Miaka 9 baada ya kifo cha Mgandu: watunzi wa sasa mna cha kujifunza!
TUNAPOENDELEA kusherehekea Jubilei ya miaka 150 ya Uinjilishaji Tanzania
Bara, tuna kila sababu ya kujivunia kwa uwepo wa Utume wa Uimbaji hapa nchini.
Uwepo wa
kwaya katika maadhimisho ya Misa Takatifu umesaidia sana kukoleza Liturujia na
kuwasaidia waamini kusali vizuri, ili Mungu atukuzwe na mwanadamu atakatifuzwe.
Ili malengo ya utume wa uimbaji yaweze kufikiwa ni lazima kuwe na mahusiano
mazuri na ya pande mbili kati ya watunzi wa muziki mtakatifu na waimbaji
(wanakwaya).
Hawa kwa
pamoja wanakamilisha mzunguko wa mawasiliano, ambapo mtunzi huwa kama mtumaji
wa taarifa (sender) huku waimbaji wakiwa wapokeaji na watekelezaji (receivers)
wa kile kilichoandaliwa na mtunzi. Hivyo basi, ili mawasiliano haya yaweze
kuleta tija kwa waamini ni lazima watunzi wawe msaada kwa wanakwaya, ili
wanakwaya wawasaidie waamini kusali vizuri.
Kwa miaka
ya hivi karibuni kumeibuka wimbi la watunzi ambao kwa namna fulani wanaenda nje
ya mstari. Utunzi wao haukaisi liturujia, haudhihirishi ule utajiri wa
mafundisho ya Kanisa. Ndiyo kusema kwamba, wengi hutunga nje ya maandiko
matakatifu, mafundisho ya kanisa na mapokeo kwa kile wakiitacho kwenda na
wakati.
Kwa hakika
huku ni kuibinfsisha liturujia. Kama wanakwaya wanageuza kanisa kuwa sehemu ya
burudani, huko ni kubinafsisha liturujia. Iwapo watunzi wanatunga nyimbo kwa
kutumia maneno ya mtaani, huko ni kubinafsisha liturujia. Utunzi wa nyimbo
ngumu zenye kona nyingi eti kwa kigezo cha kuonyesha ufundi, huko ni
kubinafsisha liturujia.
Hayo yote
hayamsaidii muumini kusali vizuri, tena zaidi haimfanyi Mungu atukuzwe na
binadamu atakatifuzwe. Ndiyo maana tuna kila sababu ya kujifunza kutoka kwa
watunzi walioturithisha tunu na hadhi bora za muziki mtakatifu. Wapo walio hai
na wengine wametangulia mbele ya haki, lakini mifano yao ingali inaishi.
Tuchote na tuutumie utajiri huo.
Mmoja kati
ya watunzi ambao walijitahidi kutumia karama zao katika kuwasaidia waamini
kusali vizuri kwa njia ya uimbaji ni Mwalimu John Stephano Mgandu.Yeye
alizaliwa Oktoba 8, 1940 kijijini Busondo, katika Parokia ya Ndala-Nzega,
mkoani Tabora.
Alipata
elimu katika Shule ya Msingi Puge (1951-1953), kisha Seminari ya Lububu (1954 –
1955), baadaye Seminari ya Itaga (1956 – 1959) na Seminari ya Kipalapala 1964.
Mwaka 1960 hadi 1970 alikuwa katika Chuo cha Ualimu cha Chang’ombe.
Elimu ya
muziki aliipata katika Chuo Kikuu cha Toronto nchini Canada ambako alisomea
Shahada ya Muziki (Bsc – Music) 1972 – 1976, na baadaye Chuo Kikuu cha Dar es
salaam akisomea Shahada ya Uzamili (MA – Music) 1987.
Amewahi
kufanya kazi katika maeneo mbalimbali pamoja na Benki ya NBC tawi la Masdo
(1968), Shule ya Sekondari ya Kibasila (1970), Shule ya Sekondari ya Mirambo
(1971), Shule ya Sekondari ya wavulana Tabora (1976 – 1978), Taasisi ya Elimu
(1978 – 1980) na kisha Chuo Kikuu cha Dar es salaam katika Idara ya Sanaa na
maonyesho (Julai 1980 – Julai 2008)
Alifunga
ndoa na Elizabeth Kulwa Binti Constatino Ngelegi, na kupata watoto wawili, wa
kiume na wa kike. Licha ya kuwa mtunzi, Mwalimu Mgandu alikuwa mpiga kinanda,
filimbi na ala nyingine nyingi. Pia alikuwa mwalimu na muongozaji wa muziki na
kwaya mbalimbali.
Ikumbukwe
kuwa mwaka 2002 Mwalimu Mgandu alishinda
tuzo ya kuwa Mpiga Kinanda Bora Tanzania (Tanzania Kilimanjaro Music Awards).
Alifariki Julai 10 mwaka 2008.
Kuna mengi
ya kujifunza kutoka kwa nguli huyu wa muziki mtakatifu, moja kati ya mengi ni
taaluma ya muziki mtakatifu. Mwalimu Mgandu alikuwa mwanamuziki aliye na
taaluma hata kuwa na Shahada ya uzamili (Masters) ya muziki. Cha ajabu watunzi
wengi siku hizi huridhika kujifunza muziki mtakatifu kwa kuunga unga. Hii
hupelekea kuzorota kwa taaluma hii, kwani kilichobaki kwa sasa ni watu
kurithishana na kufundishana kienyeji tu.
Hii
itukumbushe pia umuhimu wa kufufua madarasa ya muziki Mtakatifu katika
Seminari, nyumba za malezi, vyuo vikuu vya kanisa ili tupate wataalamu wa
kutosha.
Lakini
kubwa zaidi, pamoja na kuwa na elimu kubwa mwalimu Mgandu daima tungo zake
zilizingatia liturujia na alitumia maandiko matakatifu kama rejea ya nyimbo
zake. Sasa watunzi wa leo wanaotunga nyimbo kama ‘chenga ya mwili’, ‘gari la
shetani’ nk, wamejifunza wapi mambo hayo.
Ikiwa sisi
tulirithi muziki mtakatifu uliokolezwa liturujia nyoofu kutoka kwa watunzi kama
Padri Gregory Kayetta, Padri Malema, Padri Ntampambata, Nyundo, Syote, Makoye,
Mujwahuki, Mkomagu na wengine wengi, kwa nini nasi tusirithishe muziki huo kwa
vizazi vijavyo? Kwa nini tunataka kuwarithisha maneno ya mitaani?
Mchambuzi:
0657835343
Habari za Kazi Mr Pascal. Pascal asante sana kwa makala yako nzuri inayowatahadharisha wwatunzi wa nyimbo za iabada kuendana na maandiko. Nakupongeza sana! Ila nahisi kuna makosa kidogo katika historia ya Mwl John Mgandu. Umeandika kuwa alikuwa Seminari ya Kipalapala mwaka 1964 na mwaka 1960 hadi 1970 alikuwa chuo cha ualimu Changómbe. Ina maana mwaka 1964 alikuwa Kipalapala na wakati huo huo yupo Changómbe. Naomba ucheck vizuri hizo tarehe
ReplyDeleteMzee wetu mgandu apumzike kwa Amani. Hakika mchango wake wa uinjilishaji ni mkubwa sana ambao tuliobahatika kufundishwa kidogo naye tunajisikia wenye bahati na upendeleo mkubwa.
ReplyDeleteTunaendelea kumkumbuka na kumthamanisha sana.
Tunamwomba Mungu amsamehe makosa yake na kumstahilisha tuzo mbinguni. Apumzike kwa Amani AMINA
Mgandu akumbukwe daima
ReplyDelete