JINSI MAPADRI WALIVYOIKOMBOA TANZANIA



n Na Pascal Mwanache
UJENZI wa amani nchini, kuboresha huduma za kijamii na uokoaji wa roho za watanzania ni moja ya mambo yaliyotajwa kama mchango uliotolewa na mapadri Tanzania, tangu mapadri wa kwanza wazalendo wapewe Daraja Takatifu ya Upadri miaka 100 iliyopita hapo Agosti 15, 1917. 

Hayo yameelezwa na watu mbalimbali katika Misa Takatifu ya Kilele cha Jubilei ya Miaka 100 ya upadri Tanzania, maadhimisho yaliyofanyika katika Kanisa Kuu la Mtakatifu Paulo wa Msalaba na vkituo cha hija cha Mbwanga, Jimbo Kuu Katoliki Dodoma. 

Akitoa homilia katika Misa hiyo Askofu Msaidizi wa Jimbo Katoliki Bukoba Mhashamu Methodius Kilaini amesema kuwa kwa miaka 100 padri amekuwa funguo wa ukombozi, ambapo amewaingiza wanadamu katika fumbo la ukombozi kwa ubatizo, huku akiponya na kuurudisha uhusiano wa mwanadamu na Mungu kwa njia ya Sakramenti ya Kitubio. 

“Padri ndiye ufunguo wa ukombozi kwa sababu bila yeye milango yote imefungwa na hazina zote zilizomo, kwa sababu anaingiza binadamu katika ushirika wa ukombozi kwa Ubatizo, anamtibu anapougua kwa dhambi kwa Sakramenti ya Kitubio, anampa chakula cha uzima ambaye ni Bwana wetu Yesu Kristo katika Ekaristi Takatifu, anaunda familia kwa kushuhudia na kubariki pingu za Ndoa Takatifu, anampa tumaini na nguvu mgonjwa kwa Sakramenti ya Mpako na mwishoni anamfungia pamba ya njiani au viatiko ya mwisho anapokufa na kwenda kwa Baba mbinguni” amesema Askofu Kilaini. 

Aidha ameongeza kuwa kupitia Sakramenti ya Daraja Takatifu, Kanisa Katoliki nchini lilimpa mwafrika hadhi, uwezo na elimu sawa na mzungu, jambo ambalo halikuwa rahisi kwa kuwa mapadri wa kwanza nchini walipatikana wakati wa ukoloni. 

“Miaka 100 iliyopita sehemu kubwa ya Afrika ilikuwa chini wa wakoloni. Wakoloni wengine walitia mashaka hata utu wa Mwafrika na kwa mantiki hiyo walimdhalilisha sana. Ni wakati huo Kanisa Katoliki liliwapa hadhi kubwa sana waafrika kuwafanya mapadre sawa kama wazungu. Hili halikuwa rahisi. Tumshukuru Askofu wa Vikariati ya Nyanza ya Kusini John Joseph Hirth ambaye aliamini sana katika uwezo wa Mwafrika “ ameongeza.
 
Askofu Kinyaiya awaasa vijana 
Kwa upande wake Askofu wa Jimbo Kuu Katoliki Dodoma Mhashamu Beatus Kinyaiya amewataka vijana kutodanganyika na ulimwengu na badala yake wafuate aina ya maisha waliyoitiwa na Mungu. Pia ametoa rai kwa wazazi na walezi nchini kutokuwa vikwazo kwa watoto wao wanapohitaji kujiunga na malezi kwa ajili ya kuwa mapadri.
“Kuna baadhi ya wazazi wanakuwa vikwazo kwa watoto wenye miito ya kuwa mapadri. Msiingilie kazi ya Mungu kwa kuweka maslahi yenu mbele. Waacheni watoto wafuate sauti ya Mungu. Pia muone sasa umuhimu wa kulitegemeza kanisa mahalia” amesema.
Ameeleza kuwa tangu mwaka 1917 walipopadrishwa mapadri wa kwanza nchini, jumla ya mapadri 3316 wamepatiwa Daraja Takatifu ya Upadri, ambapo kati yao 2926 ni mapadri wanajimbo na mapadri 390 wakiwa wanashirika. Amewaomba maaskofu kuendeleza roho ya kimisionari kwa kushirikiana na kushirikishana mawazo na rasilimali mbalimbali walizojaliwa katika utume wao.

Balozi wa Papa ajitambulisha
Naye Balozi wa Baba Mtakatifu nchini ambaye amehudhuria maadhimisho hayo na kujitambulisha rasmi kwa waamini, Askofu Mkuu Marek Solczyński, amewaasa mapadri kujibidiisha katika kutafuta utakatifu wa maisha, kama ambavyo Kristo mchungaji mwema alivyowaamini na kuwapatia utume huo.
Amewaasa kujidhatiti katika kutunza usafi wa moyo na kusali ili waweze kupambana na changamoto mbalimbali wanazokabiliana nazo huku akitoa rai kwa jumuiya ya waamini kusali kwa ajili ya kuombea miito mbalimbali nchini hasa ya upadri na ya maisha ya wakfu.
Ametumia fursa hiyo pia kukabidhi barua ya utambuzi kutoka kwa Katibu Mkuu wa Vatikani Kardinali Pietro Parolin, kwenda kwa Rais wa Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania (TEC), ambapo imepokelewa na Makamu wa Rais wa TEC Askofu Mkuu Beatus Kinyaiya.
Serikali yakiri mchango wa mapadri katika ujenzi wa amani nchini
Kwa upande wake mwakilishi wa Rais John Magufuli katika maadhimisho hayo, Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais anayeshughulikia Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, George Simbachawene amekiri kuwa uwepo wa mapadri nchini umetoa athari chanya katika uhai wa Taifa la Tanzania, huku wakishiriki katika mambo muhimu hususani ujenzi wa amani.
“Historia ya nchi yetu haiwezi kusemwa bila kutaja Kanisa Katoliki. Huduma mnazozitoa zimefanya nchi yetu iwe kama ilivyo. Mmeshiriki katika mambo muhimu ikiwemo ujenzi wa amani, kuboresha huduma za kijamii kama elimu, afya na huduma nyingine zilizoistawisha Tanzania” amesema Simbachawene.
Ameongeza kuwa ni kupitia katika Sakramenti ya Upadri Tanzania itaendelea kuimarika na kuwa nchi ya mfano. Ametumia fursa hiyo kuliomba Kanisa Katoliki liwekeze katika viwanda ili kufanikisha upatikanaji wa ajira kwa watu wengi na upatikanaji wa bidhaa, huku akisema kuwa serikali itawapa ushirikiano walio tayari.

Yaliyojiri
Ibada ya Misa Takatifu ya kilele cha jubilei ya miaka 100 ya upadri nchini imeongozwa na Askofu Mkuu Protase Rugambwa, Katibu Mwambata wa Baraza la Kipapa la Uinjilishaji wa watu na Rais wa Mashirika ya Kimissionari ya Kipapa, huku homilia ikitolewa na Askofu Msaidizi wa Jimbo Katoliki Bukoba Mhashamu Methodius Kilaini.
Katika maadhimisho haya, Balozi wa Papa nchini Askofu Mkuu Marek Solczyński amebariki Pango la Bikira Maria lililoko kwenye Kituo cha Hija cha Mbwanga, Jimbo Kuu Katoliki Dodoma huku Askofu Mkuu Protase Rugambwa akibariki Jiwe la msingi kwa ajili ya ujenzi wa Makao Makuu Mapya ya Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania yanayotarajiwa kujengwa Dodoma.


Comments

Popular posts from this blog

SALA YA ASUBUHI:SALI HIVI..

Ujio wa Wamisionari wa Kwanza Tanzania Bara (2)

MJUE MTAKATIFU MARIA GORETTI