‘WAMISIONARI SIYO WAFANYABIASHARA' ASKOFU DAMIAN DALLU
ASKOFU Mkuu wa Jimbo Kuu
Katoliki Songea Mhashamu Damian Dallu amesema kuwa wamisionari hawakuja nchini
kama wawekezaji bali ujio wao ulilenga kumkomboa mwanadamu kiroho na kimwili,
na ndiyo chanzo cha utoaji wa huduma za msingi za kijamii ikiwemo elimu, afya
na maji.
Ameeleza hayo hivi
karibuni katika Adhimisho la Misa Takatifu ya kutoa Daraja Takatifu ya Upadri
kwa aliyekuwa Shemasi Jerome Mponzi, katika Parokia ya Nyakipambo Jimbo
Katoliki Iringa.
Askofu Dallu amesema
kuwa wamisionari hawakujikita katika utoaji wa huduma za kiroho pekee, bali
walihakikisha mwanadamu anakombolewa mzima mwili na roho, ndiyo maana
walipojenga Kanisa walijenga pia vituo vya afya, hospitali au zahanati, shule
na miradi ya maji.
“Sisi ndiyo
tulioanzisha utoaji wa huduma za jamii kwa wananchi wote bila kubagua. Baada ya
Serikali kuamka ndipo Mwalimu Nyerere akataifisha shule na miundombinu ya afya
ili kuimarisha umoja wa kitaifa. Wazee wetu watangulizi walilielewa hili na
hawakupiga kelele kwani waliona ni jambo jema linalowanufaisha watu wote. Baada
ya muda huduma hizi zilizorota ndipo katika awamu ya pili baadhi yake
zikarudishwa mikononi mwa Kanisa, na kisha Serikali kuingia mkataba ili
wamisionari waendelee kutoa huduma kwa ufanisi zaidi, kwa manufaa ya wengi,
huku Serikali ikisaidia,” amesema.
Aidha Askofu Dallu
ameongeza kuwa inashangaza kuona mtawa aliyekuja nchini mwaka 1950, akajitoa
kuhudumia jamii bila faida, anafuatwa na kudaiwa kibali cha kufanya kazi nchini
na kumtaka alipe kodi, na kusisitiza kuwa huku ni kumfanya mmisionari kuwa kama
mfanyabiashara, jambo ambalo siyo sahihi.
“Sisi siyo dini ya
mtu wala hatuna mwelekeo au msukumo wa kisiasa. Hatuhitaji upendeleo wa mtu
bali tunafuata utaratibu uliowekwa. Tumesajiliwa chini ya Wizara inayohusika na
Katiba na Sheria, hatujasajiliwa chini ya Wizara inayohusika na mambo ya
ajira,” ameongeza.
Akikumbushia juu ya
Waraka wa Baba Mtakatifu Leo XIII uitwao ‘Rerum Novarum’, Askofu Dallu ameeleza
kuwa kuna haja ya kujikita katika mfumo wa elimu unaolenga kujenga dhamiri za
wasomi, ili kuliepusha Taifa dhidi ya watumishi wasio waadilifu.
Marufuku
kubinafsisha karama
Pia Askofu Dallu
ametoa angalizo kwa Vyama vya Kitume na waamini nchini kutobinafsisha karama,
na badala yake kumtambulisha Kristo kupitia yale yote wanayoyafanya. Ameonya
tabia ya watu kutaka kuonekana wao katika mambo wanayoyafanya na kumuweka
pembeni Kristo, jambo linalochochea dharau dhidi ya viongozi wa kiroho.
“Kupitia karama zenu
hakikisheni mtu anamuona Kristo na siyo ninyi. Chochote mnachokifanya ni lazima
aonekane Kristo kwanza. Msitumie karama kufanya biashara. Na isitokee watu
wanasali kwa ajili ya kuponywa tu, matokeo yake tutakuwa na makanisa ya
wagonjwa, kwani wote watakaohudhuria watakuwa wagonjwa isipokuwa yule
anayeombea. Huu ni mwanzo wa wakristo kuwa watumwa wa mwombeaji, na ni kinyume
na maagizo ya Kristo ambaye alipowaponya watu aliwaambia waende zao,” ameeleza.
Baba askofu, umenena vyema mimi nimetoka kwenye familia maskini sana na kanaisa ndiyo iliyonisomesha mpaka sasa nafanyakazi serikali na aliyekuwa akinilipia ada ni msionary "kweli wamisionary sio wafanyabiashara"
ReplyDelete