Fahamu sheria zinazomlinda mtoto katika Ukristo

KATIKA ukristo kuna amri, sheria, maagizo na hukumu. Sheria inayomhusu mtoto moja kwa moja iko katika amri kumi za Mungu.
Mtume Paulo anafafanua sheria ya mtoto na wazazi au walezi wake kutoka katika amri za Mungu pale alipoandika kusema, “Waheshimu baba na mama yako…” Efeso 6:1. “Enyi watoto watiini wazazi wenu….” “wazazi wasiwachokoze au wasiwakwaze watoto wasije wakakata tama” Efeso 3:21.

Wajibu wa wazazi kwa watoto
Ukristo unatambua kwamba mtoto ni tunda la ndoa na ni Baraka katika familia. Hivyo wazazi wana wajibu wa kutambua kuwa kupewa watoto na Mungu ni Baraka kubwa, kwani kila kitu hutoka kwa Mungu, “…Una kitu gani wewe ambacho hukupewa? Na ikiwa umepewa, ya nini kujivunia kana kwamba hukukipewa?” (1Kor. 4:7).
Hivyo hata watoto wametoka kwake, “Watoto ni riziki kutoka kwa Mwenyezi Mungu; watoto ni tuzo lake kwetu sisi” (Zab. 127:3).
Kuwapa watoto wosia mzuri, “Mwanangu, uwe mwaminifu kwa Bwana Mungu wetu siku zote za maisha yako. Usitende dhambi kwa kusudi, wala usivunje amri zake. Tenda yaliyo mema maisha yako yote wala usifuate njia ya uovu. Maana ukitenda vitu kwa uaminifu utafanikiwa katika mambo yako yote…” (Tob. 4:5-6).

Nidhamu ya kuwalea watoto inasisitizwa sana kwani ndio msingi wa kujenga taifa bora linalomcha Mungu, “Nanyi akina baba, msiwachukize watoto wenu ila waleeni katika nidhamu na mafundisho ya kikristo” (Waef. 6:4).
Wazazi wanakumbushwa kuacha hasira katika malezi ya watoto wao, kwani hasira haijengi bali hubomoa, “Usiwe mwepesi wa hasira maana, hasira hukaa ndani ya wapumbavu” (Mhu. 7:9). Kadhalika, Mungu anamkumbusha nabii Yona kuwa hasira haifai, “..unadhani unafanya vema kukasirika?” (Yona 4:4).
Wazazi wana wajibu wa kuwalea na kuwaelekeza watoto wao mambo yaliyo mema kwa upole, “…lakini sisi tulikuwa wapole kati yenu kama alivyo mama kwa watoto wake” (1The. 2:7).
Wazazi, walezi na jamii wana wajibu wa kuwasaidia, kuwajali, kuwatetea watoto yatima, “…tendeni haki, ondoeni udhalimu, walindeni yatima…” (Is. 1:17).

Wajibu wa watoto kwa wazazi
Kama ulivyo wajibu wa wazazi kwa watoto, vivyo hivyo watoto nao wana wajibu mkubwa mbele ya Mungu na mbele ya wazazi na jamii. Wanapaswa kuwa wasikivu, watii na wenye heshima kwa wazazi au walezi wao. Watoto wanapotimiza wajibu wao vizuri hupata tuzo, Baraka na heri katika maisha yao.
Katika amri za Mungu, amri ya nne inasema “ waheshimu baba yako na mama yako ili uishi maisha marefu katika nchi ninayokupa mimi Mwenyezi Mungu wako” (Kut.20:12)
Utii pia ni kitu muhimu sana kwa watoto kwani unasisitizwa sana katika maandiko Matakatifu, “Enyi watoto, watiini wazazi wenu katika Kristo maana hili ni jambo jema” (Waef. 6:1)
Watoto wana wajibu wa kusikiliza na kutekeleza maagizo wanayopewa na wazazi au walezi kwa wakati. Yesu anaonesha mfano mzuri na wa kuigwa katika hili, “Basi akarudi pamoja nao hadi Nazareti…” (Lk. 2: 51).

Haki za mtoto katika Ukristo
Ukristo umepinga ukatili kwa watoto katika mambo mengi kama ifuatavyo:
Ukristo unamtazama mtoto kuanzia mimba (Yeremia 1:4)
(Kutoka 20:13) Amri kumi za Mungu Usiue; hivyo tunasisitizwa juu ya ulinzi wa mtoto kuanzia mimba.
(Marko 10:13-14) Waacheni watoto wote waje kwangu msiwazuie, haya ni maneno ya Yesu kuonesha upendo kwa watoto.
(Mithali 22:6) Mfunze mtoto njia njema hataiacha-watoto warithishwe matendo mema hivyo wazazi ni mfano wa kuigwa
(Yoshua 24:15) kuwalea watoto katika mazingira ya imani…mimi na nyumba yangu tunamtegemea bwana.
Hivyo ni wajibu wa wakristo kuishi maisha mazuri nay a mfano katika familia na jumuiya zao, ili kuwafanya watoto waweze kufuata mifano iliyo bora na mizuri toka kwa wakubwa.


(Imeandaliwa kwa msaada wa ‘mwongozo wa viongozi wa dini na waamini wao katika kuzuia ukatili dhidi ya mtoto’)

Comments

Popular posts from this blog

SALA YA ASUBUHI:SALI HIVI..

Ujio wa Wamisionari wa Kwanza Tanzania Bara (2)

HISTORIA YA SHEREHE YA MOYO MTAKATIFU WA YESU