MUNGU ANATUTAKA TUISHI VIPI?
Kumfuatia Yesu ni kazi kubwa. Lakini wakati huohuo kwa wanaomfuata hujazwa na furaha kubwa ,hupata ufahamu na ujasiri wa kumtambua Mungu katika watu maskini wa maskini na hivyo hujitolea kwa moyo wote na kujenga urafiki na maskini na kuwahudumia kwa ukarimu. Baba Mtakatifu Francisko ameeleza hayo ,katika homilia yake, wakati wa Ibada , aliyoiongoza katika uwanja wa Kanisa Kuu la Mtakaifu Petro , Jumapili illiyopita , 04 .09.2016, kwa nia ya kumtangaza kuwa Mtakatifu , Mama Mpendwa Tereza wa Calcutta, Mama wa maskini. Papa aliomba ushuhuda wa Mama Tereza wa kuishi kwa kumtegemea Mungu , na uendelee kuwaleta wote hasa maskini wa maskini karibu na Mungu.
Papa katika homilia yake, akiyatazama maisha ya Mtakatifu Mama Tereza, na watu wengine wanaojitolea kuhudumu wengine bila kudai malipo, alisema utendaji a watu hawa , ni upendo wa Yesu, wenye kuwapa msukumo kutoka ndani ya moyo, kwenda kutumikia maskini na wahitaji, bila kutarajia shukrani yoyote au malipo, badala yake wanaonekana kujikatalia yote , kwa sababu wameugundua upendo wa kweli.
Aliendelea kusema, faraja yao ni kuinamia mtu maskini na mhitaji, kama ilivyo kwa Bwana wao ambaye alikuja duniani na kujishusha chini, akiwainamia wote hasa wale waliopoteza imani na wale wanaoishi kama kwamba Mungu hayupo. Papa alisisitiza kuwa Yesu anawainamia wote, hasa vijana waliopoteza maadili , familia zilizo katika kipeo cha maisha , wagonjwa wote , wafungwa, wakimbizi na wahamaiji , na wanyonge wasioweza kujitetea wenyewe kimwili na kiroho pia , watoto waliotelekezwa na wazee walioachwa wenyewe. Yesu yuko kila mahali ambako mtu anatafuta msaada ili apate kuinuka.
Papa alitaja kwa hao , hapo ndipo uwepo wa mfuasi wa Kristo na Kanisa unatakiwa kuwepo , kutoa farija na matumaini mapya kama jambo la lazima kwa mfuasi wa Yeu na Kanisa .
Homilia ya Papa ililenga katika masomo ya liturujia ya neno la siku, somo la kwanza lilitoka Kitabu cha Methali (9;13 ). Kabla ya maelezo yake, Papa Francisko alihojii "Nani anaweza kujifunza shauri la Mungu?". Alitoa ufafanuzi kwamba, swali hili kutoka Kitabu cha Methali, linaonyesha kwamba, maisha yetu ni Siri ya Mungu, na kwamba hatuna ufunguo wa ufahamu juu ya hilo, ila tunatambua kwamba, katika maisha watendaji wakuu husika katika historia yote ya maisha ni Mungu na mwanadamu. Na hivyo sisi kama binadamu kazi yetu ni kuitikia kile Mungu anachotaka tutende katika maisha yetu. Ni kufanya mapenzi yake.
Papa aliendelea kuhoji kwa namna gani tunaweza itikia kufanya mapenzi ya Mungu katika maisha yetu? Alitoa jibu akisema, kwanza zaidi ya yote ni lazima kujifunza yapi yanampendeza Mungu . Kuelewa Mungu anataka nini, na haya tunaweza kujifunza kutoka katika maisha ya Manabii na watakatifu, Maisha yao hutangaza yale yaliyompendeza Mungu.
Na kwamba, kwa kifupi maisha yao hutoa jibu la kushangaza , lililoandikwa katika Kitabu cha Hosea na Injili: "Nataka huruma, wala si sadaka" (Hos 6: 6; Mt 9:13). Kumbe Mungu anaridhia kila tendo la huruma, kwa sababu katika kusaiidia watu wahitaji wake kwa waume , tunatambua uso wa Mungu ambao hakuna mtu anaweza kuona hivihivi tu (cf. Yohana 1:18). Kila wakati tunapo wainamia watu wahitaji na kutoa msaada wetu , iwe msaada wa chakula, kinywaji au mavazi ,tunakutana na Yesu, tunamwona Mwana wa Mungu (Mat 25:40).
Papa aliendelea kuzungumzia utendaji halisi , kama tunavyoomba katika sala na kukiri hakuna mbadala wa upendo: wale ambao kwa riadhaa yao hupenda kuwahudumia wengine ,wakati mwingi bila hata yakujua hilo, watu hao ni wale wanaompenda Mungu (cf. 1 Yohana 3: 16-18; Yak 2: 14-18). Hayo nidiyo maisha ya kikristo, na si tu kurefusha mkono wakati wa shida lakini daima , hupenda mshikamano na binadamu wengine bila kutafuta faida binafsi. Papa amesisitiza na kumtaka kila mwanafunzi wa Yesu anayaweka maisha yake katika utumishi wa upendo kama wajibu na si kama ajira.
Papa alieleza na kuurejea umati mkubwa wa watu waliofika Rome kwa ajili ya maadhmisho ya Jubilee ya huruma , kwa wahudumu wa kujitolea, akisema wameonyesha upendo halisi na thabiti kwa Mwalimu wao kama ilivyoadikwa katika Injili ya Luka 14:25. Papa alieleza na kufanya rejea kwa maneno ya Mtume Paulo: ”Ndugu upendo wake umeniletea furaha kubwa na kunipa moyo sana. Nawe umeichagamsha mioyo ya watu wa Mungu (Flm 1: 7)”. Papa hakuweza ficha furaha yake, hasa kwa jinsi walivyoweza leta furaha na matumaini mapya kupitia kazi zao za kujitolea. Kwa jinsi mikono yao inavyofanya kazi ya kuwainua waliokata tamaa na kupagusa machozi ya wengi , kwa jinsi walivyomwaga upendo wao kwa unyenyekevu na bila kujihurumia katika huduma . Papa anasema , huduma yao yenye kustahili kusifiwa kwa kutoa sauti ya imani, na inaonyesha huruma ya Baba, ambaye huwakaribisha na kuwapokea wahitaji wote.
Papa kisha aliyarejea maisha ya Mama Teresa wa Calicutta akisema katika nyanja zote za maisha yake, alihudumia kwa ukarimu mkubwa akionyesha huruma ya Mungu, yeye mwenyewe alikuwa tayari kumhudumia kila mtu na hasa waliowekwa pembezoni au kutelekezwa na jamii. Alikuwa n ni mtetezi wa maisha ya wote na bila kuchoka kutangaza kwamba "wasiozaliwa bado ni dhaifu , wadogo na wahitaji zaidi. Na aliwainamia wale waliokuwa katika hali za kufa , waliolala kando ya barabara ,bila msaada , lakini yeye aliwainamia na kwasaidia kwa kuwa aliiona sura yaMungu kwao. Alifanya sauti yake isikike hata mbele ya dunia yenye mamlaka , iweze kutambua kuwa na hatia ya kutowahudumia umaskini.
Mama Teresa, upendo na huruma, ilikuwa ni "chumvi" iliyoweka ladha katika kazi zake, ilikuwa ni "mwanga" uliomulikia giza la wengi waliokata tamaa katika umaskini wao na mateso yao. .
Papa Francisko alimalizia homilia yake akisema utendaji wa Mama Tereza hata leo hii ni ushuhuda fasaha muhimu sana katika kuwakaribia watu maskini walio sahaulika katika mitaa ya miji. Hivyo Mama Kanisa kwa a fadhila zake , linamweka wakfu na kumtangaza kuwa Mtakatifu , Mfano wa kuigwa na wote na hasa wanao huduma kwa kujitolea . Papa alimtangaza na kuomba msaada wake uweze kuwa kioo cha upendo wa kuhudumia bila kuchoka , katika kila hatua za itikadi na majukumu yote, kutenda kwa ukarimu na huruma kwa kila mtu bila ubaguzi wa lugha, utamaduni, rangi au dini., kama Mama Teresa alivyopenda kusema, "siwezi kuzungumza lugha yao, lakini naweza kutabasamu". Kwa maneno hayo , Papa ametoa mwaliko kwa wote kuwa na tabasamu ndani ya moyo kwa ajili ya kuwapa wale tunaokutana nao katika safari yetu ya maisha , na hasa wale wanakabiliwa na kukosa mahitaji ya lazima. Kwa namnahiyo tunafugua njia na fursa ya furaha na matumaini , kwa watu wengine wake kwa waume , kwa watu wengi a waliokata tamaa ambao wanahaja ya kueleweka na kuhurumiwa ..
Kwa msaada wa Vatican Radio
Comments
Post a Comment