"RAIS HAJAKATAA KUONANA NA VIONGOZI WA DINI"

Viongozi wa Dini nchini, wamesema Rais JOHN MAGUFULI Hajakataa kuzungumza wala kuwapuuza viongozi hao ambao wamemuomba kukutana naye, kama inavyoenezwa na baadhi ya vyombo vya habari.

Akizungumza leo jijini, Dar es Salaam na waandishi wa habari Sheikh wa Mkoa wa Dar es Salaam Alhad Mussa Salum, amesema taarifa zilizochapishwa na gazeti la Tanzania Daima la Septemba 21 ISSN 0856 9762 toleo na.4310 sio za kweli.

“Taarifa hizo sio za kweli, taarifa hizo zimelenga kumgombanisha Rais na Viongozi wa Dini na watanzania kwa ujumla na hilo halitafanikiwa,” alisema Sheikh Alhad

Aidha Viongozi hao wamesema uamuzi wao wa kumuomba Rais kuonana naye, haujatokana na kuagizwa na UKAWA, bali umetokana na maono waliyopewa na Mwenyezi Mungu.

Amefafanua kuwa Rais MAGUFULI anawaheshimu Viongozi wa dini na mara zote amekua akiwaomba wamuombee na kusema leo ni siku ya tano tangu wamuandikie barua ya kumuomba kukutana naye na wanaimani Rais atakutana na Viongozi hao.

Ameeleza kuwa Barua hiyo imeandikwa Septemba 19 na kupelekwa siku hiyo hiyo Ikulu, ikiwa imesainiwa na Katibu Mkuu wa Bakwata, Katibu Mkuu wa CCT na Katibu Mkuu wa TEC.

“Naomba watanzania wasisikilize maneno hayo kwasababu hayana nia njema kwa Taifa letu, naamini Mh Rais tutaonana nae na tutaongelea mustakbali wa nchi katika mambo mbalimbali,” alisistisa Sheikh Alhad

 Akizungumzia utendaji wa Serikali ya Rais MAGUFULI, Sheikh ALHAD amesema Rais amerejesha nidhamu Serikalini, ukusanyaji mapato umeimarika na pia pengo kati ya wasionacho na walionacho linaanza kupungua.
 
 Na.Sheila Samba & Abushehe Nondo,Maelezo

Comments

Popular posts from this blog

SALA YA ASUBUHI:SALI HIVI..

Ujio wa Wamisionari wa Kwanza Tanzania Bara (2)

MJUE MTAKATIFU MARIA GORETTI