Mazingira ya
Uzaliwa wa Bikira Maria Mtakatifu
UZALIWA
au siku ya kuzaliwa kwa Bikira Maria Mtakatifu, au Kuzaliwa kwa Maria, au
Kuzaliwa kwa Bikira Maria kunaihusu sikukuu moja ya Kikristo ya kumbukumbu ya
kuadhimisha Uzawa wa Bikira Maria Mtakatifu.
Hata hivyo, kumbukumbu
ya sikukuu hii haipo katika Kanuni ya siku hizi ya Kanisa Katoliki. Maelezo ya
mapema au ya mwanzo mwanzo kabisa yanayogusia Uzawa wa Bikira Mtakatifu ni yale
ya Yakobo, ambayo nayo hata hivyo, hayana uhalisia wala uthibitisho wo wote.
Maelezo haya
yanaonekana katika Sura ya 5 Aya ya 2 ya
hayo maandishi ya awali ya Yakobo ya uinjilisti. Maandishi haya yanayosema tu
kwamba Wazazi wa Maria walikuwa Mtakatifu Anna na Mtakatifu Yoakimu yaliandikwa
mwishoni mwa karne ya pili.
Kwa kawaida, Kanisa
Katoliki linakuwa na kubukumbu ya kufa kwa watakatifu na si ya kuzaliwa kwao.
Kumbukumbu ya kuzaliwa kwa Maria na ile ya kuzaliwa kwa Yohani Mbatizaji ni
kati ya zile kumbukumbu chache sana zinazozingatiwa na Kanisa Katoliki.
Uzingatiaji wa
kumbukumbu za kuzaliwa kwa Maria na ule wa kuzaliwa kwa Yohani Mbatizaji
umetokana na ule ukweli kuwa wawili hawa walikuwa wamechukua ujumbe wa pekee sana katika historia ya
ukombozi wa wanadamu. Sababu nyingine ni ile ya kimapokeo. Sababu hii ya
kimapokeo ni kwamba, hawa hawa wawili, yaani Maria na Yohani Mbatizaji walikuwa
watakatifu kuanzia kuzaliwa kwao.
Maria alikuwa
amekingiwa dhambi ya asili na mwenzake Yohani Mbatizaji alikuwa amefanywa
mtakatifu tangu alipokuwa tumboni mwa mama yake, Mtakatifu Elizabeti. Ukweli
huu ni kwa mujibu wa tafsiri ya kimapokeo ya mwinjilisti Luka kama tusomavyo
katika Lk 1:15, “Atakuwa mkuu mbele ya Bwana. Hatakunywa divai wala kileo, na
atajazwa Roho Mtakatifu tangu tumboni mwa mama yake.”
Maandishi
ya Dini ya Kiislamu kuhusu Uzawa wa Maria:
Labda utashangaa kusoma
kuwa Uzawa wa Maria umeelezwa pia katika kitabu cha Qur’an. Katika sura ya sita
ya kitabu hicho cha Qur’an, baba mzazi wa Mariam yaani Maria ametajwa kuwa
alikuwa Imran (Yoakimu?) jina ambalo limepewa Sura hiyo ya kitabu cha Qur’an.
Mama ya Mariam (Maria) alikuwa Hannah (Anna), kwa mujibu wa maelezo ya kitabu
hicho.
Hannah (Anna) alikuwa
daima anasali kumwomba Mungu amjalie kukipata kile alichokuwa anakitamani sana
katika maisha yake, yaani mtoto. Katika sala zake hizo za maombi, Hannah (Anna)
aliahidi kuwa iwapo sala zake zingesikilizwa, mtoto ambaye angempata, aliyemhisi
kuwa angekuwa wa kiume angemtoa sadaka kwa Mungu.
Hannah (Anna) aliomba
sana mtoto wake alindwe na asidhuriwe na shetani. Mapokeo ya Dini hiyo ya
Kiislamu yanaeleza kuwa watoto waliozaliwa hapa duniani bila kuguswa na shetani
ni wawili tu. Watoto hawa ni Mariam yaani Maria na Isa yaani Yesu.
Ibada kwa Maria inayotokana
na huo ukweli kwamba alikingiwa dhambi ya asili na hivyo kustahili kupata hiyo
heshima ambayo ni ya aina ya juu kabisa ya kuitwa “Bikira Maria Mkingiwa Dhambi
ya Asili” ni ibada inayozingatiwa na wengi katika ulimwengu wote wa Kikristo.
Yale maandishi ya
Yakobo aliyokuwa ameyaandika mwishoni mwa karne ya pili, yanaeleza kuwa,
Yoakimu, baba mzazi wa Maria alikuwa mtu mwenye uwezo wa kifedha na alikuwa
tajiri katika moja wa yale makabila 12 ya Israeli. Pamoja na utajiri aliokuwa
nao, Yoakimu na mke wake Anna walikuwa wanahuzunishwa na kitu kimoja. Kitu
hicho kilikuwa kile cha kutokuwa na mtoto.
Hakuna maandishi ya
kuaminika yanayoeleza mahali alipozaliwa Maria. Maandishi mengine yanaeleza
kuwa Maria alizaliwa Nazareti, na mengine yanasema alizaliwa Yerusalemu. Vyovyote viwavyo,
inawezekana kabisa kwa mtu tajiri kama Yoakimu, kuwa na makazi Yudea na pia
Galilea.
Tarehe ya sikukuu:
Kimapokeo, tukio hili huadhimishwa tarehe ya 8 ya mwezi wa Septemba kama
sikukuu ya Kiliturujia kwa mujibu wa Kalenda Kuu ya Kanisa Katoliki. Waamini wa
Makanisa ya Kianglikana nao huadhimisha sikukuu hiyo tarehe hiyo hiyo ya 8 ya
mwezi huo wa Septemba kwa mujibu wa Kalenda za Makanisa hayo ya Kianglikana.
Tarehe hiyo ya 8 ya
mwezi wa Septemba huwa imepita miezi 9 baada ya Sherehe ya Bikira Maria
Mtakatifu Mkingiwa Dhambi ya Asili. Sherehe ya Maria Mtakatifu Mkingiwa Dhambi
ya Asili inasherehekewa tarehe ya 8 ya mwezi wa Disemba.
Maandishi ya awali
kabisa yanayohusiana na Uzawa wa Maria yanaonekana katika waraka wa karne ya
sita. Maandishi hayo yako katika wimbo unaogusia maadhimisho ya Uzawa wa Maria.
Wengi wanahisi kuwa wimbo huu ulikuwa umetungwa na kuandikwa nchini Syria kwa
sababu baada ya Mtaguso Mkuu wa Efeso Syria ilikuwa na vikundi vingi vya kidini
vilivyomshabikia sana Maria kama Mama wa Mungu.
Kumbukumbu ya kwanza ya
Kiliturujia inayohusiana na Uzawa wa Maria ni ile ya kutabarukiwa kwa Kanisa
jipya la Bikira Maria lililokuwa limejengwa mahali palipokuwa panadhaniwa kuwa
ndipo ilipokuwa nyumba ya wazazi wa Maria mjini Yerusalemu. Kanisa la kwanza
lilikuwa limejengwa mahali hapo hapo kwenye karne ya tano.
Wagriki wa Kanisa la
Kiorthodoksi huadhimisha pia sikukuu hiyo ya Kuzaliwa Bikira Maria Mtakatifu
tarehe hiyo hiyo ya 8 ya mwezi wa Septemba. Sikukuu hiyo huadhimishwa pia na
Wakristo wa nchi ya Syria. Hawa nao huadhimisha sikukuu hiyo tarehe hiyo hiyo
ya 8 ya mwezi huo wa Septemba.
Kwa kuwa maelezo ya
Kuzaliwa kwa Maria yalikuwa yamefika kama hadithi kutokana na maandishi ya
Yakobo ambayo hayakuwa na uthibitisho wowote, Kanisa Katoliki lilichelewa sana
kuiasili sikukuu hiyo. Sikukuu ya Kuzaliwa kwa Maria ilianza kuadhimishwa Roma
kuanzia mwishoni mwa karne ya saba.
Watawa wa kiume
waliokuwa wametoka sahemu za mashariki
ndio waloifanya Roma ibadili msimamo wake wa kutokuadhimisha sikukuu hiyo na
kuifanya sasa nayo pia iwe na msisimko wa kumbukumbu ya maadhimisho maalum ya
Uzawa wa Maria.
Hatuambiwi, hata hivyo,
hawa watawa wa kiume kutoka Mashariki walikuwa na hoja gani nzito iliyoweza
kuiridhisha Roma mpaka ibadili msimamo wake uliokuwa umeshikiliwa kwa karne
kadhaa.
Na
Philip Komba
|
Holy Mary mother pray for us
ReplyDeleteMbele ya mama yetu bikira consolata malkia ni wewe na wanao ni siye vyema twajitahid kuwa watoto wako na Fadhira kuiga tufiki mbinguni Ave Maria ave maria ave maria ave ave ave mama
ReplyDelete