Kanisa halitadhoofishwa-Ask Ndimbo
ASKOFU wa
Jimbo Katoliki Mbinga na Mwenyekiti wa Huduma za Jamii kwa upande wa Elimu,
katika Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania (TEC), Mhashamu John Ndimbo amesema
kuwa, licha ya vikwazo na changamoto wanazokutana nazo katika jitihada za
kumkomboa mtanzania dhidi ya ujinga, Kanisa Katoliki halitarudi nyuma wala
kudhoofishwa kwa kuwa utoaji wa elimu ni sehemu ya kazi ya uinjilishaji ya
Kanisa.
Ameeleza
hayo hivi karibuni wakati akifungua Mkutano wa Mwaka wa Makatibu wa Elimu
kutoka Majimbo Katoliki Tanzania, uliofanyika TEC Kurasini jijini Dar es
salaam. Askofu Ndimbo amesema kuwa siku zote uwepo wa Kanisa Katoliki
unatambulishwa kwa uwepo wa huduma za kijamii na kusema kuwa hakuna
uinjilishaji pasipo makuzi ya kitaaluma.
“Elimu
ndiyo inayomfanya mwanadamu kwanza ayajue mazingira yake, ajitambue yeye ni
nani na kisha imfahamishe uhusiano wake na Mungu. Miaka 150 ya Uinjilishaji
Tanzania Bara inapata maana zaidi kwa jinsi sekta ya elimu ilivyokua katika
taasisi zetu. Taasisi zetu za elimu ni wakala mashuhuri wa uinjilishaji”
amesema Askofu Ndimbo.
Pia
amewakumbusha makatibu hao kusisitiza malezi ya vijana kutoka moyoni, kwa
kuwarithisha tunu za maisha kimwili na kiroho. Amesema kuwa mabadiliko ya mfumo
wa elimu hasa kwa wanafunzi wanaotoka sekondari kwenda Vyuo Vikuu ambao
wanalazimika kuomba moja kwa moja katika vyuo husika, hayapaswi kudhoofisha
Vyuo Vikuu vya Kanisa Katoliki bali iwe fursa kwao katika kuwalea watoto
wafaulu vizuri na kuwahamasisha waendelee na masomo katika vyuo vya Kanisa.
Awali
akiwakaribisha wajumbe wa mkutano huo, Naibu Katibu Mkuu wa TEC Padri Damian
Dulle amesema kuwa Kanisa linapoadhimisha jubilee ya miaka 150 ya Uinjilishaji
Tanzania Bara, linajivunia mchango wake katika utoaji wa elimu, hasa kuongezeka
kwa shule na ufaulu.
Comments
Post a Comment