" KIU YA AMANI" YAWAKUTANISHA VIONGOZI WA DINI MBALIMBALI DUNIANI KUOMBEA AMANI
Viongozi wa dini na tamaduni mbalimbali, wanaoamini Mungu na wasio amini kutoka pande za dunia, jana, wameunganika pamoja kutolea maombi yao, wakianza na kila mmoja kulingana na kanuni yake, na kisha kwa pamoja, wakiwa na nia moja tu ya kusali kwa ajili ya amani duniani wakiongozwa na Kaulimbiu" Kiu ya amani. Uwepo wa siku hii ya kuomba amani duniani, ilianzishwa mwaka 1986, na Mtakatifu Yohana Paulo II.
Baba Mtakatifu Francisko akifuata nyayo za mtangulizi wake Yohana Paulo II, mapema Jumanne , alikwenda Assisi , kushiriki katika tukio hili muhimu baina ya dini, kuifunga Siku ya Kimataifa ya Maombi kwa ajili ya Amani, kama ilivyoandaliwa Jumuiya ya Mtakatifu Egidio.
Jumapili iliyopita, Baba Mtakatifu Francisko, wakati wa sala ya Malaika wa Bwana, akiutaja mkutano huu wa viongozi wa kidini kukutana Assis, alisema kwamba , katika nyakati hizi kuliko hata siku za nyuma , tunahitaji kuomba amani kwa dunia hii iliyojaa matendo maovu kila mahali. Papa alitoa wito kwa Parokia zote, vyama vyote vya kikanisa, na watu wote kwa ujumla na binafsi duniani kote kushiriki kwa pamoja katika maombi haya, ambayo katika ngazi ya kidunia imefanyika katika mji mdogo wa Assisi, Italia, mji alikozaliwa Mtakatifu Francis wa Assisi, mtu mashuhuri anayejulikana kuwa na sifa za ukarimu na fadhila kwa viumbe wote
Hivyo siku hii ya maombi ya amani kufanyika Assisi, ni wito unaotolewa kwa watu wote kuiga maisha ya Mtakatifu Francis , kuwa mashahidi thabiti wa matendo mema na huruma ulimwenguni kote, na hasa kwa viongozi wa kidini na tamaduni zote, kuonyesha dhamiri yao katika ujenzi wa amani na maridhiano miongoni mwa watu. Siku hizi zinazoandaliwa kwa ajili ya kuomba amani duniani, pia hutumika kama uwanja wa kujadili masuala mbalimbali muhimu katika ngazi ya kimataifa yanayogusa amani, umoja na ushirikiano pamoja na faida za mazungumzano kati ya dini na tamaduni.
Baba Mtakatifu Francisko mapema Jumanne, aliwasili Assisi kwa njia ya helkopta, na ilitua karibu na Kanisa Kuu la Mtakatifu Maria wa Malaika, ambako alipokewa na Askofu Domenico Sorretino wa Assis , wakiwepo pia viongozi wa kiraia wa eneo hilo, na kisha kusafiri kwa gari hadi katika nyumba ya Takatifu ya Asissi , ambako alipokewa na Padre Mauro Gambetti, Msimamizi wa nyumba hiyo, akiwepo pia Patriaki wa Constatinople, Barthoromew I , Wawakilishi wa dini ya Kiislamu , Askofu Mkuu wa Canterbury , Patriaki wa Kanisa la Kiotodosi la Siro ya Antokio, mwakilishi wa Wayahudi , pia akiwepo Mkuu wa dini ya Kibudha Ujapani. Na kisha kwa pamoja waliongozana hadi Makazi ya Watawa ya Sixtus 1V, ambako kulikuwa na kundi jingine la wawakilishi wa madhehebu ya Kikristo na dini zingine duniani .
Kwao wote Baba Mtaktifu aliwasalimia na kuwashukuru kwa kufika kwao katika Mkutano huu muhimu kwa ajili ya sala ya kuomba amani duniani, na nyakati za adhuhuri walipata chakula pamoja katika Nyumba Takatifu ya Watawa.
Majira ya saa kumi saa za Italia, ulikuwa ni wakati wa sala kwa ajili ya kuomba amani , sala zilizofanyika sehemu mbalimbali , Wakristo walikusanyika pamoja na kuwa na sala ya kiekumeni katika Kanisa Kuu la Mtakatifu Francisi na kisha wote walitoka na kwenda kukutana na wawakilishi wa dini zingine ambao nao tayari walikuwa wamefanya sala zao kila mmoja kulingana na kanuni yake , na wote kukusanyika katika jukwaa lililoandaliwa uwanjani.
Mkutano huo, ulifungwa na Papa Francisko majira ya saa kumi na moja za jioni .
Comments
Post a Comment