Papa Francisko na mchakato wa kuwasikiliza vijana wa kizazi kipya!
Baba Mtakatifu Francisko anaendelea kulihamasisha Kanisa kujenga utamaduni wa kuwasikiliza vijana, ili kuwajengea uwezo wa kuwajibika vyema ili hatimaye, waweze kuwa kweli ni wadau katika ujenzi wa Kanisa na jamii inayowazunguka. Kanisa halina budi kujifunza lugha inayogusa sakafu ya mioyo ya vijana wa kizazi kipya! Yataka moyo na ujasiri wa kukaa pamoja na vijana. Hivi ndivyo alivyofanya Baba Mtakatifu Francisko, Jumapili iliyopita, tarehe 17 Septemba, 2017 alipoamua kukaa na kuwasikiliza vijana wapatao 550 kutoka mkoa wa Marche, Italia, waliokuwa wameongozana na Mapadre wa Shirika la Ndugu Wadogo wa Mtakatifu Francisko. Tukio hili la aina yake, liliadhimishwa mjini Vatican, nje kabisa ya ratiba rasmi za Baba Mtakatifu Francisko siku ya Jumapili.
Vijana hawa kutoka Marche walikuwa wanaadhimisha kumbu kumbu ya miaka 20 ya uwepo wao wa pamoja katika mchakato wa malezi na majiundo ya maisha ya kiroho, unaojulikana kama “Giovaninsieme”. Hili ni tukio linalowakutanisha vijana kutoka sehemu mbali mbali za mkoa wa Marche, mwanzoni mwa shughuli za kichungaji. Ni tukio linalowakutanisha wanandoa na familia; vijana na wazee; pamoja na wanandoa waliotalakiana, ili wote kama familia ya Mungu waweze kutembea kwa pamoja!
Tukio la mwaka huu, limepewa uzito wa pekee, kwani limekuwa kama sehemua ya maandalizi ya maadhimisho ya Sinodi ya Maaskofu kwa ajili ya vijana itakayoadhimishwa mjini Vatican, mwezi Oktoba, 2018 kwa kuongozwa na kauli mbiu “Vijana, Imani na Mang’amuzi ya Miito”. Vijana walipigwa na bumbuwazi walipojikuta wakiwa mbele ya Baba Mtakatifu Francisko mjini Vatican aliyewapokea na kuwakaribisha. Vijana hawa tayari walikwisha adhimisha Ibada ya Misa Takatifu iliyoongozwa na Askofu mkuu Fabio Dal Cin, huko Loreto. Baba Mtakatifu alisikiliza “swaga za vijana wa kizazi kipya, nyimbo na shuhuda zao za maisha. Alishuhudia jinsi ambavyo Wakapuchini “walivyojichanganya na vita” kiasi cha kulisakata rumba kwa raha zao wenyewe! Waswahili husema, ama kweli ujana mali!
Baba Mtakatifu amewashukuru na kuwapongeza vijana kwa uwepo na ushuhuda wao; amewapongeza viongozi wa Kanisa wanaoendelea kuimarisha matumaini kwa vijana wa kizazi kipya pamoja na ushuhuda wa Injili ya familia inayofumbatwa katika Injili ya uhai dhidi ya utamaduni wa kifo. Baba Mtakatifu anakaza kusema, inalipa kukaa na kuwasikiliza vijana pasi ya kufanya mahubiri, bali kushirikishana nao rasilimali muda, jambo ambalo ni muhimu sana katika sera na mikakati ya shughuli za kichungaji kwa vijana wa kizazi kipya.
Kwa upande wake Padre Alessandro Angelisanti, amemweelezea Baba Mtakatifu Francisko kwamba, ili ni tukio linalowakutanisha wadau mbali mbali katika maisha na utume wa Kanisa; ili kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu, inayowafunulia watu wote mpango wa Mungu katika maisha yao na baadaye, wamemzawadia Baba Mtakatifu zawadi mbali mbali zinazogusa hija ya maisha yao ya kiroho. Baba Mtakatifu amewataka vijana hawa kuendelea kufanya hija katika maisha ili waweze kupata ukomavu wa kiroho, ili hatimaye, waweze kushiriki kikamilifu katika mchakato wa ujenzi wa Kanisa na jamii katika ujumla wake. Amekazia ushuhuda wa ukarimu katika maisha ya Kikristo; umuhimu wa kujenga na kudumisha utamaduni wa kusikiliza kwa makini na hatimaye, kujibu matamanio halali ya vijana mintarafu mwanga wa Injili pamoja na kuwasindikiza vijana katika malezi na makuzi yao.
Vijana kwa upande wao, wanataka kuthaminiwa na kuheshimiwa na Kanisa; kushirikishwa katika maisha na utume wa Kanisa pamoja na kusikilizwa kwa makini shida na mahangaiko yao ya kila siku. Baba Mtakatifu baada ya chakula cha mchana na mapumziko mafupi, alirejea tena miongoni mwa vijana, ili kushiriki nao furaha, matumaini na changamoto za maisha. Vijana wamefurahishwa na unyenyekevu, uvumilivu na uwepo wa Baba Mtakatifu kati pamoja nao kwa siku nzima, jambo ambalo si rahisi sana. Vijana wameweza kumuuliza Baba Mtakatifu maswali naye akawajibu kwa ufasaha na kuwataka kuendelea kukua na kukomaa katika maisha yao ya kiroho, ili hatimaye, waweze kufanya maamuzi makini katika maisha yao.
Vijana wamegusia maisha ya imani, matumaini na mapendo ya dhati; changamoto za maisha ya ndoa na familia; umuhimu wa kuwa waaminifu katika maamuzi ya maisha na miito yao! Mwishoni, baada ya kusali katika kimya kikuu, Baba Mtakatifu amewataka vijana kutoka kifua mbele kwenda katika barabara za maisha yao bila woga wala makunyanzi kumtangaza na kumshuhudia Kristo Yesu chemchemi ya furaha na matumaini yao!
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.
Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.
Comments
Post a Comment