WANANCHI WATAHADHARISHWA KUTOVAMIA MAENEO YA KANISA
WAnanchi wanaoishi jirani na maeneo yanayomilikiwa na
Kanisa Katoliki kwa ajili ya kutoa huduma mbalimbali zikiwemo za kiroho, na
kijamii wametakiwa kutoingilia mipaka ya maeneo hayo kwa kuwa maeneo hayo
yalitolewa kwa mujibu wa kanuni, sheria na taratibu.
Baadhi ya maeneo ya Kanisa
yamekuwa yakiingia katika migogoro mikubwa na wananchi wanaoishi kuzunguka
maeneo hayo, kutokana na watu kuvamia na kujenga pasipo kujua au wakijua kuwa
eneo hilo tayari lilishanunuliwa na Kanisa kwa ajili ya kutoa huduma katika
jamii na hatimiliki zikiwepo zinazoonyesha ukubwa wa eneo, lakini viongozi wa
vijiji husika wamekuwa wakigeuka na kusema kuwa Kanisa ndio linalochukua maeneo
ya wananchi.
Hayo yamesemwa hivi karibuni na
Askofu wa Jimbo Katoliki Musoma Mhashamu Michael Msonganzila wakati wa Misa
Takatifu ya Kumshukuru Mungu kwa shirika la Marist Brother kutimiza miaka 200
tangu lilipoanzishwa mwaka 1817, miaka 25 ya uwepo wa shirika hilo hapa nchini
Tanzania katika kijiji cha Masonga na miaka 25 ya shule ya Sekondari ya Masonga
pamoja na parokia ya Masonga tangu zianzishwe, Misa iliyofanyika katika shule
ya Masonga jimboni hapa.
Askofu Msonganzila amesema
kuwa mashirika ya kitume yanapokuja
nchini hayaji kunyang’anya wananchi maeneo yao, bali lengo lao linakuwa
kuwahudumia wananchi ambao ndio kusudio lao kubwa, hivyo kwa vile
Kanisa linakuwa na maeneo makubwa ambayo wanakuwa wameshayanunua mapema
ndio maana wanawaruhusu kujenga kwa
ajili ya kutoa huduma kwa jamii na hasa katika maeneo yaliyoachwa nyuma
kimaendeleo na ndio maana shirika la Marist Brother walipofika Masonga walianza
kutoa huduma ya kiroho na elimu dunia kwa maana kuwa ndio walioanzisha shule ya
Sekondari ya Masonga na eneo hilo lilikuwa nyuma kielimu.
“Hivi karibuni nilikuwa huku kwa
masuala ya migogoro ya ardhi, wananchi wanasema kijiji kililiuzia Kanisa eneo
hili kinyemela wakati kwenye hati ya eneo hili inaonyesha mwanzo wa eneo hadi
mwisho, na niwaambie kabisa huduma wanazozitoa hawa mabruda zitakuwa nzuri kama
mahusiano yenu baina ya wananchi na viongozi wa vijiji vinavyozunguka shule hii
yatakuwa mazuri.
“Ombi langu kwa viongozi wa vijiji na Wilaya hii ya Rorya naombeni sana
tuache mizozo ya viwanja, ambayo inasababisha huduma zisiendelee au
zicheleweshwe na sisi hapa Masonga tupo pembezoni kabisa, na Marist hawa
wametoka mbali kuja kutusaidia kimaendeleo, naomba tuwape nafasi jaza ujazwe, tuwajaze maeneo ili tufaidike
zaidi, viongozi wa Serikali toeni mwanya
ili huduma za jamii zinazoletwa na hawa watu wa mbali ziweze kutuletea
maendeleo,” amesema Askofu Msonganzila.
Reman Osca mwakilishi wa shirika hilo kutoka nchini Mexico amesema kuwa
wao walikuja kusaidia jamii ya Masonga ambayo ipo pembezoni kabisa na ilikuwa
imeachwa nyuma kimaendeleo hususani kielimu, na kwa sasa jamii iko vizuri
kielimu na kiroho.
Kwa upande wake mkuu wa shule hiyo ya Masonga Br Valerian Stephen
Kalendelo ambaye ndiye mwafrika wa kwanza tangu kuanzishwa kwa shirika hilo
hapa nchini Tanzania, amesema kuwa shule hiyo kwa sasa ina wanafunzi 470 na
mwaka huu wanaotarajia kufanya mtihani wa kidato cha nne wapo 67 na kuna shule maalum ambayo ina watoto 21
viziwi, ambapo hadi sasa wanahitaji kujenga majengo mengine kwa ajili ya
kupanua huduma wanazozitoa lakini wananchi wamezuia kwa madai kuwa eneo
wanalotaka kujenga ni la wananchi, kwa madai kuwa Serikali ya kijiji ililiuzia
Kanisa eneo hilo kinyume na taratibu.
Comments
Post a Comment