‘WAZAZI WANAOSALI PAMOJA WANAJENGA MAADILI YA TAIFA’ ASK. KILAINI
ASKOFU Msaidizi wa
Jimbo Katoliki Bukoba Mhashamu Methodius Kilaini amesema kuwa wazazi na
wasimamizi wanapaswa kuwa kitu kimoja na kuwaelekeza watoto wao ili waendelee
kuyashika waliyofundishwa.
Ameeleza hayo
katika Ibada ya Misa Takatifu Parokia ya Watakatifu wote Kiluvya Jimbo Kuu la
Dar es Salaam ambapo vijana 115 wamepokea Sakramenti ya Kipaimara. Katika
mahubiri yake amesema kuwa, Kipaimara ni Sakramenti ya ukomavu na Mafuta ya
Krisma wanayopakwa wana Kipaimara yanaacha
alama isiyofutika, na kupokea Roho Mtakatifu mioyoni mwao.
Aidha, Askofu
Kilaini amesema kuwa kijana anayepata kipaimara tayari ni askari wa Kristo kwa
sababu anayo mawazo mazuri, matendo mazuri, fikra nzuri katika kujituma
kutekeleza tendo lolote linalotendeka kadili ya miongozo ya Kanisa.
“Mwanakipaimara
asione haya kutaja maneno ya Mtume Paulo kuwa kuishi kwangu ni Kristo”
amesisitiza.
Hata hivyo, wazazi
na walezi au wasimamizi wa vijana ambao wamepewa Kipaimara wametakiwa kuendelea
kuwalea vijana hao maana mafundisho waliyoyapata hayatoshelezi hali halisi ya
imani yao bali kuendelea kuwaelekeza katika kumshuhudia Kristo.
“Ili kutengeneza
jeshi la Kristo lazima malezi bora yaanzie ngazi ya familia. Mazingira ya
nyumbani yakiandaliwa vizuri hasa wazazi kwa kusali pamoja, kufanya maamuzi ya
busara kwa pamoja hata na watoto watakuwa na hekima katika kuishi maadili yao”
amesema.
Pia wazazi
wametakiwa kutofumbia macho mambo maovu ambayo yanaweza kuchangia watoto wao
kuzama katika ulimwengu wa maovu na badala yake kuwafundisha vijana wao misingi
ya Kanisa Katoliki na kuishikilia vema katika maisha yao.
Paroko wa Parokia
hiyo Padri Maximilian Wambura, amempongeza Askofu Kilaini kwa kuwa tayari
kuitika mwito wa kufika Parokiani hapo na kuwapa vijana Sakramenti ya
Kipaimara, pia amewashukuru, Makatekista na Mafrateli kwa kazi nzuri ambayo
wameifanya ya kuwaandaa vijana hao. Amewataka wazazi wadumishe mshikamano
katika kuwalea vijana na pia kuendelea kuwahimiza katika kulinda, kusimamia,
kutetea na kulitegemeza Kanisa la Kristo kwa hali na mali.
Comments
Post a Comment