MAZINGIRA YANAYOIFANYA NDOA KUTAMKWA HAIKUWA NDOA TANGU MWANZO




BAADHI ya wanandoa wanapopata matatizo katika ndoa zao, wanaanza kutafuta sababu za kuzifanya ndoa hizo zitamkwe kuwa hazikuwa ndoa tangu mwanzo. Wanajua kuwa tamko kama hili likitolewa na viongozi wa Kanisa, wanandoa hawa wanaweza kutengana na hatimaye kuruhusiwa kufunga ndoa na mwanamke mwingine au na mwanaume mwingine.

Ni kweli kuwa kwa kuzingatia sheria husika za Kanisa, tamko la kuwahusu watu wawili mwanamme na mwanamke, waliokuwa wanaishi pamoja na kuonekana kama wanandoa, hawakuwa na ndoa tangu mwanzo, linaweza kutamkwa.

Mazingira ya aina gani, basi, yanaifanya ndoa ya Kikristo iwe ndoa tangu mwanzo au isiwe ndoa tangu mwanzo? Ili ndoa ya kikristo iwe ndoa tangu mwanzo, kuna masharti mawili ya Kanisa ambayo lazima yawe yamezingatiwa kwa ukamilifu wote. Sharti moja ni lile la mshikamano na umoja.

Sharti hili linalofafanuliwa na Kanuni ya Kanisa Na.1056 linasema kama ifuatavyo: “Jambo au hali muhimu sana kwa ndoa ya Kikristo kuwa ndoa ni hali ya umoja na ile ya kutotanguka kwake. Kwa ndoa za kikristo hali hii ya umoja na ya kutotanguka hupata uimara wake kutokana na ukweli kwamba ndoa ni sakramenti.”

Sharti la pili ni lile linalofafanuliwa na Kanuni ya Kanisa Na.1141 isemayo kama ifuatavyo: “Ndoa iliyoridhiwa na kukamilishwa haiwezi kutanguliwa kwa namna yoyote ile ya kibinadamu au kwa sababu iwayo yoyote isipokuwa kifo.”

Kanuni hizi mbili zinaambatana na mambo mengine matatu ambayo ni ya muhimu. Jambo la kwanza ni lile la kuwa   na nia ya dhati kabisa ya kila mmoja wao ya kulikubali agano hili la ndoa kwa kutamka maneno  ya kusikika kadamnasi ya watu. Hakuna mtu au watu wengine wawezao kutoa ridhaa hii isipokuwa hawa wawili. Wazazi wala jamaa au serikali hawawezi kutoa hiyo ridhaa. Jukumu hili ni la hawa wawili peke yao.

Jambo la pili ni kwamba ili makubaliano ya wawili hao yawe halali, ni lazima yafanywe kwa mujibu wa sheria. Makubaliano kamwe yasifanyike kwa kificho. Ndoa si jambo linalomhusu mtu binafsi bali ni suala lenye umhimu kwa jamii yote. Kutokana na ukweli huu, tendo la kufunga ndoa linapata uzito unaostahili si kwa kubadilishana ahadi kinyemela bali kwa vitendo maalumu vya wazi vinavyohitaji urasimu wa kisheria na wa kimila.

Jambo la tatu ni kwamba watu wawili hawa wanaokusudia kufunga ndoa ya kikristo wasiwe na kizuizi chochote cha kuweza kuwafanya wasiwe na uwezo wa kufunga ndoa na mtu mwingine yeyote yule au na huyu aliyeamua kufunga ndoa naye sasa.

Mambo  haya matatu yanaendana na mazingira ya aina tatu yanayoweza kusababisha ndoa itamkwe kuwa haikuwa ndoa tangu mwanzo iwapo itathibitika hapo baadaye kuwa mambo haya hayakuwa yamezingatiwa ipasavyo. Mazingira haya ni yale yanayohusiana na kasoro zinazoweza kujitokeza wakati wa tendo la makubaliano katika utaratibu wa ufungishwaji wa ndoa yenyewe na katika kujitokeza kwa vizuizi vya ndoa.

Mazingira yanayohusiana na kasoro zinazoweza kujitokeza wakati wa makubaliano:
Wanaokusudia kufunga ndoa ya Kikristo wawe na akili timamu wakati wa kutamka yale maneno ya kukubaliana. Ikithibitika hapo baadaye kuwa mmoja wao au wote wawili hawakuwa na akili timamu wakati wa kutamka yale maneno ya kukubaliana, ndoa yao inaweza kutamkwa kuwa haikuwa ndoa tangu mwanzo.

Utimamu huu wa akili umwezeshe mhusika kuelewa pia maana ya maisha ya ndoa na kumwelewa huyo mwenzake anayetaka kufunga ndoa naye. Adadisi vilevile vitu vingine kadhaa kama vile usahihi wa tabia ya huyo mwenzake isije ikawa ni tabia ya kujifanya tu ili afanikiwe kufunga ndoa naye. Uamuzi wake  kwa vyovyote usiwe na shinikizo ya aina yoyote ile kutoka nje ya utashi na dhamira yake.

Mazingira ya utaratibu wa ufungishwaji wa ndoa yenyewe:

Ndoa ya kikristo ifungishwe na Paroko wa Parokia husika, au na Askofu mahalia au na Paroko msaidizi au na yule aliyenaibishwa kwa kuzingatia sheria zilizopo na pia ifungishwe mbele ya mashahidi wawili. Sharti hili lisipozingatiwa  ndoa hiyo huwa si ndoa tangu mwanzo.

Mazingira ya uwepo wa pingamizi au vizuizi vya ndoa:

Jambo la tatu ni lile la kuwa na pingamizi au vizuio vya ndoa. Mifano ya pingamizi au vizuio hivi ni kama hii ifuatayo:
Kipingamizi cha umri: Mvulana hawezi kufunga ndoa kihalali kabla hajatimiza miaka 16 na msichana kabla hajatimiza miak 14. Lakini Baraza la Maaskofu linaweza kuamua kuufanya umri huu uwe wa juu zaidi kufuatana na mazingira ya mahali.

Ndoa halali ya awali: Mtu aliyekwishafunga ndoa kihali hapo awali, hata kama ndoa hiyo haikukamilishwa hawezi kufunga ndoa ya kikristo.

Maumbile ya kimwili yasiyo rafiki kwa tendo la ndoa: Iwapo wawili hawa wanaotarajia kufunga ndoa ya kikristo hawawezi kufanya tendo la ndoa kutokana na maumbile yao kutokuwawezesha kufanya hivyo, hawawezi kufunga ndoa.

Nadhiri za useja: Mashemasi, mapadri na maaskofu hawawezi kufunga ndoa kwa sababu wamefunga nadhiri za useja. Kibali cha kufunga ndoa kwa hao hutolewa na Papa. Hata hivyo, kibali hicho hakiwezi kutolewa kwa Maaskofu na hutolewa kwa nadra sana kwa mapadri.

Nadhiri za Kudumu za Usafi wa Moyo: Wale waliofunga nadhiri hizo katika Shirika la Kitawa hawawezi kufunga ndoa kihalali. Nadhiri za hao walizozifanya katika Shirika la Kitawa lazima pia ziwe zimepokelewa na Mkuu halali wa Shirika husika kwa niaba ya Kanisa.

Uhusiano wa karibu mno wa damu kiukoo: Baba, kwa mfano, hawezi kufunga ndoa na binti yake au babu na mjukuu wake. Katika sheria zake, Kanisa limepambanua ngazi mbalimbali za mahusiano haya ya karibu mno ya damu kiukoo ambayo yanaweza kuwa vizuio vya ndoa.

Ndoa ya Kikristo ile tu iliyofungishwa katika mazingira yaliyokubaliwa na Kanisa Katoliki kwa kuzingatia sheria na utaratibu wote ulioainishwa na Kanisa hilo huwa ndoa tangu mwanzo. Lakini ikithibitika wakati wowote hapo baadaye kuwa utaratibu ulikiukwa, ndoa husika hutamkwa kuwa haikuwa ndoa tangu mwanzo.

 Na Philip Komba

Mwandishi ni Mhadhiri mstaafu,
Chuo Kikuu Huria cha Tanzania,
Dar es Salaam.
0754 054 004


    


       
    

Comments

Popular posts from this blog

SALA YA ASUBUHI:SALI HIVI..

Ujio wa Wamisionari wa Kwanza Tanzania Bara (2)

MJUE MTAKATIFU MARIA GORETTI