MIAKA 150 YA UINJILISHAJI TANZANIA NA 100 YA UPADRI KUZINDULIWA BUKOBA OKTOBA MOSI
KANISA Katoliki nchini linatarajia kuzindua Jubilei ya
Miaka 150 ya Uinjilishaji Tanzania Bara na miaka 100 ya Upadri Mosi Octoba 2016
huko Rubya Jimbo Katoliki Bukoba.
Taarifa
kutoka Kurugenzi ya Uchungaji ya Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania (TEC)
zimesema kuwa, siku hiyo hiyo itakuwa pia ni uzinduzi wa yubilei ya upadri
katika Tanzania ambayo kilele chake kitakuwa Agosti 15, 2017 (Mapadri wa Kwanza
walipadrishwa tarehe 15/8/1917 parokia ya Rubya Jimbo Katoliki la Bukoba) huko
Jimbo Kuu Katoliki Dodoma, pia Kanisa linatarajia kuwa na hija katika Kituo cha Bwanga huko Dodoma.
Yubilei ya
upadri ipo ndani ya Yubilei ya Uinijilishaji, hivyo matukio hayo yote yanagusa
Kanisa zima la Tanzania kwa sababu yanagusa Imani ya Kanisa Katoliki.
Hivyo
waamini, mapadri, watawa na watu wote wenye mapenzi mema wanaalikwa na
kuhamasishwa kuhudhuria sherehe za uzinduzi wa Yubilei ya miaka 150 ya
Uinjilishaji na miaka 100 ya upadri katika Tanzania, utakaofanyika katika
seminari ya Rubya jimboni Bukoba.
Taarifa hizo
pia zinaeleza kuwa, Mosi Oktoba mwaka huu
ilichaguliwa kuwa siku ya uzinduzi wa yubilei hizo kwa sababu ni sikukuu
ya Mtakatifu Theresia wa Mtoto Yesu mlinzi wa misioni, mwanzo wa mwezi wa
umisionari (Uinjilishaji) na Rozari Takatifu, mapadri wa kwanza wa Rwanda
waliosomea Rubya walipadrishwa tarehe
hiyo na ni siku ya kukumbuka kifo cha mwanzilishi wa Shirika la Roho
Mtakatifu....... ambalo liliinjilisha Afrika ya Mashiriki.
Kwakuwa
sherehe hizo ni za kitaifa, waamini kutoka majimbo yote 34 ya Kanisa Katoliki
nchini wanaaswa kushiriki wakiongozwa na utaratibu uliopangwa kuwa siku ya
kufika Bukoba ni Septemba 30, 2016 na kuondoka Oktoba 3, 2016.
Uzinduzi
utakuwa Mosi Oktoba 2016 na kutakuwa na Hija huko Nyakijoga Oktoba 2, 2016.
Gharama za kila mshiriki bila kuweka nauli ya
kwenda huko Bukoba ni TZS 150,000/=.
Fedha hiyo itagharamia milo yote utakapokuwa kule tangu tarehe 30/9
mchana mpaka siku ya kuondoka tarehe 3/10 asubuhi, malazi kwa siku tatu,
usafiri wa kutoka Bukoba kwenda Seminari ya Rubya, kutoka Seminari Rubya kwenda
Parokia ya Mugana kwa Hija Nyakijoga na kurudi Bukoba.
Mapadri
wanakumbushwa kwenda na mavazi meupe ndiyo yatakayotumika katika Liturujia
siku hizo.
Askofu Kilaini
azungumza
Askofu
Msaidizi Jimbo Katoliki Bukoba Mhashamu Methodius Kilaini amezitaja Yubilee
hizo kama matunda ya uinjilishaji toka mwaka 1868 ulipoingia Bagamoyo.
‘Katika
Yubilee hizi ambazo zitazinduliwa huko Rubya ni katika kusherekea miaka 100 ya
upadri toka mwaka 1917 tulipopata mapadri wa kwanza ambazo kilele chake ni
mwaka 2017 na miaka 150 ya uinjilishaji Tanzania bara ambazo kilele chake ni
mwaka 2018’ amesema Askofu Kilaini.
Pia
aliongeza kwa, Yubilei ya miaka 100 ya upadri na 150 ya Uinjilishaji Tanzania
Bara zinazinduliwa kwa pamoja kwa sababu ni matukio makuu mawili yanayofanana
kwa sababu uinjilishaji ndio uliotuletea mapadri wazawa.
‘Tunawakaribisha maaskofu, mapadri watawa na waamini
wote katika uzinduzi huo wa kipekee hapa Bukoba ili tuweze kuimarisha imani yetu
na kufahamu ni wapi imani yetu ilitoka’ amesema Askofu kilaini.
Katika
uzinduzi huo kivutio kikubwa ni katika Seminari ya Kwanza Kuu ya Mtakatifu Leo
ambapo jengo lake bado lipo mpaka leo na ndilo liliokuwa likitumika kama darasa
na wakati mwingine kama bweni.
‘Seminari
ya Mtakatifu leo bado ipo lakini majengo mengine yaliyokuwa yamejengwa kwa
msonge yalishabomoka lakini tunaimani watakaokuja watajifunza kitu kutoka
katika seminari hiyo,’ameeleza.
Historia ya
uinjilishaji Tanzania Bara.
Kanisa
katoliki lilianza kazi yake Tanzania Bara miaka 150 iliyopita ikitokea Zanzibar
mwaka 1868.
Historia
yake inaanza mwaka 1860, Askofu Maupoint wa Reunion alipomtuma Padri wake Fava
pamoja na watawa kuanzisha mission ya Zanzibar.
Kwa
bahati mbaya kwa wakati ule Zanzibar ilikuwa ni kitovu cha biashara ya utumwa
na asilimia kubwa ya wakazi wa Zanzibar walikuwa waislam hivyo kufanya ugumu wa
kupata wazawa wa kuweza kuwabatiza na kukuza imani katika Zanzibar.
Lakini
kwa sababu Askofu Maupoint asingeweza kufanya kazi kubwa sana aliomba shirika
la Roho Mtakatifu ili liweze kuja na kusaidia katika uinjilishaji wa Zanzibar.
Kutokana
na changamoto za biashara ya utumwa Zanzibar, Shirika la Roho Mtakatifu lilihamishia
uinjilishaji wao Tanzania Bara baada ya kuona hawapati matunda ya kazi yao
ingawa walibaki na kituo cha kuendelea kufanya kazi Zanzibar.
Mnamo tarehe 4 march 1868 Shirika la Roho
Mtakatifu lilikuja na mapadri wawili, Padri Antoine Horner na Padri Etienne
Baur pamoja na mabruda wawili Celestine na Feliocian walifika Bagamoyo na
kuanzisha uinjilishaji.
Ingawa
walikutana na changamoto mbalimbali huko Bagamoyo wamisionari hao walianzisha
vijiji vya watumwa ili kuweza kuwakomboa watumwa na hata waingereza
walipokomesha biashara hiyo shirika la Roho Mtakatifu walipata watumwa wengi sana
kutoka kwa waingereza kama ishara ya kumaliza biashara ya watumwa.
Licha
ya kupata shida nyingi ikiwa ni pamoja na ugonjwa wa malaria, wamisionari hao
walianza kueneza injili katika maeneo yote waliyokuwa wakipita kuingia Tanzania
Bara eneo la Morogoro na mwaka 1890
walifika katika maeneo ya mlima
Kilimanjaro na kusali misa yao ya kwanza katika mlima kilimanjao ikiwa pia na
kuukabidhi mlima huo kwa Mama Maria na ukawa mwanzo mkubwa wa mafanikio ya
uinjilishaji hasa katika maeneo ya Vunjo na Kilimanjaro.
Mapadri
wa Roho Mtakatifu wakafungua Mission ya Kibosho baada ya Vunjo na Kilimanjaro
na kuelekea maeneo ya Rombo na Moshi ndipo wakaanza kusambaa maeneo ya Tanga,
Arusha na kufanya Arusha kuwa Makao yao Makuu mpaka sasa.
Baada
ya Shirika la Roho Mtakatifu kuinjilisha sana maeneo hayo kwa wingi, Shirika la Mapadri Weupe walifuata wakitokea
Algeria walipokuwa wakifanya utume wao huko baada ya kusikia juu ya uenezaji
injili Afrika ya Mashariki na Kati.
Alikuwa
ni Baba Mtakatifu Leo wa Kumi na Tatu aliyewaruhusu Mapadri Weupe (White
Fathers) kufika Bagamoyo na kupokelewa
na mapadri wa Roho Mtakatifu. Wakaanza uinjilishaji wao katika maeneo ya
Unyanyembe Tabora.
Kutoka
hapo Mapadri Weupe waligawana katika sehemu kuu mbili, sehemu ya kwanza
ilikwenda maeneo ya kusini kuelekea Ujiji na sehemu ya pili ilikwenda maeneo ya
kaskazini kuelekea Mwanza.
Kundi
hili la kwanza lililoelekea Ujiji lilirudi baada ya kupata changamoto hasa pale
walipotaka kwenda Rwanda na kwa wakati ule Ujiji ilikuwa ni kitovu kikuu cha
biashara kiasi ambacho iliwawia ngumu kuendelea kukaa na kunya uinjilishaji
pale Ujiji.
Waliporudi
pia Tabora wahakufanikiwa sana kwa sababu Tabora yalikuwa Makao Makuu ya Mtemi
Milambo na uislamu ulikuwa umeshamiri sana hivyo walikimbilia maeneo ya Kalema
mwabao wa ziwa Tanganyika mwka 1886 na kuweka Makao yao Makuu hapo iliyokuja
kuinjilisha maeneo yote ya Sumbawanga, Mbeya na Rukwa.
Baadaye
walirudi Tabora na kukaa kwa kiasi maeneo ya kipalapala na wakafanikiwa zaidi
walipoweka kambi maeneo ya Ushirombo na kuwa mission yao kubwa katika maeneo ya
Unyanyembe. Baadye sana walirudi na kwenda tena Ujiji na Tukuyu.
Kundi
la pili lililoelekea Mwanza wao walifika kuelekea katika Ufalme wa Kabaka kwa
sababu walijua kuwa ufalme wa Kabaka kati ya Baganda kuna uwezekano mkubwa sana
wa kuinjilisha kwa maana walijuwa wakiweza kumshika mfalme wa Kabaka wataweza
kuinjilisha kabila lote na ufalme wote.
Padri
Roodey aliyekuwa maarufu sana kama Padri mapera ambaye pia aliyewaongoza Mashahidi
wa Uganda akiwa na mapadri wenzake waliweka makao yao maeneo ya Bukumbi baada
ya kupata urafiki na Mtemi Rwoma wa maeneo ya Bukumbi na kujenga Makao yao
Makuu ya Mapadri Weupe kwa upande wa kaskazini.
Mapadri
Weupe walipigana vita vya pili na mtemi wa Uganda Mwaka 1892 na kufukuzwa na
kuuwawa kwa wakristo 22 wakatoliki na 22 wakianglikana ambao ndio Mashahidi wa
Uganda.
Baadhi
yao walifanikiwa kukimbila Bukumbi na wengine wakaenda kusini mwa Ufalme wa Kabaka
uliokuwa unaitwa budu ambao makao makuu leo ni masaka.
Mwaka
1892 kundi la mapadri na wakatoliki kutoka budu walivuka na kuingia bukoba na
kufungua makao yao ya kwanza ya Missioni ya Kashozi ambayo ndiyo iliyoinjilisha
maeneo ya Rulenge -Ngara na ukanda wote wa Mkoa wa Kagera.
Ingawa
Makao Makuu ya Mapadri Weupe yalikuwa Bukumbi lakini Askofu John Hirth
aliyekuwa Askofu wa Ukanda wote wa ziwa victoria alikuwa akikaa katika mission
ya Kashozi.
Mission
hiyo ya Kashozi na wamisionary wake ndio inayotupa historia nzima ya mapadri wa
kwanza Tanzania Bara na kufunguliwa kwa seminari ya kwanza mwaka 1903 iliyokuja
kuzaa matunda ya mapadri wa kwanza.
Historia
hii ya jinsi uinjilishaji ulivyoingia Tanzania Bara miaka 150 iliyopita ndiyo
inayotoa fahari kwa Kanisa la Tanzania kufanya Yubilee ya miaka 100 toka
mapadri wa wa kwanza kupadrishwa katika Seminari ya Mtakatifu Leo Rubya Jimbo
Katoliki Bukoba mwaka 1917.
Hii ndiyo
historia ya Mapadri wa Mwanzo
Mwaka
1892 Askofu John Hirth alipofukuzwa kutoka Uganda kati ya vita ya kwanza ya
wakristo na waislam na vita ya pili kati ya waangikana na wakatoliki aliingia
Bukoba na kuanzisha mission ya kashozi mwaka 1892 na mwaka 1897 akenda kufungua
mission ya Katoke Jimbo la Rulenge-Ngara.
Baadaye
alianzisha seminari katika bonde la Kyegokola mahali ambapo walikuwa wanafanya
matambiko na penye hali ya hewa mbaya .
Kutokana
na hali hiyo, alihamisha seminari hiyo kutoka Kyegomola mwaka 1904 na kuanzisha
seminari maeneo ya Rubya ambako ni mahali penye mwinuko, hali ya hewa nzuri,
ndizi nyingi na baridi.
Hivyo
seminari ndogo ya kwanza ilianza mwaka huo 1904 huko Rubya ingawa mawazo ya
wengi walidhani anaazisha shule ya secondari ya kawaida .
Lakini
toka mwanzo Askofu hirth alitaka kuwa na mapadi waafrika hivyo alianza
kufundisha kilatini kama ulaya na masomo yote ya upadri kama ulaya pia.
Hali
hiyo iliwafanya baadhi ya wamisionari kwenda kumshitaki kwa kutoa sababu mbili
moja ikiwa anawapatia wazawa elimu kubwa mno inayowazidi waafrika na pili
anataka kuwa na mapadri wakati bado hata waamini hawajawa wengi wakutosha ambao
wengi wao walikuwa wakiamini katika mambo ya jadi.
Lakini
Askofu Hirth alisimama katika kuamini kuwa waafrika wanaweza kuwa mapadri.
Wanaseminari
wa mwanzo walitoka Kagera, wengine katika maeneo ya usukumani na kwa namana ya
kipekee katika kisiwa cha Ukerewe na Kome na wengine kutoka Rwanda na Burundi.
Mwaka
1909 Askofu Hirth alianzisha seminari Kuu ili kuwezesha wanaseminari kupata
elimu ya juu zaidi na seminari hiyo ilianza pale pale Rubya na kuitwa Seminari
Kuu ya Mtakatifu Leo Rubya.
Lakini
kuanza kwa Seminari Kuu kukachochea mgongano kati yake na mapadri wenzake kwa
sababu ya kutokuamini kwao juu ya mwafrika kuwa padri sawa sawa na mapadri wa
kizungu.
Kazi
ya kufundisha na kuandaa mapadri iliendelea na mwaka 1917 seminari ya Mtakatifu
Leo ilipata wanafunzi saba ambao
walipata upadri, wanne walitoka Tanzania na wawili Rwanda na mmoja kutoka
Burundi
Katika
hao wanne watanzania wawili walitokea Bukoba na wawili walitoka Mwanza katika
visiwa vya Ukerewe na Kome.
Mnamo
tarehe 15/8/1917 ndipo Tanzania ilipata mapadri wa kwanza waliopadrishwa katika
Seminari ya Mtakatifu Leo Rubya.
Mapadri
hao ni pamoja na Padri Wilboad Mupapi aliyetokea Kashozi Bukoba, Padri Oscar
Kyakaraba aliyetokea Kashozi Bukoba, Padri Celestine Kipanda aliyetokea
Kagunguli Ukerewe na Padri Angelo Mwilabure aliyetokea katika Visiwa vya Kome Mwanza.
Mapadri
wengine wa Rwanda wao walipata upadri Rwanda baada ya vikarieti ya Nyanza kugawanywa
na kupata vikarieti ya Kivu ndipo askofu Hirth alihamishiwa huko na aliwachukua
wanafunzi hao wawili na kuwapatia upadri tarehe 7/10/1917 huko Rwanda.
Mapadri
hao wa Rwnada walikuwa ni Padri Donatus Reberaho aliyejiunga katika Seminari ya
Rubya November 1904 akiwa ni mwanafunzi wa 42 na wa pili alikuwa ni Padri
Josephus Bugondo aliyejinga mwaka huo huo na wenzake ila yeye alikuwa
mwanafunzi wa 47 kuingia Rubya Seminari.
Padri
aliyetokea Burundi alikuwa ni Padri Balthazar Kafuko ambaye yeye alikuwa mwanafunzi
wa 38 kujiunga katika Seminari ya Rubya.
KURUGENZI YA MAWASILIANO TEC
Comments
Post a Comment