BARAZA LA MAASKOFU KATOLIKI KUHAMIA DODOMA
BARAZA la
Maaskofu Katoliki Tanzania (TEC) limethibitisha kuwa lina mpango wa kuhamisha
makao yake makuu kutoka Kurasini jijini Dar es salaam kwenda Dodoma. Hayo
yameelezwa na Makamu wa Rais wa TEC ambaye pia ni Askofu Mkuu wa Jimbo Kuu
Katoliki Dodoma Mhashamu Beatus Kinyaiya, wakati wa Misa Takatifu ya kilele cha
jubilei ya miaka 100 ya upadri Tanzania, iliyofanyika katika kituo cha hija cha
Mbwanga, Dodoma.
Akitoa
salamu za TEC katika maadhimisho hayo yaliyohudhuriwa na mamia ya waamini,
Askofu Kinyaiya amesema kuwa baraza lina mpango wa kuhamisha makao yake makuu
yaende Dodoma na mchakato huo utaanza baada ya kufanya mazungumzo na serikali
ya kupata ardhi itakayotumiwa na shughuli za TEC.
“Tuna
mpango wa kuhamisha makao yetu makuu yaje Dodoma. Bado tunaongea na serikali
ili tupate kipande cha ardhi, ambapo leo pia tumebariki jiwe la msingi la
kikanisa kitakachojengwa mahali hapo” ameeleza Askofu Kinyaiya.
Kwa upande
wake mwakilishi wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika sherehe hizo,
ambaye ni Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais anayeshughulikia Tawala za Mikoa na
Serikali za Mitaa, George Simbachawene, ametoa agizo kwa serikali ya Mkoa wa
Dodoma ihakikishe inafanya mazungumzo na TEC ili ndani ya siku 10 kiwanja kiwe
kimepatikana kwa ajili ya kuanza ujenzi wa Makao Makuu ya TEC.
“Maamuzi
ya kubariki jiwe la msingi la kikanisa cha TEC kama ishara ya kuhamia Dodoma ni
ujumbe mzito sana kwa serikali ya awamu ya tano na serikali ya Dodoma.
Ninaagiza ndani ya siku kumi zoezi la upatikanaji wa kiwanja sehemu
wanapohitaji liwe limekamilika. Sisi tutawapa kila aina ya msaada kwa haraka,
nasi wana Dodoma tutoe ushirikiano” ameeleza.
Awali
akitoa salamu za Mkoa wa Dodoma, Mkuu wa Mkoa huo Jordan Rugimbana amesema kuwa
TEC imebariki wazo la Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John
Magufuli la kuhamishia Makao Makuu ya nchi mkoani Dodoma.
Aidha
Rugimbana amesema kuwa serikali ya mkoa huo itatoa mifuko 100 ya saruji kwa
ajili ya ujenzi wa makao makuu hayo mapya ya TEC.
Comments
Post a Comment