Miaka 100 ya Upadri yaleta neema Njombe
IMEFAHAMIKA kuwa Mwaka wa Jubilei ya Miaka 100 ya
Upadri Tanzania Bara imezaa matunda mema baada ya Parokia ya Mt. Yosefu Njombe
Mjini kufanikiwa kutoa Sakramenti ya kipaimara kwa vijana 750, tukio ambalo
limefanyika ndani ya siku tatu.
Askofu wa Jimbo Katoliki Njombe Mhashamu Alfred
Maluma katika mahubiri yake sambamba na kutoa Sakramenti hiyo, amewaasa watoto
kuzingatia mpango wa Mungu katika maisha yao hasa katika mwaliko wa Mungu
unaowaita wamtumikie yeye kwa namna mbalimbali za miito mitakatifu ya Upadri na
Utawa.
“Mungu alituumba kwa sura na mfano wake, na hivi
hakuna mtu aliyeumbwa kwa bahati mbaya. Kila mwanadamu ni chapa ya Mungu. Mungu
ana malengo na makusudi yake katika uumbaji wa kila mwanadamu. Mpango huo wa
Mungu unasikika katika kuitwa kwetu tumtumikie Mungu katika wito mtakatifu. Ili
tuweze kusikia vyema na kuifuata sauti ya Mungu vizuri, tunahitaji kuwa na
familia bora ambazo zitawalea vyema watoto na kuwafundisha maadili mema
yatakayowasaidia vijana kuitambua sauti ya Mungu. Katika maadhimisho ya Maika
100 ya Upadri Tanzania, tumwombe Mungu awaite vijana wema watakaomtumikia
katika wito wa upadri. Mavuno ni mengi lakini watenda kazi ni wachache.
Tumwombe Bwana wa mavuno apeleke watenda kazi katika shamba lake. Daima
zingatieni kazi ya Mungu na mwito wenu.”
Mara baada ya kupokea Sakramenti Takatifu ya
Kipaimara, watoto wameahidi mbele ya Askofu na Kanisa zima kuwa watadumu katika
imani yao Katoliki ya Mitume na pia wataitetea imani yao kwa nguvu zao zote
kwani mapaji ya Roho Mtakatifu waliyoyapokea ni kwa ajili ya kulilinda na
kulitetea Kanisa na imani yao.
Wazazi wa watoto hao waliopokea Sakramenti ya
kipaimara wamemshukuru Askofu Maluma kwa kazi nzuri na nzito aliyoifanya kwa
vijana wao huku wakimuahidi kuwalea watoto wao katika imani yao na kuwaongoza
vyema katika kuitikia sauti ya Mungu.
Comments
Post a Comment