Papa amteua Padri Kassala kuwa Askofu mpya Jimbo la Geita

Baba Mtakatifu Fransisko amemteua Padri Flavian Kassala kuwa askofu mpya wa Jimbo Katoliki Geita.

Taarifa iliyotolewa na Katibu Mkuu Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania (TEC) Padri Raymond Saba kwa vyombo vya habari imeeleza kuwa Balozi wa Baba Mtakatifu nchini Askofu Mkuu Fransisko Padilla anayo furaha kutangaza kuwa Papa Fransisko amemteua Padri Kassala kuwa Askofu mpya wa Jimbo la Geita.

Mpaka wakati wa uteuzi wake Askofu mteule Kassala alikuwa Mhadhiri katika Chuo Kikuu Kishiriki cha Stella Maris Mtwara.

Askofu mteule Kassala amezaliwa Desemba 4, 1967 katika Parokia ya Sumve, Jimbo Kuu Katoliki Mwanza. Alipata masomo yake ya Sekondari katika Seminari ndogo ya Mtakatifu Pio wa X, iliyoko Makoko, Jimbo Katoliki la Musoma.

Alijiendeleza zaidi kwenye Seminari Ndogo ya Sanu Jimbo Katoliki Mbulu. Masomo ya falsafa aliyapata kutoka Seminari ya Mtakatifu Anthony wa Padua- Ntungamo, iliyoko Jimbo Katoliki la Bukoba.

Askofu mteule Kassala alijipatia elimu ya Teolojia kwenye Seminari Kuu ya Mtakatifu Paulo- Kipalapala iliyoko Jimbo Kuu Katoliki Tabora.

Alipewa Daraja Takatifu la Upadri hapo Julai 11, 1999 kama Padri wa Jimbo Katoliki Geita. Baada ya Upadrisho kati ya mwaka 1999 hadi mwaka 2002 alikuwa ni Paroko msaidizi katika Parokia ya Sengerema, Jimbo Katoliki la Geita.

Mwaka 2002- 2004 alikuwa ni mlezi na Padri wa maisha ya kiroho Seminari ndogo ya Bikira Maria Malkia wa Mitume, Jimbo Katoliki Geita pamoja na kuwa Mkurugenzi wa Jimbo kwa Mashirika ya Kimissionari ya Kipapa.

Kuanzia mwaka 2004 hadi mwaka 2012 alitumwa na Jimbo kujiendeleza zaidi katika utume wa vijana na katekesi katika Chuo Kikuu cha Kipapa cha Wasalesiani, kilichoko mjini Roma na hapo akajipatia shahada ya uzamivu.

Mwaka 2013 Askofu mteule Kassala alirejea Jimboni Geita na huko akapewa dhamana ya kuratibu miradi ya Jimbo. Kuanzia mwaka 2013- 2015 akepewa dhamana ya kusimamia na kufundisha Chuo Kikuu cha SAUT, Kitivo cha Utalii, Arusha.

Mwaka 2015 alihamishiwa katika Chuo Kikuu Kishiriki cha Stella Maris.


Itakumbuka kwamba, Jimbo Katoliki Geita limekuwa wazi kuanzia Machi 14, 2014 baada ya Baba Mtakatifu Fransisko kumhamisha na kumpandisha hadhi Askofu Mkuu Damian Dallu kuwa Askofu Mkuu wa Jimbo Kuu Katoliki Songea

Comments

Post a Comment

Popular posts from this blog

SALA YA ASUBUHI:SALI HIVI..

Ujio wa Wamisionari wa Kwanza Tanzania Bara (2)

HISTORIA YA SHEREHE YA MOYO MTAKATIFU WA YESU