CRS YAWARAHISISHIA HUDUMA YA MAJI WAKAZI KARATU
SHIRIKA la Catholic Relief Services (CRS)
kwa kushirikiana na mdau wake Grundfos Lifelink A/S kupitia Idara
ya Maendeleo ya Jamii Jimbo Katoliki Mbulu (DMDD) limebuni mradi wa kipekee na
wa kwanza nchini Tanzania unaolenga kubadilisha mfumo wa kulipia maji
kutoka malipo ya baada kwa sasa na kuja kwenye malipo ya kabla kwa kutumia
vocha katika utoaji wa huduma ya maji.
Kwa mujibu wa Meneja mradi kutoka
CRS Mhandisi Ephraim Tonya, mradi huo unalenga kuhudumia watu zaidi ya 11,604
kwa awamu ya kwanza kutoka wilaya ya Karatu mkoani Arusha ulioanzia katika
kijiji (1) cha Gongali na mitaa minne (4) Karatu mjini ambayo ni Mjini
kati, Bomani, Mazingira bora na Sabato vinavyohudumiwa na bodi ya KAVIWASU
na kijiji cha Qaru kinachohudumiwa na bodi ya ENDAWASU.
Mhandisi Tonya ameeleza kuwa lengo
la mradi huo wa kulipa maji kabla ni kuwezesha udumisho na uendelevu wa
miradi ya maji, upatikanaji wa huduma muda wote mtumiaji anapohitaji, kuongeza
ufanisi katika ufanyaji kazi wa miundombinu ya maji, kuongeza vyanzo vipya ya
maji pamoja na kuboresha vyanzo vilivyopo.
Amesema mara nyingi katika bodi za
maji kumekuwa na upotevu wa mapato yatokanayo na huduma za maji, hivyo mradi
huo wa malipo kabla kwa kutumia vocha utasaidia kupunguza upotevu huo kutoka
asilimia 39 kwa bodi ya maji ya KAVIWASU na asilimia 34 kwa bodi ya maji ya
ENDAWASU kushuka kwa asilimia 20 bodi zote.
Tonya amesema kuwa upotevu huo
husababisha miradi ya maji kutokuwa endelevu na mingine kufa na kusababisha
waathirika wakuu ambao ni watoto chini ya miaka 5 kukosa afya na kudumaza akili
zao.
Mhandisi Tonya amefafanua kuwa mradi
huo umekuwa na mafanikio makubwa ambapo mradi wa KAVIWASU uliokuwa
unakusanya sh.30,000 kwa mwezi kwa kituo cha umma awali kwa malipo baada, kwa
sasa unakusanya sh.laki mbili kwa mwezi kwa mfumo wa malipo kabla.
Amefafanua kuwa fedha hizo ambazo
hutokana na mradi zinawekwa katika akaunti maalum benki kwa lengo la kutatua
changamoto mbalimbali ikiwemo ukarabati wa miundombinu na pia upanuzi wa huduma
za maji kwa wilaya.
Mhandisi Tonya ameongeza kuwa mradi huo
unafadhiliwa na shirika la Serikali ya Uingereza (UKAID) kupitia shirika la
HDIF kwa awamu ya kwanza kwa maeneo tajwa na katika utekelezaji wake umegharimu
kiasi cha shilingi milioni 630,550,700.
Kwa upande wake mhamasishaji mkuu
kutoka Idara ya Maendeleo ya Jamii Jimbo Katoliki Mbulu (DMDD) Rither Mallewo
ameeleza changamoto mbalimbali wakati wa utekelezaji wa mradi ikiwemo uelewa
mdogo kutoka wa walengwa kutokana na mradi huo kuwa na teknolojia ya kisasa na
wa kwanza nchini Tanzania.
Mallewo amesema kuwa kutokana na
changamoto hiyo ya mradi kuwa wa kwanza Tanzania, waliwapeleka walengwa
kujifunza nchi jirani ya Kenya na baada ya hapo mradi ulijikita zaidi kwa
uhamasishaji ambao ulichukua mwaka mmoja ili kujenga uelewa wa pamoja kwa
walengwa kwa ajili ya udumisho wa mradi huu wa R3W wilayani Karatu.
Naomba mawasiliano ya mhandisi hii teknolojia nmeipenda
ReplyDelete