Wananchi wachangamkie Ushirika
IMEELEZWA
kuwa jitihada za sasa za Serikali kuboresha miundombinu ya usafirishaji na kupeleka nishati ya umeme vijijini
zitapunguza changamoto na kuongeza fursa za ujenzi wa viwanda kupitia ushirika.
Hayo yameelezwa na Makamu Mkuu wa
Chuo Kikuu cha Ushirika Profesa Faustine Karrani Bee katika ufunguzi wa warsha
ya Chuo Kikuu cha Ushirika Moshi na wanahabari kuhusu elimu ya Ushirika nchini
na mchango wa Chuo katika kuendeleza ushirika.
Amesema kuwa Ushirika ndio njia pekee
ya usawa ya kujenga uchumi utakaomilikiwa na watanzania ambapo uchumi
utamuondoa Mtanzania katika umaskini na kumuwezesha kumiliki rasilimali za
nchi.
Bee amesisitiza kuwa tafiti,elimu na
ushauri vinavyotolewa na chuo cha Ushirika Moshi vinahitaji na vimekuwa
vikipata ushirikiano wa karibu kutoka kwa wanahabari ili kufikia malengo yanayo
tarajiwa ya jamii kuwa na uelewa na kuzidi kuviamini vyama vya ushirika nchini.
Chuo kikuu cha Ushirika kinatarajia
mtazamo chanya kwa watanzania katika kufikia malengo ya ushirika hapa nchini,
kwa kushirikisha wadau mbalimbali katika kutoa elimu ya Ushirika na kuhakikisha
kuwa jamii inapata habari sahihi za Ushirika.
Ameongeza kuwa kwa sasa vyama vingi
vya ushirika vimekuwa na changamoto mbalimbali zilizosababisha uaminifu wa
vyama vya ushirika kutoweka katika jamii, hivyo kumtaka Mrajisi wa vyama vya
Ushirika kufanya jitihada za kurudisha imani hiyo kwa wananchi kwa kutoa
maelekezo kwa vyama vya msingi vya ushirika nchini.
Kwa upande wa wanahabari katika
warsha hiyo wametaka Chuo Kikuu cha Ushirika ambacho ndio watendaji wakuu wa Elimu ya Ushirika nchini kuondoa
dhana ya kupenda kuongelewa kwa mazuri kwani wengi hawapendi kukosolewa na ndio
chanzo cha kuwa mbali na wanahabari.
Aidha wamebainisha kuwa vyombo vya
habari vimekuwa vikishutumiwa kwamba vinaleta uchochezi pale vinapotafuta na
kutoa taarifa kuhusu ubadhilifu na madhaifu mengine ya ushirika jambo ambalo ni
kinyume, hivyo kutaka Chuo hicho kutoa
elimu kwa jamii na watendaji wa bodi za vyama vya ushirika kukubali kazi za
wanahabari.
Warsha hiyo imelenga kuanzisha na
kuendeleza ushirikiano wa pamoja kati ya chuo kikuu cha Ushirika Moshi- MOCU na
wanahabari katika kutekeleza mpango wa kuendeleza Elimu ya Ushirika hapa nchini
pamoja na kutoa fursa kwa wanahabari kufahamu shughuli mbalimbali zinazofanywa
na chuo katika kutoa elimu ya ushirika.
Comments
Post a Comment