CARITAS-TUNAWEKA KAMBI BUKOBA
Na Pascal Mwanache, Dar es salaam
KUFUATIA majanga yaliyosababishwa na
tetemeko la ardhi lililoikumba baadhi ya mikoa ya Kanda ya Ziwa, hasa Mkoa wa
Kagera, Idara ya Caritas, katika Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania imedhamiria
kuweka kambi Mkoani Kagera.
Akizungumza
na Gazeti la Kiongozi, Katibu Mtendaji wa Caritas Tanzania, Laurent Masui
ameeleza kuwa tayari idara hiyo imepeleka maafisa wake mkoani Kagera, kwa ajili
ya kufanya tathmini ya awali itakaowezesha kubaini ukubwa na madhara ya
tetemeko hilo.
“Sisi
tutaendelea kuwepo pale kwa kuwa hiyo ndiyo kazi yetu. Awali ya yote ni lazima
tutambue msaada wa aina gani unaohitajika; ni wa dharula, wa haraka au wa muda
mrefu. Hivyo lengo la kupeleka wataalamu wetu ni kufanya tathmini
itakayotusaidia kuwa na vipaumbele vinavyoakisi mahitaji ya muda huu” ameeleza
Masui.
Pamoja
na timu ya wataalamu wa Caritas kuwasili Bukoba na kuanza kufanya tathmini,
Masui amebainisha kuwa ofisi ya Caritas Taifa imewasilisha fedha zipatazo Tsh Milioni
10 katika ofisi ya Caritas Jimbo Katoliki Bukoba, ikiwa ni hatua za awali za
kusaidia wahanga wa tetemeko hilo.
Aidha
Masui amesema kuwa utoaji wa misaada kwa wahanga hao ni lazima ujali mahitaji
halisi ya waathirika hao, na kushauri kuwa lazima kuwe na kipaumbele katika
kutoa misaada mbalimbali.
“Tetemeko
limeathiri huduma za kijamii, miundombinu na maisha ya wakazi husika, hivyo
misaada tunayoitoa ni lazima iongozwe na kipaumbele kadiri ya mahitaji. Ni
lazima tukaone watu wanahitaji nini ili tuweze kujua kipaumbele ni kipi.
Tutaweka kambi Kagera, na kambi hiyo itakuwa endelevu” ameongeza.
Madhara mpaka sasa
Vifo vya waathirika wa tetemeko
la ardhi mkoani Kagera mpaka kufikia Septemba 14 vimefikia watu 17.
Kwa mujibu wa Mkuu wa Mkoa wa
Kagera, Salum Kijuu, shule za sekondari za Nyakato na Ihungo mkoani humo
zimefungwa kwa muda wa wiki mbili kutokana na miundombinu yake kuharibika, huku
wanafunzi wakiruhusiwa kurudi katika familia zao baada ya kuonekana kuathirika
kisaikolojia.
Aidha licha ya tetemeko hilo
kuyakumba maeneo kadhaa ya mkoa huo, Kijuu amebainisha kuwa Manispaa ya Bukoba ndiyo iliyoathiriwa zaidi,
kwa kuwa na idadi ya vifo 17, kujeruhi watu 252, kati yao 169 wakiwa wamelazwa
hospitalini, takribani nyumba 753
zimeanguka, na nyumba 1,037 kupata nyufa. Athari za tetemeko hilo pia zimezikumba Halmashauri za Wilaya ya Bukoba,
Misenyi, Muleba, Karagwe na Kyerwa.
Michango mbalimbali na mahitaji
Kwa mujibu wa RC Kijuu, fedha
zinazohitajika kukabiliana na janga hilo ni zaidi ya Tsh bilioni 2.3 kwa ajili
ya mahitaji mbalimbali ya waathirika, na tayari serikali ikihamasisha na
kupatikana zaidi ya Sh bilioni 1.4.
Kati ya fedha hizo
zilizopatikana, TSh milioni 700 zilikuwa ahadi, TSh milioni 646 pesa taslimu,
Dola za Marekani 10,000, Euro 10,000 na mifuko 2,800 ya saruji, huku kampuni za
mafuta ya Oilcom, GBP na Moil, zikijitolea kujenga shule mbili za sekondari
zilizoathiriwa na tetemeko hilo.
Kwa mujibu wa Kijuu mahitaji
yanayohitaji kwa haraka ni dawa, tiba na vifaa tiba, vifaa vya ujenzi mabati 90,000
yenye gharama ya Tsh bilioni 1.7, saruji mifuko 9,000 yenye thamani ya Tsh milioni
162, mbao zenye thamani ya Tsh milioni 450 na misumari yenye thamani ya Tsh
milioni 12 ambapo jumla ni Tsh bilioni 2.3.
Pia Kijuu amewaomba wananchi,
wadau na marafiki walioguswa na janga hilo katika mkoa na nje ya mkoa,
wachangie michango yao kupitia akaunti ya maafa iliyopo katika benki ya CRDB
yenye namba 0152225617300 na kwa walioko nje watumie Swift code:CORUtztz, huku
akiomba watakaowiwa kutoa wawasiliane na ofisi yake kwa maelezo zaidi.
Septemba 10, 2016 majira ya saa
9.27 alasiri mji wa Bukoba ulikumbwa na tetemeko la ardhi, ambalo nguvu ya
mtetemo wake ulikuwa ni 5.7 kwa kutumia skeli ya “Ritcher”. Ukubwa huo ni wa
juu kiasi cha kuleta madhara kama yalivyotokea.
Comments
Post a Comment