WAOMBEENI WATUMISHI WA MUNGU-ASKOFU MSONGANZILA
WAKAtoliki jimboni Musoma wameaswa
kuhakikisha wanawaombea mashemasi,
mapadri na watawa, ili waweze
kudumu na kuziishi nadhiri zao,
kama walivyotoa ahadi kwa Mwenyezi Mungu na mbele ya Kanisa Katoliki.
Hayo yamesemwa na
Askofu wa Jimbo Katoliki Musoma Mhashamu Michael Msonganzila wakati wa ibada
Takatifu ya kutoa daraja ya Ushemasi kwa Flateri Thomas Nsabamusabe Samwel na
Flateri Gabriel Boli Wadan, iliyofanyika hivi karibuni katika Parokia ya
Mtakatifu Yohane Mbatizaji Nyamiongo jimboni hapa.
Askofu Msonganzila
amesema kuwa ni wajibu wa waamini
wakatoliki kuhakikisha wanaweka muda wa kuwaombea wahudumu wa Kanisa ambao
wanajitoa kwa Mungu kwa ajili ya kulitumikia Kanisa na jamii kwa ujumla, ili
waweze kuziishi na kudumu katika nadhiri
zao, kwa kuwa bila maombi hawawezi
kufanya chochote.
“Niwaombe wakristo
wa jimboni Musoma, tusisahau kuwaweka katika maombi mashemasi wetu, mapadri,
watawa na wanovisi, ili wazidi kuimarika kiroho na kimwili katika kumtumikia
Mungu, kwani hii ni zawadi ya wito kwa vijana wetu na pia tunamshukuru Mungu
kwa kutupatia nafasi hii ya walelewa na vijana kuonja miito hii ndani ya Kanisa
letu,” amesema Askofu Msonganzila.
Paroko wa Parokia ya
Mtakatifu Yohane Mbatizaji Nyamiongo Padri Bosco Kiyuga amesema kuwa wanamshukuru Mungu ndani ya shirika lao la
Wana wa Moyo Safi wa Bikira Maria (WAKLARETI) kwa karama ya Utumishi wa neno la
Mungu katika kueneza neno hilo kwa njia mbalimbali ikiwemo uchapishaji wa
vitabu na majarida.
Padri Kiyuga amesema
kuwa kwa sasa shirika hilo limeadhimisha
miaka 25 ya uwepo wake katika nchi tatu za AfrikaMashariki yaani Kenya,Uganda
na Tanzania ambapo kwa Tanzania shirika hilo lina jumuiya jimboni Musoma,
Mwanza, Dar es Salaam, Morogoro na Moshi, na tangu lianzishwe linaadhimisha
miaka 168, hivyo wanamshukuru Mungu kwa Neema na Baraka nyingi alizowajalia,
baada ya kuanzishwa na Mtakatifu Antoni Maria Claret na mapadri wengine watano
huko Vic nchini Hispania mwaka 1849.
Kwa upande wake
shemasi Gabriel Wadan amesema kuwa safari yake ya wito shirikani ilianza mwaka 2007 alipoanza malezi ya kwanza huko
Kupang Indonesia na aliweka nadhiri zake za kwanza Julai 16, 2011 ambapo
amepokea daraja ya Ushemasi Julai 27, 2017 kutoka kwa Askofu Michael
Msonganzila wa Jimbo Katoliki Musoma katika Parokia ya Mtakatifu Yohane
Mbatizaji Nyamiongo, ambapo anamshukuru Mungu kwa zawadi hiyo huku akiahidi
kuitumikia hadi kufa kwake.
Naye Shemasi Thomas
Nsabamusabe amesema kuwa safari yake ya wito shirikani ilianza Septemba 2007 alipojiunga na malezi ya kwanza Makoko Centre jimboni Musoma na aliweka
nadhiri zake za daima Julai 26 mwaka 2017, na amepokea daraja ya Ushemasi Julai
27, 2017 katika parokia ya Mtakatifu Yohane Mbatizaji Nyamiongo kutoka kwa
Mhashamu Michael Msonganzila wa Jimbo
Katoliki Musoma ambapo amewaomba waamini wa Jimbo hilo kuendelea kuwaombea kwa
Mungu ili waendelee kuziishi na kudumu katika wito wao kama walivyoahidi mbele
ya Mungu na mbele ya Kanisa Katoliki.
Comments
Post a Comment