TAASISI ZA KIDINI KUWENI MACHO NA ARDHI MNAYOMILIKI-WAZIRI AONYA
Stan Likomawagi na Rodrick Minja, Dodoma
BARAZA la Maaskofu Tanzania (TEC),
Mtandao wa Tume ya Haki na Amani Afrika (AFJN),Wamissionari wa Damu Takatifu ya
Yesu na baadhi ya taasisi za Kiraia
wameandaa Kongamano juu ya haki katika uporaji wa ardhi, madhara kwa
aatanzania na Afrika.
Kongamano hilo
la siku mbili limefanyika Septemba 14-15 mwaka huu mjini Dodoma katika
Hoteli ya Mtakatifu Gaspar likiwashirikisha wanamazingira, wasomi, watunga
sera, wakulima,Viongozi wa Dini, wawakilishi wa taasisi za kiraia na wadau
wengine.
Katika kufungua
Kongamano hilo, Naibu waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt
Angelina Mabula amezitahadharisha taasisi za kidini hapa nchini kuhakikisha
zinakuwa na hati ya umiliki wa maeneo ya ardhi waliyoyanunua kwaajili ya
shughuli mbalimbali za maendeleo.
Amesema kuwa,
Serikali inatambua juhudi kubwa zinazofanywa na mashirika au taasisi za kidini
katika kuleta maendeleo hasa kwa kujenga shule, zahanati, hospitali na miradi
mingine.
Hivyo zinahitaji ardhi ya kutosha lakini ili
ziepuke migogoro na matatizo ya uporaji wa ardhi lazima zihakikishe zinakuwa na
hati miliki za maeneo waliyonunua.
Dkt Mabula amesema
kuwa, tatizo la uporaji wa ardhi Barani Afrika ni kubwa mno na linatishia amani
na ustawi wa bara hili, hata hivyo kumekuwa na namna tofauti za kulitazama
tatizo hilo.
Amefafanua kuwa
wakati mwingine kumekuwa na mkanganyiko miongoni mwa wadau juu ya nini hasa
maana ya uporaji wa ardhi hivyo aliwataka washiriki wa kongamano hilo katika
mijadala yao waje na uelewa wa pamoja wa dhana hii ili iwe rahisi kushughulikia
tatizo hilo.
“Wakati mwingine
matukio ya uporaji wa ardhi yamekuzwa kupita kiasi na vyombo vya habari
,wanaharakati au wanasiasa ambao wana malengo ya kushinda chaguzi hali ambayo
hukimbiza wawekezaji wazuri ambao wanahitaji kukuza uchumi na kuboresha maisha
ya watanzania” amesema waziri Mabula.
Hata hivyo
alisisitiza kuwa ardhi ni rasilimali ambayo ni lazima impatie manufaa mmiliki. Ardhi
isiyotumika vizuri kiuzalishaji haina maana.
Amesema kuwa, serikali
imekuwa ikiboresha mazingira bora ya uwekezaji katika ardhi ili wananchi wa
kawaida na wawekezaji wakubwa wapate kipato kutokana na Ardhi yao. Ametaja
juhudi hizo za Serikali ni pamoja na kupanga, kupima na kumilikisha ardhi kwa
kutoa hati za kawaida na hati za kimila.
Waziri Mabula
amesema kuwa, katika kuhakikisha taratibu na sheria zinafuatwa katika umiliki
wa ardhi kwa sasa serikali imeanza kutwaa ardhi kwa watu waliohodhi maeneo
makubwa hasa vijijini bila ya kuyaendeleza katika baadhi ya mikoa ikiwemo Tanga
na mengineyo na pia itatwaa viwanja visivyoendelezwa.
“Utakuta katika
baadhi ya maeneo hasa vijiji kuna watu wamehodhi mashamba makubwa ambayo
yamegeuka mapori bila ya kuyaendeleza hali hii inasababisha chuki baina ya wamiliki
na wananchi ambao hawana ardhi kwa ajili ya shughuli mbalimbali ikiwemo kilimo
na ufugaji kitendo kinachosababisha kuvamia eneo hilo na kujigawiya,” amesema
waziri huyo.
Kwa upande wake
Mkurugenzi Mtandao wa Haki na Amani Afrika Padri Aniedi Okure amesema kuwa,
tatizo la uporaji wa ardhi katika bara la Afrika ni kubwa kwani asilimia 50.
Amesema hali hii
inatokana na kukithiri kwa vitendo vya Rushwa ambayo imekuwa ni saratani katika
kukuza maendeleo kwa nchi za Afrika pamoja na ukosefu wa uadilifu na utawala
bora baadhi ya viongozi.
Padri Okule ameongeza
kwamba, wananchi wamekuwa wakihadaiwa kupitia kivuli cha uwekezaji kwamba
wakitoa ardhi watapata maendeleo lakini baadaye hawanufaiki na jambo lolote
kutoka kwa wawekezaji hali inayosababisha chuki na migogoro isiyokwisha.
Comments
Post a Comment