DUMISHENI AMANI-RAIS MAGUFULI
RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania John Magufuli, amewataka
watanzania wote kutunza amani ya nchi ambayo ndio tunu ya Taifa ikiwa ni pamoja
na kuiunga mkono Serikali ya awamu ya tano katika utendaji wake.
Kauli hiyo imetolewa hivi karibuni
Mjini Dodoma na Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali
za mitaa, George Simbachawene kwa niaba ya Rais katika ibada ya
kusheherekea Jubilei ya Miaka 100 ya
Upadri Tanzania Bara iliyofanyika katika eneo la Hija Kata ya Miyuji Manispaa
ya Dodoma.
Aidha Waziri Simbachawene amesema
kuwa Serikali inaendelea kuuenzi mchango wa taasisi za kidini ambao umekuwa
ukitolewa kwa jamii hususani katika masuala ya elimu, afya na maendeleo ya
jamii kwa ujumla.
Hata hivyo amezitaka taasisi mbalimbali za kidini nchini kuwekeza katika
viwanda ili kufikia uchumi wa kati wa viwanda kwa kutoa ajira kwa vijana.
Mbali na hayo amewataka watanzania kuwa waadilifu na waaminifu kwa
Serikali yao kwa yale mema ya kimaendeleo ambayo yanafanywa.
Kwa upande wake Rais wa Baraza la Maaskofu Katoliki nchini Burundi
Askofu Mkuu Joakim Kambanda amewataka
mapadri nchini kujali umuhimu wa nafasi yao katika jamii.
Amebainisha kuwa mapadri wa kwanza katika nchi za Burundi na Rwanda
walilelewa Tanzania na hivyo kuwahamasisha kujali umuhimu wa ukuhani wakati
wote.
“Tukio hili ni la kihistoria, hata sisi tumehamasika kuiga hasa kwa kuwa
mapadri wa mwanzoni kabisa nchini mwetu wamelelewa Tanzania,” amesema Askofu
Joakim wa Burundi.
Sherehe hizo za Jubilei ya Miaka
100 ya Upadri Tanzania Bara zimehudhuriwa na waamini mbalimbali wakiwemo
viongozi wa kisiasa na Serikali.
Comments
Post a Comment