“SITASAHAU UTAJIRI WA LITURUJIA TANZANIA” KARDINALI JOAO
RAis wa Baraza la Kipapa
la Maisha ya waliowekwa wakfu Mwadhama Joao Kardinali Braz de Aviz amewaasa
waamini nchini kudumisha utamadunisho katika maadhimisho ya Misa Takatifu huku
akishangazwa na utajiri mkubwa wa liturujia nchini Tanzania.
Amesema hayo
alipoongoza adhimisho la Misa Takatifu ya ufunguzi wa Mkutano Mkuu wa 17 wa
Shirikisho la Masista Wakatoliki nchi za Afrika Mashariki na Kati (ACWECA),
uliofanyika katika Kanisa la Bikira Maria Mkingiwa dhambi ya asili, Baraza la
Maaskofu Katoliki Tanzania (TEC), Kurasini jijini Dar es salaam.
“Nimestaajabishwa
na namna ambavyo neno la Mungu limeletwa hapa mbele, ukitanguliwa na moto
katika chungu kuonyesha mwanga wa neno la Mungu, huo ni wito kwa watawa
kuliishi neno hilo kwa furaha katika utume wenu. Taswira hii itabakia katika
maisha yangu. Kwa kweli tamaduni zenu zina nguvu mno” ameelezea Kardinali Joao.
Ameongeza kuwa
amefurahishwa na Liturujia nchini Tanzania ambayo inaakisi urithi wa utamaduni
na kukiri kuwa liturujia hiyo ni tofauti sana na ile anayoishuhudia akiwa
Vatikani.
“Nimefurahishwa na
urithi wa utamaduni katika Liturujia yenu, hii ni tofauti sana na kile
nachokiona kule Vatikani. Utamaduni wenu na karama viende sambamba, kamwe
msiviache” amesisitiza.
Comments
Post a Comment