MAAGIZO YA HATI YA LITURUJIA KWA WANA KWAYA NA WATUNZI

Na Pascal Mwanache

TUNAENDELEA kuangazia changamoto mbalimbali zinazoukabili Muziki Mtakatifu na hata kuleta ukakasi kwa waamini na watu wenye mapenzi mema. Uchambuzi huu unalenga kutoa mwanga kwa watunzi, wanakwaya, waamini na wakleri, ili kwa pamoja tuelewe mipaka ya utume wa uimbaji na hivyo kutunza hadhi ya muziki huo ulio tunu bora.
Na moja ya miongozo inayotoa mwelekeo sahihi wa utume huu wa uimbaji ni ile Hati ya Liturujia (Sacrosanctum Concilium), ambayo ni maelekezo yaliyotolewa na mababa wa Mtaguso Mkuu wa pili wa Vatikani. Basi tuendelee kujishibisha kwa maagizo hayo, yatujenge na yatukomaze katika utume wetu.

Uwepo wa Kristo katika Liturujia
Tunaambiwa kuwa katika adhimisho la Misa Takatifu, Yesu mwenyewe yupo na anajumuika na kundi la waamini. Hivyo kwa kutambua kwamba katika adhimisho hilo tunaungana na Kristo mwenyewe, ni wazi kuwa tunapaswa kufanya yote kwa uchaji mkubwa, unyenyekevu na unyamavu mtakatifu.
Kwa hivyo hata namna ya kuimba, au aina ya nyimbo tunazoziimba katika misa ni lazima zidhihirishe heshima, uchaji, unyamavu na kilele cha sala kwa Bwana wetu Yesu Kristo. Hati ya liturujia inasema:
“7. Kusudi kutimiza tendo kubwa namna hii, Kristo yupo daima katika Kanisa lake, kwa jinsi ya pekee katika maadhimisho ya kiliturujia. Yupo kwenye Sadaka ya Misa katika nafsi ya kasisi, ‘Yeye ambaye, akijitoa mara moja msalabani, anajitoa tena mwenyewe kwa huduma ya mapadre’
Kwa hiyo kila adhimisho la kiliturujia, kwa kuwa ni tendo la Yesu Kristo Kuhani na la Mwili wake, ndilo Kanisa, ni tendo takatifu kupita yote na hakuna tendo jingine la Kanisa linalofanana nalo kwa manufaa kwa kiwango kilekile na kwa daraja ileile”.
Tujitathmini sasa, tunaimba kwa uchaji au tunapiga kelele na kufanya fujo? Je kwa kuimba kwetu, kweli tunaungana na Kristo katika liturujia?

Muziki mtakatifu ni shirikishi: lazima waamini washiriki kikamilifu
Kama nilivyowahi kueleza hapo awali, kazi ya wanakwaya siyo kuimba. Kazi ya waimbaji wa muziki mtakatifu ni kuwasaidia waamini wasali vizuri ili Mungu atukuzwe na mwanadamu atakatifuzwe. Ili hayo yatimie, ni lazima waamini washiriki kikamilifu katika matendo yote ya liturujia ikiwa ni pamoja na kuimba na kuitikia zaburi na viitikizano.
Lakini hali iko tofauti katika makanisa mengi hapa nchini. Waamini wamefanywa mabubu na watazamaji tu, kwa kuwa nyimbo zinazoimbwa katika misa hazifahamiki. Yaani kila dominika ni nyimbo mpya, tena ngumu ambazo hazishikiki kirahisi. Hali hii haiwasaidii waamini kusali vizuri na kufikia lengo la kuwepo kwa muziki mtakatifu. Katika hili, hati ya liturujia inaagiza hivi:
“30. Ili kuwawezesha waamini washiriki kimatendo, mashangilio ya waamini, maitikio, kuimba zaburi, antifona, nyimbo, vitendo, ishara na mkao wa mwili vitiliwe maanani. Unyamavu mtakatifu utumike pia, wakati unapodaiwa.
113. Tendo la Liturujia hupata kuwa na heshima zaidi wakati linapoadhimishwa katika sherehe kwa kuimba, wakiwepo makasisi na kwa ushirikiano hai wa waamini.
118. Nyimbo za kidini za (wakristo) wenyeji zihimizwe kwa bidii, ili katika ibada mbalimbali za watu na pia katika matendo ya Liturujia sauti za waamini ziweze kusikika vizuri, kadiri ya utaratibu na madai ya miongozo”.

Muziki ni sala: Tunga na imba huku ukisali
Moja ya mambo ambayo watunzi wa mwanzo hapa nchini walifaulu basi ni kutunga wakiwa katika hali ya sala. Nyimbo zao zilikuwa tafakari tosha inayomuingiza muumini katika hali ya sala.
Ndiyo maana hata ukisikia nyimbo kama Roho yangu (E. Nyundo), Bwana Yesu waniita (Padri Mutajwaha), Nimtume nani (Padri Ntapambata) nk, unaonja yale yanayoimbwa humo kuwa ni sehemu ya maisha yako ya ukristo.
Tungo za leo ni kizunguzungu. Chaguzi za maneno hufanywa kwa hisia tu na siyo sala. Melodia zinazotumika humpeleka mtu katika tamasha, sehemu za burudani au mitaani badala ya kumfikisha mbele ya Ekaristi Takatifu. Zaidi ya hapo, hapaswi kuishia katika kuimba tu. Bali uimbaji umsaidie katika kumfikisha katika kilele cha sala. Tunaagizwa na hati ya liturujia kufanya yafuatayo:
“121. Watunga muziki, wakisukumwa na roho ya kikristo, wajione kuwa wameitwa kuustawisha muziki mtakatifu na kukuza hazina yake.
Pia watunge melodia zinazolingana na sifa za muziki mtakatifu na ambao unaweza kuimbwa si tu na kwaya kubwa, bali pia na kwaya ndogo. Tena ziwasaidie waamini wote kushiriki kikamilifu.
Maneno yaliyomo katika nyimbo yalingane na mafundisho ya Kanisa katoliki, zaidi yachukuliwe hasa katika Maandiko Matakatifu na vitabu vya liturujia”.

Muziki unadai elimu ya teolojia: Jifunze
“115. Jitihada kubwa ifanyike ili kuhamasisha elimu na mazoezi ya muziki katika seminari, katika nyumba za unovisi za mashirika ya kiume na ya kike, katika nyumba za wanafunzi, kama vile vyuo na shule za kikatoliki; ili kupata elimu hii, walimu waandaliwe kwa bidii kubwa, kisha watumwe kufundisha muziki mtakatifu. Ikiwa inafaa, uundaji wa Taasisi za Juu za muziki mtakatifu uhimizwe.
Wanamuziki, wanakwaya, na juu ya wote watoto, wapewe elimu halisi ya kiliturujia”

Biblia na uimbaji
Hatuna haja ya kuvamia maneno ya mtaani au kuzidiwa na muziki wa kidunia. Tunayo hazina kuu isiyokauka, ambayo kwayo tunapata maneno yanayotutafakarisha vya kutosha. Watunzi na waimbaji, tumieni Biblia Takatifu. Yako mengi ya kujifunza humo. Maneno ya mtaani tuwaachie wengine. Tunaagizwa hivi:
“24. Jambo muhimu kuliko yote katika adhimisho la Liturujia ni Maandiko Matakatifu, maana katika hayo huchukuliwa masomo ya kusomwa na kufafanuliwa katika mahubiri, na pia zaburi zinazoimbwa.
Sala, maombi na nyimbo hupata uvuvio toka Maandiko, kama vile toka Maandiko matendo na ishara hupata maana. Kwa hiyo, ili kufaulu kufanya marekebisho na maendeleo na malinganisho ya Liturujia, ni lazima kuhimiza ule upendo mtamu na hai wa Maandiko Matakatifu, ambao unashuhudiwa na mapokeo mastahiki ya Makanisa ya Mashariki na ya Magharibi”.

Mchambuzi 0657835343


Comments

Popular posts from this blog

SALA YA ASUBUHI:SALI HIVI..

Ujio wa Wamisionari wa Kwanza Tanzania Bara (2)

MJUE MTAKATIFU MARIA GORETTI