Papa Francisko atuma salamu za rambi rambi nchini Sierra Leone
Baba Mtakatifu Francisko amesikitishwa sana na maafa makubwa ambayo yameikumba familia ya Mungu nchini Sierra Leone, Jumatatu, tarehe 14 Agosti 2017 kiasi cha kusababisha watu zaidi ya 400 kufariki dunia na wengine 600 hawajulikani mahali walipo pamoja na uharibifu mkubwa wa makazi ya watu na miundo mbinu mjini Free town. Baba Mtakatifu katika salam za rambi rambi zilizoandikwa kwa niaba yake na Kardinali Pietro Parolin, Katibu mkuu wa Vatican kwenda kwa Askofu mkuu Charles Edward Tamba wa Jimbo kuu la Free Town, anasema, anapenda kuwahakikishia sala na sadaka yake, wale wote walioguswa na kutikiswa na maafa haya!
Papa Francisko anawaombea faraja na nguvu kutoka kwa Baba wa mbinguni, ili kuweza kukabiliana na kipindi hiki kigumu katika historia na maisha ya wananchi wa Sierra Leone. Baba Mtakatifu anapenda kuwatia shime wale wote wanaoendelea kujisadaka kwa ajili ya kuokoa maisha ya watu ambao bado wamefukiwa na maporomoko ya udongo; anawatia moyo wale wote wanaoendelea kutoa msaada wa hali na mali kwa ajili ya kuwasaidia waathirika katika kipindi hiki kigumu! Taarifa kutoka Sierra Leone zinaonesha kwamba, Serikali kuanzia tarehe 16 Agosti 2017 imeanza Juma zima la maombolezo kwa ajili ya kuwakumbuka na kuwaombea wale wote waliofariki dunia katika maafa haya. Takwimu zilizotolewa na Chama cha Msalaba Mwekundu zinaonesha kwamba, kuna zaidi ya watu 3, 000 hawana makazi baada ya nyumba zao kubomolewa au kufunikwa kwa udongo!
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.
Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.
Comments
Post a Comment