HISTORIA FUPI YA UPADRI NA UINJILISHAJI TANZANIA-KUELEKEA JUBILEI YA MIAKA 150 YA UINJILISHAJI HUKO BUKOBA
Nini maana ya Jubilei
KABLA hatujaendelea na maelezo juu ya historia ya Upadri nchini Tanzania na Uinjilishaji, kwanza tueleze kwa ufupi
maana ya Jubilei. Neno Jubilei linatokana na neno la kiebrania lina maana ya
kupiga tarumbeta kwa sababu ya furaha, uhuru na
kutubu baada ya kumaliza miaka hamsini.
Neno hili baada ya kuingia katika Kanisa Katoliki lina
maana ya mwaka wa furaha, kumshukuru Mungu kwa baraka zake, kujipatanisha na
Mungu kama una dhambi ulizotenda hasa kwa kuomba msamaha, kusamehe, mwaka wa
matumaini, mwaka wa haki, mwaka wa kupokea sakramenti, mwaka wa kuweka maagano
ya kumtumikia Mungu na ndugu zako kwa furaha na amani.
Jubilei inaambatana na kufanya hija kwenye sehemu
takatifu, hii ndiyo maana tutafanya hija kwa kituo cha Hija cha Bikira Maria wa
ludi kilichopo parokia ya Mugana, katika kufunga Jubilei wa Upadri tutafanya
hija katika kituo cha Hija huko Bwanga Jimbo Kuu la Dodoma, hivyo hivyo katika
kufunga Jubilei ya Unjilishaji nchini Tanzania
tufanya Hija katika Kituo cha hija cha Bagamoyo – Mlango wa Imani.
Uzinduzi wa jubilei
Baada ya kupata maana ya Jubilei hebu tuangalie tarehe za
Uzinduzi wa Jubilei. Tarehe 1/10/2016, itazinduliwa
Jubilei ya Miaka 150 ya Uinjilishaji ambayo tunategemea kilele chake kitakuwa
28/10/2018 kwenye kituo cha kitaifa cha hija- huko Bagamoyo- mlango wa Imani.
Siku hiyo pia itakuwa ya uzinduzi wa jubilei ya upadri
katika Tanzania ambayo tunategemea kilele chake kitakuwa tarehe 15/8/2017 huko
jimbo Kuu la Dodoma kituo cha Hija cha
Bwanga. Mapadri wa Kwanza walipadrishwa tarehe 15/8/1917 parokia ya Rubya Jimbo
Katoliki Bukoba. Kama tunavyoona Jubilei ya upadri ipo ndani ya Jubilei ya
Uinijilishaji. Haya matukio yanagusa Kanisa zima la Tanzania kwa sababu
yanagusa Imani yetu.
Kwa hiyo tunawaalika
na kuhamasisha mapadri, watawa, waamini wote na watu wenye mapenzi mema kuhudhuria sherehe
za uzinduzi wa Jubilei ya miaka 150 ya Uinjilishaji na miaka 100 ya upadri
katika Tanzania, utakaofanyika katika seminari ya Rubya jimboni Bukoba.
Pia kujiandalia sherehe za Kilele cha jubilei ya upadri na Kilele cha Jubilei ya Uinjilishaji
kwa tarehe zilizotajwa hapo. Tunapojiandaa kuadhimsha jubilei hizo tutajiandaa
kiroho kwa semina, mafungo na kufanya hija katika vituo vya hija vya majimbo
yetu, vya kanda na kimataifa.
Tarehe 1/10/2016 ilichaguliwa kuwa siku ya uzinduzi wa
jubilei hizo kwa sababu ni sikukuu ya Mtakatifu Theresia wa Mtoto Yesu mlinzi
wa misioni, mwanzo wa mwezi wa umisionari (Uinjilishaji) na Rozari takatifu,
mapadri wa kwanza wa Rwanda waliosomea Rubya walipadrishwa tarehe hiyo na mwisho ni siku ya kukumbuka kifo cha
mwanzilishi wa Shirika la Roho Mtakatifu la
Francois Poullart des Places ambalo liliinjilisha sehemu kubwa ya
Tanzania.
Wakati wa Jubilei ni wakati wa
kujitathimini
Kwa upande wa Upadri, ni nafasi ya kumshukuru Mungu kwa
baraka zake kwa zawadi ya Sakramenti ya Upadri,
kwa mapadri 4 kutoka Tanzania na mapadri
3 kutoka Rwanda. Kwa kuinuliwa katika daraja la upadri walionyesha kuwa inawezekana. Kwa hiyo ni
nafasi ya kujitathimini, je zawadi hii tuliyopewa tunaiishi namna gani?
Je tuna changamoto
zipi katika maisha yetu na kutafuta dawa ya changamoto hizo. Kwa upande wa
Uinjilishaji tunaangalia zawadi ya Furaha ya Injili tuliyoipata na tunamshukuru Mungu.
Tunaangalia maisha yetu ya Kiroho na maendeleo ya mwanadamu yaliyoletwa na
ukristo hasa elimu ya Mungu na ya dunia,
shule, hospitali hata siku hizi tunaongelea vyuo vikuu, tunajitathimini ,
changamoto zilizopo na kuangalia namna
ya kwenda mbele.
Historia fupi ya seminari ya Rubya-
mapadri wa kwanza walipopatikana
Seminari hii ya Rubya ilianzishwa Novemba 1903
huko Kyegoroma Jimbo la Bukoba parokia ya Kagondo na Askofu John Joseph
Hirth ( Mjerumani- kutoka eneo la Alsace ). Huyu alipokuwa Uganda pia alianzisha seminari ya Villa Maria huko
Uganda.
Katika nchi ya Uganda walipata mapadri wa kwanza mwaka
1913. Wakiwa ni padri Victor Mukasa Womeraka na Bazilio Lumu. Hawa mapadri
walizikwa katika Kanisa Kuu la Villa Maria alipozikwa Askofu Streicher na
Adrian Dgungu.
Waseminarist walioanzia
Kyegoromora walihamishiwa seminari ya Rubya
tarehe 21 Novemba 1904. Seminari
ilianza na waseminari 30 na kufika
Novemba 27 mwaka 1904 walikuwa 55. Rubya ilichaguliwa kuwa sehemu ya seminari
kwa sababu ipo mlimani, Askofu John
Joseph aliona ni sehemu nzuri hasa kwa waseminari waliotoka nchi za Rwanda na
Burundi waliozoea sehemu ya milima.
Wakati huo seminari ilikuwa chini ya vikariati ya
Viktoria Nyanza ambayo iliongozwa na Askofu John Joseph Hirth. Wakati huo vikariati hii ya Viktoria Nyanza
ilijumuisha majimbo ya sasa Geita, Mwanza, Musoma, Kayanga, Rwanda, Bunda,
Bukoba, Rulenge- Ngara, nchi ya Rwanda na Burundi.
Kwa hiyo waseminarista walitoka katika maeneo hayo.
Waseminarista hawa baada ya kumaliza masomo yao ya seminari ndogo ya Rubya
waliingia seminari kuu ya Rubya Mtakatifu Leo mwaka Oktoba 1909 wakiwa na
waseminarista 18. Kati ya hao waliofikia upadri walikuwa wanafunzi 7.
Waseminarista walioingia
mwaka 1903 hakuna aliyefikia daraja Takatifu la Upadri. Wale ambao
walipewa daraja la upadri wa kwanza
walitoka mwaka 1904 ambao walisajiliwa
wakiwa wanafunzi 33, mwaka huo walitoka
mapadri watano ambao ni Pd. Celestini Kipanda toka Ukerewe- Jimbo la Bunda, Pd.
Barthasar Kafuko toka Nsasa Rwanda, Pd. Donatus Leberaho toka Issavi Rwanda, Pd.Josephus Bugondo toka Issavi Rwanda naPd.
Oscar Kyakaraba Jimbo la Bukoba.
Wale waliosajiliwa mwaka 1905 wakiwa 11, waliofikiwa daraja la Upadri
walikuwa Pd. Angelus Mwilabure kutoka Kome Jimbo katoliki Geita na Pd.
Wilbard Mupapi kutoka Jimbo katoliki Bukoba.
Tarehe (15/8/1917)
mapadri wa Vikariati ya Viktoria Nyanza walipopewa daraja la upadri, pia padri wa
kwanza wa nchi ya Jamhuri ya watu wa Kongo(ikijulikana kama Upper Congo) Padri
Stephano Kaoze naye alipata daraja la Upadri katika sehemu ya Baudouinville.
Na Jovitus Mwijage
Waitu mbakasinge kutumanyisa
ReplyDelete