MKUTANO MKUU WA 17 ACWECA KUFANYIKA TANZANIA
UMoja wa Mashirika ya
Watawa wa Kike Afrika Mashariki na Kati, (ACWECA) kufanya Mkutano Mkuu wa
17 Katika Baraza la Maaskofu Katoliki
Tanzania( TEC) Kurasini jijini Dar es Salaam.
Katibu Mkuu wa
umoja huo Sista Eneless Chimbali
amethibitisha kwamba Mwadhama João Kardinali Bráz de Aviz ndiye atakayeongoza
Ibada ya Misa takatifu ya ufunguzi wa Mkutano huo wa 17 wa ACWECA Agosti 27, maaskofu wengine
kutoka nchi wanachama, Msimamizi wa Maisha ya wakfu kutoka Vatikani na Rais wa
Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania Mhashamu Tarcisius Ngalalekumtwa
watahudhuria.
Mkutano huo wa
juma moja utaanza Agosti 26 hadi
Septemba 2 mwaka huu ukiongozwa na kauli mbiu: “Kuimarisha umoja wetu katika
uinjilishaji wa kina katika mazingira ya sasa.”
Rais wa Umoja huo,
Sista Priscar Matenga amesema kuwa, dhamira ya mkutano huo inatoa mwito kwa
wanachama wa ACWECA Kuimarisha umoja na kusherehekea umoja wao.
“Tupo na tunaishi
katika ulimwengu uliounganishwa kama kijiji kimoja na mambo yanabadilika kwa haraka na sisi kama watawa lazima turejee
na kutafakari maisha yetu kwa pamoja na kuona mambo kama vile Kristo
alivyoyaona, kwa hiyo tunahitaji ushirikiano kujiimarisha kwa ajili ya
kuinjilisha. Hivyo, tunawasisitiza wanachama
kujiuliza, nini hitaji letu katika nyakati hizi? Tunataka kueleza nini,
tufanye nini ili kujiunganisha pamoja kama wanachama wa ACWECA ili utume wetu
uzae matunda yanayohitajika na kizazi cha leo
na watu tunaokutana nao katika maisha yetu ya siku?” amesisitiza Sista
Matenga.
Katibu Mkuu wa
Umoja huo, Sista Eneless Chimbali
ameelezea pia umuhimu wa umoja huo akisema kuwa, baadhi ya nchi wanachama wa
ACWECA wanazo rasilimali nyingi zaidi ya wengine hivyo umoja wao utasaidia
wanachama wengine walio katika nchi zilizo na upungufu wa rasilimali hivyo kufikia malengo yao hayo kuliko kila
watawa wangebakia katika nchi zao tu.
Amesema, “Wajibu
wa Umoja wetu ni kukuza ari ya
ushirikiano na kushirikishana maisha ya kiroho, wanadamu na uchumi kati ya
wanachama na na kuimarisha malezi ya utawa, uwezo wa uongozi kwa Uinjilishaji
wa kina,” amesema.
Aidha ameeleza
kuwa, Mkutano huo utawajumuisha wamama wakuu kutoka nchi mbalimbali wanachama,
hivyo watapata fursa ya kufahamiana, kufarijiana na kupeana moyo katika kazi ya
kuinjilisha.
Pamoja na mambo
mengine ametaja moja ya mada zitakazojadiliwa kuwa ni : Watawa wa Kike wa
Kanisa Katoliki kama mabingwa wa Malengo ya Maendeleo Endelevu (SDGs).
“Umoja wa Mataifa
daima huzungumzia kuhusu SDGs lakini mara nyingi sisi watawa hususani wa kike
tunakwepa jukumu hilo bila kutambua kwamba watawa ndiyo wanaohusika wa shughuli
hizo za maendeleo,” amesema.
Amesema
majadiliano ya mada hiyo yatawasaidia watawa kuanza kuandika baadhi ya shughuli
wanazofanya ili waweze kukubali
kikamilifu SDGs.
Katibu Mkuu pia
ameeleza kuwa masista wengine wawili watafafanua zaidi dhumuni la Mkutano huo
mkuu ili kuwasaidia watawa kuelewa zaidi.
Sista Mary Abut
mwanachama wa Bodi ya umoja huo amesema kuwa, dhamira ya mkutano huo ni matokeo ya tafakari na sala ndefu ya
wanachama wa ACWECA.
“Suala la
Uinjilishaji siyo jambo jipya kwa wanachama lakini uinjilishaji mpya
unaohitajika katika ulimwengu wa sasa ni tofauti na wa zamani. Hivyo Wanachama
walitaka dhamira itakayowawezesha kutafakari njia bora za uinjilishaji wa sasa
katika Kanda ya Mashariki na Kati,” Amesema Sista Abut.
Aidha ameeleza
kuwa, mkutano huo ni muhimu kwa watawa kwani utakuwa kama jukwaa la kutathmini
majumuisho ya Mkutano Mkuu wa 16.
“Mkutano huo
utatusaidia kujua kama mapendekezo ya Mkutano wa 16 yamefanyiwa kazi,
yamefanikiwa au la na nini kilitufanya tufanikiwe ili tusiendelee na changamoto
hizo kwa miaka mitatu ijayo,” Amesema Sista Mary.
Taarifa kutoka
Ofisi ya Mawasiliano ya ACWECA zinafafanua kuwa mada nyingine zitakazotolewa ni
pamoja na Uongozi wa ufanisi kwa maisha endelevu, ya watawa,
“Masuala ya
Uongozi na malezi endelevu hususani uchumi
ni mambo ya msingi kwa watawa ili wajue namna ya kufanya biashara
endelevu.
Suala la Uongozi
na malezi ni sehemu ya kwanza ya mpango Mkakati wa 2017-2022 wa ACWECA.
“Malezi ni suala
nyeti na ndio kipaumbele cha maisha ya utawa. Lazima tuwaandae watawa wetu
ipasavyo ili waishi maisha ya wakfu ipasavyo na kutumikia kikamilifu,” amesema
Katibu Mkuu wa Umoja huo Sista Chimbali.
Ifahamike kuwa
wanachama wa ACWECA ni watawa kutoka Ethiopia, Kenya, Uganda, Malawi, Tanzania
na Zambia.
Comments
Post a Comment