AMINA, AMINA, AMINA - Kiitikio muhimu sana katika Liturujia
Kiitikio hicho tunakifahamu sisi
sote; tunaitikia mara nyingi lakini je, tunaelewa umuhimu wake? Binafsi
nikichunguza wakati wa maadhimisho mbalimbali ya Liturujia hasa Adhimisho la
Ekaristi, ni baadhi tu ya waamini wanaoitikia Amina sehemu mbalimbali wakati wa Misa. Waamini wengine huitikia kwa sauti
ya kuungama dhambi na wengine hawaitikii kabisa.
Asili yake
Kwa asili Amina ni neno la
kiebrania na maana yake ni: ni kweli
kabisa. Neno hilo lililotumika
kukubali au kuthibitisha ukweli wa maneno au jambo lililokuwa limesemwa. Kwa
hiyo mtu aliyesema Amina alitakiwa
kusikia nini kilichosemwa na ndipo akubalie:
Amina.
Neno hilo limetumika katika Agano la
Kale hasa katika Zaburi. Katika Agano Jipya Bwana Yesu alilitumia mara nyingi
alipotaka kusisitiza siyo tu ukweli wa lile alilolisema bali pia uzito wake.
Kwa namna hiyo Bwana Yesu alidhihirisha pia
mamlaka yake katika lile alilosema.
Katika kitabu cha Ufunuo
Yesu mwenyewe anaitwa Amina, kwani yeye ni mwaminifu
kabisa katika maneno yake na kwamba yale anayosema kwa uhakika yatatimia.
Tunasoma hivi: “Haya ndiyo anenayo yeye aliye Amina. Shahidi aliye mwaminifu na wa
kweli...” (Ufu 3:14). Yesu
mwenyewe anajiita “njia, na ukweli na
uzima” (Yn 14:6).
Katika
Liturujia
Katika Liturujia yetu Amina
ni kiitikio muhimu sana. Tunapoanza Sala zetu na kuhitimisha tunafanya Ishara ya Msalaba
na kuitikia Amina.Tunaposema Amina tunasisitiza umuhimu wa kuanza
Sala au Liturujia tunayoadhimisha kwa jina la Utatu Mtakatifu. Kwa Sala hiyo msingi
tunautukuza Utatu Mtakatifu na kuomba utuongoze katika Liturujia yetu
tunayoadhimisha au Sala yetu tunayoitoa. Kwa kupiga Ishara ya Msalaba
tunajiweka mikononi mwa Utatu Mtakatifu tunapoanza Sala zetu au kuadhimisha
Liturujia, na tunapomaliza tunapiga tena
Ishara ya Msalaba na kusema Amina. Katika Adhimisho la Liturujia
kwa kawaida kuhani huhitimisha kwa Baraka ndipo waamini hujiandika Ishara ya
Msalaba.
Hata hivi katika Adhimisho moja la
Liturujia kuna Sala mbalimbali ambazo kuhani au atazitamka kwa sauti peke yake
kama mwongoza Adhimisho ili waamini wasikie na hatimaye waitikie Amina
lakini kuna Sala ambazo kuhani hutakiwa kusali pamoja na waamini na wote
watazihitimisha kwa pamoja kwa kiitikio hichohicho Amina. Tufuatane
kuangalia Amina katika Adhimisho la Ekaristi, yaani Misa.
Mwanzo wa
Misa
Mwanzoni kuhani huanza: Kwa
Jina la Baba, na la Mwana, na la Roho Mtakatifu. Kama tulivyosema
hapo juu hii ni Sala ya msingi ambayo inatuweka
mikononi mwa Utatu Mtakatifu tunapoanza kuadhimisha Liturujia yetu. Kuhani
akishasema vile Wakristo wote wanatakiwa kuitikia Amina. Wale wasioitikia
wanafanya kosa kubwa la kutokukiri imani kwamba tunajiweka mikononi mwa Utatu
Mtakatifu. Wanatakiwa kujiuliza wamefika kanisani kufanya nini?
Kuhani huwasalimu waamini na kisha
hutualika kukiri dhambi zetu. Hapo kuna namna mbalimbali za kukiri dhambi,
lakini zote huishia na Sala anayotamka kuhani: Mungu mwenyezi atuhurumie,
atusamehe dhambi zetu, atufikishe kwenye uzima wa milele. Waamini wote
hutakiwa kuitikia Amina. Kwa nini wengine
basi hawaitikii?
Hata hivi tukumbuke tendo hilo ni la
kukiri dhambi na kuomba msamaha wa jumla katika kujiweka tayari kuadhimisha
mafumbo matakatifu kama mwaliko wa kuhani unavyosema. Hiyo siyo nafasi ya
Sakramenti ya Kitubio na Upatanisho. Mkristo mwenye dhambi kubwa lazima aende
kuungama kwa kuhani yaani padri au Askofu.
Baada ya tendo la kukiri dhambi na
kuomba msamaha hufuata Utenzi wa Utukufu ambao huimbwa au kusemwa siyo na kwaya
peke yao bali na waamini wote pamoja na kuhani. Utenzi huishia na Amina.
Waamini wote pamoja na kuhani hukiri kwamba walivyoimba au kusali ni ukweli
kabisa.
Sehemu ya Mwanzo wa Misa huhitimishwa
na Sala iitwayo Kolekta, kutokana na neno la kilatini lenye maana ya kukusanya. Kuhani akishasema: Tuombe, inampasa kunyamaa kitambo ili kila Mkristo
na kuhani mwenyewe wasali kimya ndipo kuhani ahitimishe maombi yao kwa sala
iliyomo katika kitabu cha Misa. Sala anayosali kuhani ni kama inakusanya na
kuhitimisha maombi ya Wakristo wote wanaoshiriki Misa hiyo. Mwishoni mwa Kolekta hiyo wote hutakiwa kuitikia Amina.
Asiyeitikia huwaza nini moyoni mwake?
Liturujia ya
Neno
Wakati wa Liturujia ya Neno, kabla ya
Injili, kuhani hujiandaa kwa Sala fupi
ili kutangaza Injili. Iwapo Misa huongozwa na Askofu, shemasi au padri iwapo shemasi hayuko huomba
Baraka kwa Askofu. Anapopata Baraka
hupiga ishara ya Msalaba na kutikia Amina.
Baada ya mahubiri, siku za Dominika
na Sherehe hufuata Kanuni ya Imani ambayo, kama utenzi wa Utukufu kwa Mungu juu, huimbwa au
husemwa na Wakristo wote, na mwishoni wote humaliza kwa Amina.
Tunapomaliza sehemu ya Liturujia ya
Neno kuhani huwaalika waamini kusali: Salini ndugu, ili sadaka yangu na yenu
ikubalike kwa Mungu Baba mwenyezi. Wakristo wakishasali hawasemi
Amina
kwa sababu kuhani huendelea mara na Sala iitwayo Sala juu ya Vipaji (oratio super oblata) ambayo ni ya kuombea
dhabihu. Baada ya Sala hiyo ndipo Wakristo wote huitikia Amina. Tujibidishe kufanya
vile.
Sala Kuu ya
Ekaristi
Sala ya kuombea vipaji huhitimisha
sehemu ya kuandaa vipaji. Hufuata Sala Kuu ya Ekaristi inayoanza na dayalojia: Bwana
awe nanyi,... Inueni mioyo .. Mwishoni mwa Sala Kuu ya Ekaristi
hufuata kiitikio cha Amina, ambayo huitwa Amina
Kuu. Waamini wote hutakiwa kuitikia kwa nguvu Amina hiyo Kuu. Katika
Sherehe waamini wote siyo kwaya
peke yao, waimbe Amina mara tatu. Wanamuziki wazingatie
hilo wakitunga muziki.
Baada ya Amina kuu hufuata sehemu
ya kujiandaa kwa Komunyo Takatifu, inayoanza na Sala ya Bwana: Baba
yetu uliye mbinguni. Baada ya sala hiyo hatuitikii Amina kwa
sababu kuhani huendelea`mara :Ee Bwana, tunakuomba utuopoe ...hatimaye
wote huitikia: Kwa kuwa ufalme ni wako, na nguvu...
Hufuata mara Sala ya kuomba Amani
ambayo kuhani husali na mwishoni wote huitikia Amina. Wakati wa kupokea Ekaristi kila Mkristo
hutakiwa kuitikia Amina kabla ya kupokea Mwili wa Bwana. Ni tendo la kukiri imani
kwamba unasadiki huo ni Mwili wa Kristo. Wote huitikia Amina mwishoni mwa Sala
baada ya Komunyo.
Hatima
Mwishoni mwa Misa wakati kuhani
anapowabariki waamini ndipo wote wakiinamisha vichwa vyao, hupiga Ishara ya
Msalaba na kuitikia Amina ya mwisho.Wito kwa Wakristo wote: Tuitikie AMINA
wakati wa Liturujia, bila kusita.Kwa kufanya vile tunashiriki na kusali na kuhani tena tunakiri imani yetu kwamba alivyotamka
kuhani ninakubali, ni kweli kabisa na Sala hiyo huwa Sala yetu pia.
Comments
Post a Comment