Kard.Pengo aikabidhi serikali mradi wa kisima
KANISA Katoliki Jimbo
Kuu la Dar es salaam limekabidhi mradi wa kisima kwa serikali, katika kituo cha
mafunzo kwa watoto (mahabusu ya watoto) cha Upanga jijini Dar es salaam, huku
serikali ikiazimia kujifunza kupitia jitihada za Kanisa katika kujenga jamii ya
watanzania yenye maadili, upendo na kujali wengine.
Akikabidhi mradi
huo kwa niaba ya watoto wa Shirika la Kimisionari la Utoto Mtakatifu, Askofu
Mkuu wa Jimbo Kuu Katoliki Dar es salaam Mwadhama Polycarp Kardinali Pengo
amesema kuwa Kanisa linajikita katika utoaji wa huduma za kijamii kuonyesha
kuwa linaunga mkono jitihada za serikali katika kuandaa taifa adilifu
linaloongozwa na upendo bila kujali tofauti za uchumi, siasa au dini, kwa
manufaa ya watanzania wote.
“Watoto ndiyo
tumaini la kila taifa. Kadiri tunavyokuwa na watoto wenye maadili, wale
wanaojua kipi kifanywe ili kujenga taifa, tunaweza kuwa na matumaini kwa taifa
la kesho. Kuonyesha kwamba Kanisa hatuko mbali na serikali yetu katika kujenga
yale yanayokua ya manufaa kwa taifa letu ndiyo maana tunafanya haya yote. Sisi
tuna sehemu yetu, kimacho au kimwili inaweza kuonekana ni sehemu ndogo
kulinganisha na kinachofanywa na serikali. Lakini kidogo kile tunachoweza
kuchangia, daima tunakichukulia kama ishara ya nje ya hali iliyokuwa kubwa
zaidi kutoka moyoni” amesema.
Aidha ameongeza
kuwa lugha pekee inayozungumzwa na Kanisa ni upendo, ndiyo maana wanapotoa
huduma mbalimbali za kijamii hawaulizi dini ya mtu, bali wanasaidia wote kwa pamoja, ili kuwafunza umuhimu wa
kuwa wamoja.
Akipokea mradi huo
uliogharimu Milioni 11, 780, 000/=, Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia,
Wazee na Watoto Ummy Mwalimu amesema kuwa serikali itaendelea kuthamini na
kujifunza kupitia jitihada zinazofanywa na Kanisa Katoliki katika kujenga jamii
ya watanzania yenye maadili, upendo, na kujali watu wengine.
“Napenda kutoa
shukrani zangu kwa niaba ya serikali kwako wewe Baba Mwadhama kwa kufikiria
kutuwezesha kupata huduma hii muhimu kwa watoto. Tumesikia kuwa unakuwa
unawaelekeza watoto, walezi wao na wazazi kufanya matendo mema. Mimi ni mtu wa
imani tofauti ila nataka kukiri kwamba Kanisa Katoliki linatusaidia sana katika
kujenga jamii ya watanzania yenye maadili yenye upendo, yenye kujali watu
wengine” ameeleza.
Pia ameliomba
Kanisa liendelee kushirikiana na serikali katika kuwasisitiza watanzania hasa
wazazi na walezi, watimize wajibu wa malezi kwa watoto wao. Amesema kuwa malezi
bora kwa watoto yatasaidia kutokomeza ukatili wa kijinsia kwa watoto, kwani
wanaofanya vitendo hivyo ni watu wa karibu na watoto, ambao wanapaswa kuwa
walinzi.
“Tutaendelea
kutambua mchango mkubwa wa Kanisa katika kutatua changamoto na kero
zinazowakabili watanzania. Kila mwezi tulikuwa tunatumia takribani shilingi
laki nne kwa ajili ya kulipia bili za maji. Maana yake kukamilika kwa mradi huu
tutaweza kuokoa shilingi laki nne kila mwezi, na kwa mwaka ni takribani ni
shilingi milioni 4 na laki 8, tunawashukuru sana” ameeleza.
Aidha Waziri
Mwalimu amewathibitishia watoto walio katika kituo hicho uhakika wa matibabu
yao kwa mwaka mzima, kwa kuwapatia bima ya afya inaitwa toto afya card.
Ushauri
wa Padri Nyasulu waitea taswira mpya kwa Taifa
Katika hatua
nyingine Mkurugenzi wa Shirika la Kimisionari la Utoto Mtakatifu Jimbo Kuu
Katoliki Dar es salaam, Padri Timothy Nyasulu ameomba kuangalia uwezekano wa
kuacha kutumia jina ‘mahabusu’, kwa kuwa maana hiyo ina mwelekeo wa unyanyapaa,
ushauri ulioungwa mkono na Kardinali Pengo na Waziri Ummy Mwalimu, ambaye
ametoa agizo kwa Taasisi ya Kiswahili nchini kutafuta neno linalofaa.
“Nakubaliana na
Padri Timothy kwamba kuita mahabusu inaweza ikawa kama tunazidi kuwanyanyapaa
watoto. Kwa jina la kiingereza tunaita retention home. Kwa kiingereza haileti
ukakasi, kwamba ni sehemu ambayo tunawazuia watoto ambao wapo katika mkinzano
na sheria, kwa hiyo tutawaomba wenzetu wa taasisi ya Kiswahili Tanzania
watutafutie jina zuri la Kiswahili”
Chimbuko
la kukabidhi mradi huo
Mnamo Desemba 3,
2016 Askofu Msaidi wa Jimbo Kuu Katoliki Dar es salaam Mhashamu Eusebius
Nzigilwa akiambatana na watoto wa Shirika la Kimisionari la Utoto Mtakatifu wa
Parokia ya Kurasini, walitembelea kituo cha mafunzo cha watoto Upanga na
kukabidhi zawadi mbalimbali zilizotokana na michango ya watoto hao.
Hapo ndipo Afisa
Mfawidhi wa Mahabusu hiyo ndugu Ramadhan Yahaya alipotaja kero inayohitaji kupatiwa
ufumbuzi wa haraka kuwa ni kero ya maji kwa ajili ya matumizi ya kila siku.
“Tangu nimekuja
kituo hiki miaka mitatu iliyopita, kituo kinakabiliwa na changamoto ya ukosefu
wa maji. Tunadaiwa bili kubwa zaidi ya shilingi milioni 5, hadi kupelekea kukatiwa
huduma ya maji” alieleza ndugu Yahaya.
Baada ya kusikiliza
kero hizo, Askofu Nzigilwa mara moja aliagiza kufanyika kwa tathmini na
upembuzi yakinifu ili kuona uwezekano wa kuchimba kisima kwa ajili ya kutatua
changamoto ya upatikanaji wa maji. Na Agosti 21, 2017 zoezi la kukabidhi mradi
wa kisima hicho kwa serikali likakamilika, ikiwa ni mwendelezo wa utoaji huduma
kwa jamii, unaofanywa na Kanisa Katoliki nchini kwa zaidi ya miaka 150 sasa.
Comments
Post a Comment