WANANCHI KENYA WATAHADHARISHWA
BARAZA
la Maaskofu Katoliki Kenya limewataka wananchi nchini humo kuweka kando tofauti
zao ili kwa pamoja waweze kujenga nchi yao.
Baraza la Maaskofu Kenya limekishukuru Chama cha upinzani cha NASA kwa
kufikisha malalamiko yake ya uchaguzi kwenye Mahakama kuu badala ya kesi hiyo
kusikilizwa na kutolewa hukumu na raia mitaani, hali ambayo ingepelekea
machafuko makubwa ya kisiasa nchini Kenya.
Uamuzi huu umeiongezea Mahakama kuu sifa ya kuweza kutatua migogoro ya wananchi
katika hali ya usalama na amani. Maaskofu wanawaalika wananchi wote wa Kenya
kuzingatia utawala wa sheria kwa kukubali na kutekeleza maamuzi yaliyotolewa na
Mahakama kuu. Uhuru, heshima na haki ya Mahakama kuu vinapaswa kuheshimiwa hata
kama kimsingi mtu hakubaliani na maamuzi yaliyotolewa na Mahakama kuu.
Maaskofu wanampongeza Jaji Mkuu David Maraga kwa maamuzi aliyoyafanya na
kwamba, sasa changamoto iliyoko mbele yao ni kushikamana ili kujenga taifa kwa
kujikita katika nia njema. Baraza la Maaskofu Katoliki Kenya linawasifu na
kuwapongeza wananchi wote waliojitokeza kupiga kura, kwa amani na utulivu na
kuwataka tena kujitokeza kwa wingi wakati wa kupiga tena kura ya marudio hapo
tarehe 17 Oktoba 2017.
Wananchi wa Kenya wanahimizwa kufanya kampeni za kistaarabu,
zinazowajibisha, ili hatimaye, kuwapata viongozi watakaosukuma mbele gurudumu
la maendeleo ya wananchi wote wa Kenya. Baraza la Maaskofu Katoliki Kenya
linavialika vyama vyote kushirikiana na Tume huru ya uchaguzi na mipaka nchini
Kenya, IEBC sanjari na kuiachia uhuru wa kuweza kutekeleza majukumu yake pasi
na kuingiliwa na wanasiasa.
Badala ya kuishambulia Tume huru ya Uchaguzi na Mipaka nchini Kenya,
wanasiasa watoe ushauri wa namna ya kuboresha utendaji wao wa kazi na kwamba,
busara haina budi kutumika kwani si mambo yote yanaweza kufanyiwa marekebisho.
Maaskofu wanaunga mkono mchakato wa mabadiliko kwenye Tume huru ya
uchaguzi na mipaka nchini Kenya, IEBC ili kuwajengea wananchi imani katika
mchakato mzima wa uchaguzi wa marudio hapo tarehe 17 Oktoba 2017.
Comments
Post a Comment