JIMBO KATOLIKI MAHENGE LAWAMWAGIA NEEMA WANAKIJIJI
KANISA KATOLIKI nchini limeendelea
kuinjilisha kwa vitendo katika Jimbo Katoliki Mahenge baada ya kuwafikishia
huduma ya nishati ya umeme wananchi zaidi ya elfu nane wa kijiji cha Lugalawa-
Ludewa mkoa wa Njombe.
Akizungumza
na gazeti hili, Mkurugenzi wa maendeleo jimboni humo Padri Nestory ameeleza kuwa, Kanisa kama mama wa wote limeamua
kuwagusa watu waishio vijijini ambao wametengwa na huduma za msingi za kijamii
ikiwemo umeme, maji, hospitali nk.
“Tumeamua
kusambaza umeme vijijini ili wananchi wapate fursa ya kujiendeleza kiuchumi na
kuwa na unafuu wa maisha. Umeme huo una Megawati 1.7 ambao unasambazwa kwenye vijiji
20, shule za msingi na sekondari 43, vituo vya afya na zahanati 19, viwanda
vidogo na vya kati 340 pamoja na
hospitali moja.
Hospitali
na vituo vya afya vinahitaji umeme wa kudumu ambao utawawezesha kutoa huduma
kwa kiwango kinachostahili. Viwanda vitaweza kuzalisha kwa haraka, wakulima
watapata soko la uhakika na wafanya biashara wataweza kufanya biashara kwa
wakati na watapata soko. Kwa kuanza tunaanza kuwasambazia watu elfu nne halafu
tutaendelea na elfu nne waliobaki.
Umeme
huo ni mwingi hivyo baada ya kuwasambazia watu elfu nane utakaobaki tutawauzia
TANESCO,” ameeleza Padri Nestory.
Amesema
kuwa, mradi huo wa kupeleka umeme vijijini utaisha Juni, 2018. Kwa sasa
taratibu zote za kisheria na kitaalamu zimekamilika ambapo zinafanyika harakati
za kusimika nguzo, kufunga nyanya na mambo mengine.
Ameeleza
kuwa, si umeme tu bali jimbo hilo limeanzisha mradi wa ‘Soya ni pesa.’ Mradi
huo ni kwa ajili ya kuondoa umasikini vijijini kwa kuwapatia mbegu ya soya
wakulima hao ili walime kwa utaalamu na kukidhi mahitaji ya soko.
“Tuliona
kuwa, soya ni moja ya zao lenye soko hapa nchini. Mradi huu umefadhiliwa na US
Agricultural Department kupitia Catholic Relief service hapa nchini.
Tunachokitaka
ni kuongeza uzalishaji wa soya vijijini . Hivyo tunatoa semina juu ya kuchagua mbegu inayofaa, namna ya
kuzalisha, kuvuna na kutunza ili kupata
mazao mengi yenye ubora wa soko.
Mradi
huo umeongeza mradi ndani yake wa kufuga kuku. Soya ni chakula bora cha kuku.
Hivyo mkulima akilima soya, wakati anavuna anapata chakula chake, mazao ya
kuuza na chakula cha kuku.
Hivyo
tunawapa mbegu ya soya na vifaranga ili waweze kulima na kufuga kwa pamoja.
Mradi
huu umekuwa na mafanikio makubwa yanayoridhisha kwani baadhi yao tayari
wamejenga nyumba, wanasomesha watoto na kujiinua kiuchumi,” amesema Padri
Nestori.
Amesema
kuwa, kwa mwaka jana na mwaka huu soko la soya limeongezeka kwani kilo moja
wakulima hao wameuza kwa shilingi 1200 na kuna uhitaji mkubwa wa soya nchini.
Lengo la
miradi hiyo ni kutaka tu kumuinua maskini kutoka katika hali duni na kuishi
maisha bora ambayo anapata mahitaji yote ya msingi kwa mwanadamu.
Comments
Post a Comment