MAENDELEO HAYALETWI NA SIASA ZA UADUI- ASKOFU NKWANDE
Viongozi wa siasa nchini wameaswa
kuchukulia changamoto walizonazo kuwaunganisha
kwa maslahi ya taifa badala ya kujenga uadui.
Mhashamu
Askofu wa Jimbo katoliki Bunda Renatus Nkwande
amezungumza na gazeti hii juu ya mustakabali wa taifa baada ya mvutano wa
UKUTA na wabunge wa vyama pinzani kukubali kuingia bungeni kwa heshima ya
viongozi wa dini na Spika wa Bunge Job Ndungai
Askofu
Nkwande amesema mustakabali wa taifa hili utakuwa hasi kama serikali itawaona
wapinzani kitu cha bure. Kadhalika kama wapinzani watakuwa wanakosoa kila kitu
serikali inachofanya tena kwa ushabiki wa maandamano. Amesema hayo ni mawazo dhaifu
na haoni kama demokrasia inayotafutwa pamoja na maendeleo ya nchi hii
yatapatikana kwa namna hiyo.
“Watawala
wasifikiri kwa kuwadhoofisha wapinzani ndipo taifa litapata maendeleo na amani.
Utawala mzuri unachukua changamoto kama sehemu ya kuimarika na kuwaacha
wapinzani wafanye yao kwani kuitwa wapinzani lazima wakosoe utawala aidha kwa propaganda
zao ama kwa maendeleo ya taifa.
Vilevile
wapinzani wasifanye hoja zao kuwa sheria ambayo haipingwi na wasikosoe kila
kitu. Wawe wavumilivu, wenye subira kwa ajili ya maendeleo ya taifa. Upinzani
si kukataa kila kitu tu,” ameeleza Askofu Nkwande.
Amesema
nchi ni ya kila mwananchi, na ni wajibu wa kila mwananchi kulinda amani na
utulivu uliopo kwa manufaa ya sasa na ya baadaye.
Aidha
baadhi ya viongozi wa dini wameeleza kuwa, ijapokuwa wabunge wapinzani
wamekubali kuahirisha UKUTA na kuingia bungeni kwasababu ya kuwasubiri
wakazungumze na rais inaonyesha kuwa wamekubali ushauri kwa masharti.
Iko hoja
moja kuwa, endapo viongozi hao hawatafanikiwa kuonana na rais watarudia
misimamo yao ya awali.
Kumbe kuwashawishi CHADEMA na serikali kufanya maridhiano ni
kutimiza wajibu wao wa kuhakikisha amani ya nchi inadumu na kuondokana na dhana
ya viongozi wa dini kutafuta usuluhishi badala ya kuacha nchi iingie katika
machafuko.
“Baadhi ya watu wanachukulia suala la maandamano kama kitu
kidogo lakini ingefaa wakajifunza kutoka katika mataifa mengine. Heri kuzuia
moto kuliko kupambana na moto.
Sisi maaskofu, wachungaji na masheikh ni washauri tu hivyo pale tunaposhauri na
kukubaliwa ushauri wetu kwa masharti pia kuna ulakini.
Kuambiwa tunakubaliana kuahirisha maandamano kwa muda fulani ili
mkazungumze na rais ni kama kushurutishwa kufanya interesti za vyama. Sisi ni
viongozi wa dini tulio na dhamana ya kulinda maadili na imani za watu si siasa.
Hivyo ningependa serikali pamoja na vyama vya siasa kutusikiliza kama washauri
badala ya kutupa masharti,” ameeleza kiongozi mmoja wa dini ambaye hakupenda
kutajwa jina lake.
Amesisitiza kuwa, viongozi wa dini pia wanapaswa kufahamu wajibu
wao lakini si kuwa na interesti na chama flani ama upande mmoja wa mvutano.
Wakiwa ni wanachama wa baadhi ya vyama hatutaweza kushauri vizuri na serikali
haitapata ushauri unaofaa.
Ameiasa serikali kuwa
imara, kutoshindana na vitu vidogovidogo ambavyo vinapoteza muda badala ya
kufanya kazi za maendeleo.
“Upinzani uachwe ufanye yake na serikali ifanye yake. Serikali
ni kama inaweka makucha na kutumia nguvu nyingi kupambana na vitisho ambavyo
kimsingi vilikuwepo tangu enzi za mwanzo wa mfumo wa vyama vingi.
Wapo viongozi wa siasa waliokuwa wakivuma sana kipindi kile
lakini hata Nyerere mwenyewe aliwaacha wafanye yao na yeye akizidi kujiweka
imara.” Ameeleza kiongozi huyo.
Amewaasa wapinzani kufanya kazi yao ya kuikosoa serikali kwa
subira na uvumilivu bila kuhatarisha amani ya taifa.
Kuandaa polisi na jeshi kupambana na vitisho vya wapinzani
ni kuleta woga wa kivita kwa wananchi.
Kadhalika kuandaa maandamano kwa kutumia nguvu na kauli za vitisho kunaleta pia
woga wa kivita wa wananchi. Hivyo ninawasihi wanasiasa kufanya kazi zao kwa
subira na uvumilivu.
Kubwa zaidi ni serikali kuangalia inapambana na nani. Kuna mambo
ambayo wapinzani lazima wayafanye hivyo isiogope. Pengine wapinzani wameshajua
kuwa serikali inaogopa changamoto ndio maana wanatishia ili kuifanya serikali
dhaifu. Pia pengine serikali ina washauri wabovu ambao wanaweza kuidhoofisha
serikali badala ya kuipa nguvu.
Ajenda yetu iwe moja tu, ‘kulijenga taifa.’ Si kitu kingine.
Tutumie busara za mwalimu ili taifa liende mbele kimaendeleo. Wapinzani
wasiogopwe wala wasichukuliwe kama maadui wa serikali. Serikali isionekane
haifanyi chochote. Pale wanapofanya vyema wapewe motisha na wapinzani kusonga
mbele badala ya kuidhoofisha serikali kwa kauli za vitisho na kupoteza muda
kukimbizana barabarani na mahakamani.
Tufanye shughuli za maendeleo kama watanzania na kuacha itikadi
za vyama pembeni,” Amesistiza Kiongozi huyo. Pia alivishauri vyombo vya dola
kuongoza nchi kwa mujibu wa sheria na kanuni zinazosimamiwa na Katiba ya nchi
bila kukandamiza demokrasia.
Amesisitiza kuwa, hayo lazima jamii hususani wanasiasa
wayatafakari kwani bila hekima baada ya UKUTA na kususia vikao vya bunge
linaweza likatokea jingine kubwa zaidi litakaloushtua ulimwengu.
Na Sarah Pelaji, Dar es Salaam
Comments
Post a Comment