MAAFA YA TETEMEKO KAGERA, WAZIRI MKUU AWAAGA MAREHEMU WAKATI JINGINE LIKITOKEA TENA JUMAPILI
WAZIRI
MKUU Kassim Majaliwa ameongoza maelfu ya wananchi wa Manispaa ya Bukoba
mjini kuaga miili ya watu 16 waliofariki kutokana na tetemeko la ardhi
lililotokea Jumamosi, 10 Septemba, 2016 mkoani Kagera.
Tetemeko hilo limesababisha vifo vya watu 16 na wengine 253 kujeruhiwa. Pia limesababisha maelfu ya wananchi kukosa makazi baada ya nyumba 840 kuanguka na nyingine 1264 zikipata nyufa yakiwemo majengo 44 ya taasisi mbalimbali za umma.
Kufuatia
tukio hilo Waziri Mkuu ambaye alimuwakilisha Mheshimiwa Rais, Dk. John
Magufuli amewaomba wananchi kuwa watulivu wakati Serikali ikiendelea
kufanya tathmini ya athari zilizotokana na maafa hayo.
“Poleni
sana tukio hili ni kubwa na halijawahi kutokea nchini. Haya yote ni
mapenzi ya Mwenyezi Mungu. Tuendelee kuwa na imani na watulivu Serikali
ipo pamoja nanyi na haitawatupa mkono,” amesema.
Waziri
Mkuu amesema Kamati ya Maafa ambayo ipo katika Ofisi ya Waziri ya Mkuu
itakwenda wilaya za Kyerwa, Karagwe na Bukoba mjini kwa ajili ya kufanya
tathmini na kubaini athari zilizosababishwa na tetemeko hilo na kuona
namna ya kuwasaidia waathirika.
Wakati
huo huo Waziri Mkuu amewaagiza viongozi wa mkoa huo kuchukua hatua za
haraka kwa kuwatafutia eneo salama la kulala wanafunzi wa Shule ya
Sekondari Nyakato ambayo mabweni yake yote yameathirika na tetemeko hilo
na hayafai kutumika.
Waziri
Mkuu ametoa agizo hilo baada ya kutembelea shule hiyo na kujionea namna
mabweni ya shule hiyo yalivyopata nyufa hali iliyosababisha wanafunzi
kulala uwanjani.
Pia
Waziri Mkuu ameiagiza Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) kuangalia
kama kuna tetemeko linguine linaweza kutokea nchini ili Serikali iweze
kuchukua tahadhari pamoja na kutoa elimu kwa umma namna ya kujikinga.
Naye
Mkuu wa Mkoa wa Kagera, Meja Jenerali Mstaafu, Salum Kijuu amesema kwa
sasa wanaendelea na jukumu la kuwatafutia makazi wananchi ambao nyumba
zao zimeanguka. Pia mkoa unaendelea kufanya tathmini ya kina kujua
athari zilizosababishwa na tetemeko hilo.
Awali
Waziri Mkuu alitembelea Hospitali ya Mkoa wa Kagera ambako majeruhi 170
wamelazwa na kutoa pole na kwamba anawaombea kwa Mwenyezi Mungu wapone
haraka na wenye matatizo ambayo yanahitaji matibabu kwenye hoispitali
kubwa Serikali itahakikisha wanapelekwa huko na kuhudumiwa.
IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU,
Comments
Post a Comment