KANISA KATOLIKI LAIKABIDHI SERIKALI JENGO LA OFISI YA KATA MOROGORO
MAKAMU Askofu
wa Jimbo Katoliki Morogoro Padri Patrick Kung’alo amesema kuwa Kanisa Katoliki
limejiwekea malengo ya kuendelea kutoa huduma bora za kijamii hasa afya na
elimu ili kuwahudumia waamini na wananchi wengi zaidi kimwili na kiroho.
Padri Kung’alo amesema hayo hivi karibuni katika
hafla maalumu ya kumkabidhi Mkurugenzi wa wilaya ya Mvomero Frolent Laurenti
jengo la ofisi ya Kata ya Kinda ambalo limejengwa na Kanisa Katoliki ili
kutumika kama ofisi ya Kata hiyo.
Padri Kung’alo ameeleza kuwa malengo ya Kanisa
Katoliki kusimamia huduma za kijamii ni kuisaidia Serikali kwa lengo la
kuhakikisha kuwa mwanadamu anapata huduma msingi za kibinadamu ili kumtumikia
Mwenyezi Mungu daima.
Aidha padri
Kung’alo amesema zipo shule nyingi, hospitali, vituo vya afya na zahanati
mbalimbali katika ushiriki wa utoaji huduma za jamii, ambapo Serikali pia mara
kwa mara imekiri wazi namna Kanisa linavyochangia utoaji wa huduma msingi za
kijamii.
“Kanisa Katoliki linajulikana sana katika utoaji huduma
za jamii kupitia elimu na afya, na litaendelea kufanya hivyo mpaka mwisho wa
nyakati, tunazo shule zinazoendeshwa na Kanisa Katoliki kuhudumia jamii ikiwa
ni kuisaidia Serikali yetu,” amesema padri Kung’alo.
Hata hivyo kiongozi huyo wa kiroho amesema kuwa
Kanisa Katoliki litaendelea kuwa bega kwa bega na Serikali ya Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania huku akiwaomba watumishi watakaotumia ofisi hiyo kutumia
karama zao kuboresha huduma kwa wananchi.
Wakati huo huo padri Kung’alo amewaasa watanzania
kumtanguliza Mwenyezi Mungu, kama ambavyo Rais John Magufuli anavyoendelea
kusisitiza katika hotuba zake mbalimbali ili jengo hilo litumike kufanya
mikutano mbalimbali kwa lengo la kuwagusa wanadamu kwa mujibu wa mapenzi ya
Mwenyezi Mungu.
“Tuiombee ofisi hii na wale watakaoitumia kuguswa na
mahitaji ya wanadamu, kila mtumishi ahakikishe anafanya kazi kwa kuzingatia
mahitaji ya jamii, na nina hakika haya ni mapenzi ya Mwenyezi Mungu kwa sababu
wote tupo kwa ajili ya kusaidiana na kuhurumiana,” amesema padri Kung’alo.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa wilaya ya Mvomero
Frolent Laurent amelishukuru Kanisa Katoliki kuendelea kushirikiana na Serikali
huku akiwaomba watumishi wa Kata hiyo kufanya kazi kwa ushirikiano na
mshikamano kugusa mahitaji ya wananchi.
Comments
Post a Comment