Mchango mkubwa unaotolewa na watawa ni
bidii yao ya kufanya kazi ya kutoa huduma nchini. Uwepo wa masista umekuwa
chachu ya maendeleo ya Kanisa mahali popote, hakika wao wamekuwa nguzo imara.
Tunawaomba msimamie maadili katika taasisi zenu ili kukuza utawala bora na
maendeleo ya watu” ameeleza.
Mkutano huo wa 17 wa Shirikisho la Masista Wakatoliki nchi za
Afrika Mashariki na Kati (ACWECA) umefunguliwa Agosti 26, 2017 na unatarajiwa
kufanyika hadi Septemba 2, 2017 katika kituo cha mikutano cha Baraza la
Maaskofu Katoliki Tanzania (TEC), Kurasini jijini Dar es salaam.
Umoja huo unaundwa na nchi 9 ambazo ni
Tanzania, Kenya, Uganda, Malawi, Zambia, Ethiopia, Sudani ya Kusini, Sudani na
Eritrea. Baadhi ya wageni waliohudhuria ufunguzi wa mkutano huo ni pamoja na
Askofu wa Jimbo Katoliki Bunda Mhashamu Renatus Nkwande, Askofu Msaidizi wa
Jimbo Kuu Katoliki Dar es salaam Mhashamu Eusebius Nzigilwa, na Balozi wa Papa
nchini Askofu Mkuu Marek Solczyński.
Wakati
huo huo wajumbe wa Mkutano Mkuu wa ACWECA wamefanya uchaguzi na kumchagua Sista
Cesilia Njeri wa Shirika la Wadada wadogo wa Mtakatifu Fransisko wa Asizi kuwa
Mwenyekiti mpya wa ACWECA.
Comments
Post a Comment