MUSWADA WA HABARI: WADAU WATOA MAONI
MUSWADA
wa Sheria ya upataji wa taarifa wa mwaka 2016 (The access to information bill
2016), umewasilishwa bungeni huku wadau mbalimbali wa tasnia ya habari wakitaka
taaluma ya habari ipewe hadhi stahiki.
Kiongozi imeongea na
baadhi ya wadau wa habari nchini ambapo pamoja na kupongeza hatua hiyo ya
serikali, imewataka wabunge kutoa michango itakayowezesha kuboresha na kusimamia
mambo muhimu yanayotarajiwa na wananchi.
Kwa upande wake
Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Mtakatifu Agustino Mwanza (SAUT), Mlagiri Kopoka
ameeleza kuwa, kupitia michango yao, wabunge hawana budi kusimama imara ili
haki za kupata taarifa zisiporwe tena.
“Jambo la msingi
tunalotazamia katika muswada huu ni fursa ya kupata taarifa hasa katika taasisi
za umma. Uendeshwaji wa serikali unapaswa kuwa wazi, na siyo wa siri tena.
Katika hili wabunge wetu wanatakiwa kusimama imara ili haki yetu ya kupata
taarifa isiporwe tena” ameeleza Kopoka.
Aidha Kopoka ambaye pia
ni mwandishi wa makala na vitabu, ametahadharisha kuwa matarajio ya watanzania
ni kufanyiwa marekebisho kwa vipengele vinavyopora uhuru wa kupata taarifa.
“Tusipofanya hivyo
tutajikuta tuna sheria mpya huku mambo yakiwa ni yale yale” ameongeza.
Naye Denis Mpagaze,
mwandishi na Mkuu wa Idara ya Habari na Mawasiliano katika Chuo Kikuu cha
Askofu Mkuu James Songea (AJUCO), ambacho ni Chuo Kikuu Kishiriki cha Mtakatifu
Agustino (SAUT), amesema kuwa muswada huo usaidie kufanya taaluma ya habari iheshimike.
“Kuna haja ya kuifanya
taaluma ya habari itambulike na kuheshimiwa. Na ili tasnia hii iweze kuwa
taaluma ni lazima kuwe na mafunzo ya muda mrefu, tuwe na vyuo vinavyoaminika na
vyenye ubora, wahadhiri waliobobea na bodi itakayosimamia taaluma hiyo”
ameeleza Mpagaze.
Pia Mpagaze ameweka
wazi kuwa kukithiri kwa utitiri wa vyuo visivyokuwa na sifa za kutoa mafunzo ya
uandishi wa habari, kunachangia kushuka kwa hadhi ya taaluma hiyo. Aidha
ameonya kuwa uandishi wa habari ni kazi inapaswa kufanywa na watu wenye weledi
na siyo waliokosa kazi ya kufanya.
“Zile fikra kuwa mtu
yeyote anaweza kuwa mwandishi wa habari ziishe. Unakuta mtu amemaliza darasa la
saba, kwa kuwa ana sauti nzuri basi anafaa kuwa mtangazaji. Ni lazima turatibu
taaluma ya habari ndipo mambo mengine kama maslahi ya waandishi
yatakapoboreshwa” ameongeza.
Michango
ya wabunge
Baada ya muswada huo
kupelekwa bungeni katika mkutano wa nne wa bunge la 11, Septemba 6, 2016
wabunge mbalimbali walipata fursa ya kutoa michango yao katika muswada huo.
Kwa upande wake Mbunge
wa Rufiji, Mohamed Mchengerwa amesema kuwa kupitishwa kwa muswada huo
kutawasaidia wananchi kupata taarifa kuhusu miradi na utekelezaji wa majukumu
ya serikali.
“Utasaidia upatikanaji
wa taarifa zilizopo katika chini ya himaya ya wizara na taasisi zilizopo chini
yake. Pia tutambue kuwa nchi hii ni ya wananchi. Kupitishwa kwa muswada huu
kutatoa fursa kwa wananchi wetu kupata taarifa ya utekelezaji wa miradi ya
maendeleo” ameeleza.
Tanzania itakuwa nchi
ya tano Barani Afrika kupitisha sheria ya upatikanaji wa taarifa, huku ikiwa
nchi ya 67 duniani kupitisha sheria hiyo. Nchi ya kwanza kupitisha sheria hiyo
ni Newzland, ambayo ilipitisha sheria hiyo mwaka 1766.
Maelezo
ya Waziri wa Habari, Utamaduni, Wasanii na Michezo
Akiwa mkoani Mbeya
mwezi Aprili mwaka huu, Waziri wa Habari, Utamaduni, Wasanii na Michezo Nape
Nnauye aliwaeleza wadau wa habari wa mikoa ya Mbeya na Songwe kuwa muswada huo
tayari umeshafanyiwa marekebisho, ambapo mwaka jana uliondolewa bungeni baada
ya kupigiwa kelele na wadau kuwa ulihitaji kufanyiwa marekebisho katika baadhi
ya vifungu.
Nape alieleza kuwa
muswada huo umebeba mambo mbalimbali ikiwa ni pamoja na maslahi ya waandishi wa
habari, tatizo la utitiri wa vyuo vya habari visivyokuwa na sifa ambavyo havina
budi kuondolewa, huku ukilenga kurudisha heshima ya tasnia ya habari.
“Muswada huu mzuri na utasaida kuleta
suluhishi la malalamiko ya kuwepo kwa sheria kandamizi, pia itasaidia kukuza
tansia ya habari pamoja na kuifanya tasnia ya habari kuheshimiwa kama tansia
nyingine”,amesema Nape.
Na
Pascal Mwanache, Dar es salaam
Comments
Post a Comment