Kanisa Katoliki lawa msaada mkubwa kwa wakazi Mtwara
IMEELEZWA kuwa uwepo kwa Kanisa Katoliki katika
Jimbo Katoliki Mtwara umekuwa msaada mkubwa wa maelfu ya waamini kutokana na
wengi wao kumjua Kristo na kupata huduma za Kiroho ndani ya maisha yao.
Kauli hiyo imetolewa kwa nyakati tofauti na baadhi ya mapadri wa Jimbo hilo wakati
wakizungumza na gazeti la Kiongozi lilipotaka kujua Historia mbalimbali juu ya
Imani Katoliki kwa waamini.
Padri Nixon Mbila ambaye ni Paroko wa Parokia ya
Watakatifu Wote Jimbo Katoliki Mtwara pamoja na Padri Silvanus Chikuyu Paroko
wa Parokia ya Watakatifu Petrol na Paulo Mitume
wamesema kuwa Parokia ya Watakatifu Wote
ilianzishwa mwaka 1957 na Parokia ya Watakatifu Petrol na Paulo Mitume
ilianzishwa mwaka 2006 ambapo kumekuwepo na mafanikio makubwa kwani waamini
wengi na wengine kutoka madhehebu tofauti wamekuwa wakifika parokiani hapo
kupata huduma za kiroho na kimwili tofauti na hapo awali.
Wamesema kuwa wapo waamini ambao hapo awali walikuwa
wakipata matatizo na wengine walipofariki hawakupata huduma za Sakramenti
lakini kwa sasa wanajivunia kwa jinsi mapadri ambavyo wamekuwa nao bega kwa
bega kuwapa msaada.
Wamesema kuna idadi kubwa ya waamini wanaotoka Dini
zingine kuja kupata huduma za kikanisa, kuongezeka kwa uandikishwaji wa
Sakramenti ya Ndoa, kuwepo kwa Sakramenti ya Kipaimara, kuanzishwa shule za
Chekechea pamoja na kupanua makanisa.
Vile vile Kanisa Katoliki limefanya kazi kubwa ya
kutatua migogoro mbalimbali ya kifamilia katika jamii, hivyo kila parokia kuwa
na Kamati imara ambayo inashughulikia mambo hayo.
Aidha kwa ushirikiano wa waamini wamekuwa wakifanya
kazi za kijamii hususani kutoa misaada ya chakula, mavazi na fedha kwa watoto
yatima, wajane, wafungwa, na wote wasiojiweza huku wakitoa huduma ya kuwaombea
wagonjwa hospitalini jambo ambalo limekuwa msaada mkubwa kwa jamii.
Mbali na mafanikio hayo kumekuwa kukijitokeza
changamoto mbalimbali za kutaka kurudisha nyuma imani Katoliki kwa madai kwamba
baadhi ya vijana wakatoliki husahau imani zao.
Hata hivyo mbali na changamoto hizo kumekuwepo
mipango mizuri ya kuhakikisha waamini hawapotei kwani wamekuwa wakiimarisha
Jumuiya ndogondogo, kuimarisha utume wa
vijana wadogo kwa kuwapa Semina mbalimbali na makongamano ambayo
yanawafundisha kukaa katika imani zao na kwa kiwango kikubwa vijana na waamini
wamekuwa na uelewa juu ya imani yao.
Padri Silvanus Chikuyu Paroko parokia ya Watakatifu
Petrol na Paulo amesema kuwa parokia yake wana miradi ya shamba la ndizi,
minazi na machungwa huku wakiwa na malengo makubwa ya kuanzisha miradi ya
vibanda vya biashara.
Hata hivyo amewataka waamini kuwa karibu mbele za
Mungu kwa kumtolea sadaka inayompendeza kutokana na parokia hiyo kutokuwa na
msaada kutoka nje huku akiwasihi baadhi ya wakristo kuacha kasumba ya kuvaa
Rozali kama pambo bila kusali kwani kumekuwepo na vijana wengi ambao hawajui
kuitumia.
Naye Paroko Nixon Mbilla wa parokia ya Watakatifu
Wote amesema kuwa parokia ina miradi mbalimbali ikiwemo ya kukarabati nyumba ya
mapadri ambayo wanaendelea nayo kutokana na kuchakaa kwani tangu mwaka 1957
haijawahi kufanyiwa ukarabati na kwamba mpaka sasa kumalizika kunahitajika
kiasi cha shilingi milioni thelathini na sita, mpaka sasa wametumia milioni kumi na moja.
Pia amesema wana mradi wa kujenga uzio na mageti ya
kisasa, kuanzisha kiwanda cha kuzalisha maji, kuanzisha duka la vitabu, ukumbi
wa mikutano pamoja na shamba la mahindi na mihogo.
Hata hivyo ametoa wito kwa wakristo kuwanyenyekea na
kujishusha mbele ya viongozi wao hata kama wakichukizwa bali wanapaswa kuwa na
busara ya kukaa pamoja kumaliza tofauti zao.
“Wapo wakristo hawataki kujishusha mbele ya mapadri,
na viongozi wao wanakuwa na kiburi ambacho matokeo yake sio mazuri, hivyo
nawasihi onyesheni upendo na mshikamano kwa viongozi wenu,” amesema padri
Nixon.
Comments
Post a Comment