"AFRIKA INAHITAJI MARAISI 50 KAMA MAGUFULI"
Na
Stanslaus Likomawagi, Dodoma
MKURUGENZI
wa Mtandao wa Tume ya Haki na Amani Afrika (yenye makao yake makuu mjini
Washinton nchini Marekani) Padri Ariedi Okure wa Kanisa Katoliki amesema kuwa,
Bara la Afrika linahitaji maraisi 50 kama Dkt. John Magufuli ambao watasaidia
kujenga uadilifu katika Serikali, kukuza maendeleo na kujali watu wanyonge
zaidi.
Padri Okure ambaye ni Raia wa Nigeria amesema hayo hivi
karibuni Septemba 15 mwaka huu wakati
akizungumza na mwandishi wa habari mara baada ya kumalizika Kongamano juu ya
haki katika Uporaji Ardhi na madhara kwa Watanzania na Afrika lililofanyika
mjini Dodoma.
Ameweka wazi kuwa, yeye ni mwafrika anayefanya kazi ughaibuni
lakini anajivunia sana pale anapoona juhudi kubwa anazozifanya Rais Magufuli
ambazo zimemjengea heshima ndani na nje ya Bara la Afrika. Ameeleza kuwa,
utendaji wake ni mzuri hauwezi kuulinganisha na Maraisi wengine wa Afrika.
Aidha amefafanua kuwa Dkt. Magufuli ameonyesha kwa dhati
kuwa anawapenda wanyonge na anataka rasilimali za Tanzania ziwanufaishe watu
wote wa nchi hii.
“Nikiwa Marekani nilifurahishwa na hatua yake ya kuamua
fedha za maadhimisho ya sherehe za uhuru wa Tanzania zielekezwe kwenye miradi
ya maendeleo kwa ajili ya kuwasaidia watu.
Hata zile fedha za hafla ya yeye kuzindua Bunge la 11
kuzipeleka Hospitali ya Taifa Muhimbili kununua vitanda na magodoro kwa
wagonjwa ilitoa fundisho kwa dunia na kwa viongozi kuwa na moyo wa kuwasaidia
wahitaji na wenye shida,” amesema Padri Okure.
Pia amefafanua kuwa, Raisi Magufuli anapaswa kuungwa mkono
na Watanzania wote wenye mapenzi mema katika jitihada zake za kujenga Tanzania
mpya na siyo kumkatisha tamaa.
“Najua hata maandiko yanasema Yesu alipingwa na maadui
kutokana na kuwa mkweli, kupenda wanyonge na kusaidia wenye shida , hivyo
Magufuli ni msaada kwa wanyonge” amesema Padri Okure.
Kuhusu matatizo mbalimbali ya Bara la Afrika Padri Okure
amesema yanatokana na mambo mengi lakini kubwa ni rushwa ambayo imekuwa ni
saratani ya kuzuia maendeleo na imesababisha hata mapigano kwa watu kugombea
ardhi na rasilimali nyingine Barani humo.
Comments
Post a Comment