Fahamu undani wa Ensikliko ya Papa Fransisko juu ya Mazingira

Swali: Hivi karibuni Baba Mtakatifu Fransisko ametoa ensikliko yake kuhusu mazingira na kuiita ‘Laudato Si’ unaweza kutuambia maana yake ni nini?

NI ada ya nyaraka zote za kimawasiliano kutoka Vatikani kujulikana kwa jina linalotokana na sentensi (au kishazi) ya kwanza katika waraka ule. Katika ensikliko hii maneno hayo ni ‘Laudato Si’ yaani ‘ sifa kwako ee Bwana’.
Maneno haya yametoka katika ‘mashairi ya Mtakatifu Fransisko’ juu ya mazingira. Lakini waraka wenyewe, kama zilivyo nyingine zote, unajulikana kwa kichwa cha habari chenye dhima zinayowasilishwa humo: Juu ya uangalizi wa nyumbani mwetu.

Swali: Je ni mambo yapi ambayo yameongelewa ndani ya ensikliko hii?

Kabla mtu hajasoma waraka huu anapaswa ajue aina ya uandishi uliotumika. Baba Mtakatifu anaandika kwa kufuata mtindo wa ‘tafakari tunduizi’: ona, amua na tenda. Hii inaonekana kadri sura zinavyojitokeza, kuanzia sura ya kwanza hadi ya mwisho.

Kwa kufuatia dhima zake kazi hii imegawanyika katika makundi makubwa sita. Dhima hizi tumeziongelea tayari hapo juu. Uzuri ni kwamba kila sura ya waraka huu inaongelea kwa kina dhima tofauti.  

Swali: Hebu kwa ufupi kabisa tukumbushie dhima kuu za ensikliko hii

Dhima kadhaa zimeelezwa kwa mapana kabisa na kwa uwazi wa hali ya juu kiasi kwamba kusifiwa kwa kuweza kuyasema yale ambayo wenye maslahi mbalimbali walichelea kuyasema. Dhima hizo ni pamoja na uhusiano kati ya maskini na umaskini pamoja na unyeti (fragility) wa sayari yetu hii. 
Hivi karibuni, kwa mfano Benki ya Dunia imetoa ripoti yake kuhusu athari za mabadiliko ya hali ya hewa na upatikanaji wa chakula. Kulingana na ripoti yao, kwa hakika chakula kimepungua sana na hivyo njaa itaongezeka na umaskini kama yalivyo magonjwa vitaongezeka vile vile.  
Dhima nyingine ni pamoja na uelewa kuwa vitu vyote vilivyomo duniani kwa asili vinahusiana, ni mahusiano. Pia upo ukosoaji wa mitazamo kadhaa mipya juu ya kimazingira na pia nguvu na uwezo utokanao na teknolojia.
Ipo pia haja ya kutafuta njia mpya na mbadala za kuuelewa uchumi na maendeleo, thamani halisi ya/kwa kila kiumbe,  maana ya kiutu ya ekolojia, haja ya kuwepo kwa mazungumzo na mijadala ya wazi na kweli juu ya hali hii,  wajibu madhubuti wa sera za kimataifa na kitaifa juu ya hilo.  Inamalizia na dhima ihusuyo utamaduni hasi uliojitokeza wa utumiaji na utupaji vitu na mapendekezo ya maisha mapya.

Swali: Ni mahusiano yapi hayo yanayoongelewa humu?

Ama kwa hakika mahusiano ndio msingi mkuu kabisa wa maelezo yanayotolewa humu ndani ya ensikliko hii: mahusiano kati ya binadamu, viumbe wengine na sayari yetu hii. Dunia inarejelewa mara zote kama nyumbani mwetu, kama mama yetu na kwa upande mwingine kama dada yetu.
Kwa bahati mbaya uhusiano huu unaelekea kuendelea kuharibika kadri tunavyoyaharibu mazingira yetu. Mara nyingi tunasahau kuwa sisi tumepewa uwakili tu wa kutunza dunia na mazingira yake kwa ajili yetu na kizazi kijacho. Hii yote inatukumbusha juu ya mahusiano yetu sisi na mazingira yetu.

Swali: Kulikoni masuala ya mazingira, mbona tungetaraji abakie katika masuala yanayohusu mafundisho na maadili kama  tulivyozoea?

Kwa kutumia maneno ya Mtakatifu Agustino (Askofu) wa Hippo (maeneo ya Libya ya sasa) viongozi wa kidini ni raia kama walivyo raia wengine wote lakini kwa ajili ya raia hao wanateuliwa kuwa viongozi wao.
Hivyo basi sio sahihi kumzuia kiongozi huyo asiongelee masuala ambayo yanawagusa waumini wake na hata yeye mwenyewe. Mwelekeo huu hasi unazidi kujengeka miongoni mwa wanasiasa wetu ama kwa kutojua au kwa makusudi kabisa, ili wasiwajibishwe na umma.
Katika mchakato wa kuandaa ensikliko hii baadhi ya wanasiasa hasa wa kimarekani, kama ilivyo ada yao kupinga kusikia chochote kutoka kwa viongozi wa kidini sembuse masuala ya kisayansi, walitahadharisha juu ya kanisa kuongelea juu ya suala hili kwa kuwa tu eti ni la kisayansi.
Kwa kuwa huu ndio mwelekeo wao hawakutaka kutambua kuwa, kwanza mwandishi wa ensikliko hii, Papa Fransisko pia ni mwanasayansi. Anayo shahada ya uzamivu ya stadi za kemia. Wengine waliwatania kuwa kwa hili walau wao ndio wanaopaswa kumsikiliza yeye kama wanavyodhanika kufanya kwa wanasayansi wengine.
Pili, mara zote uandiki wa enskliko kama ilivyo hii uhusisha pia mashauriano mengi, marefu na ya kina yanayohusisha kada mbalimbali za kitaaluma na kijamii. Ensikliko hii ilijumuisha michango ya wanasayansi, wanafalsafa, wanateolojia, na hata makundi ya kijamii. Bahati mbaya wagomvi wa wanasiasa hao mara nyingi huwa wanateolojia na imani zao.
Mababa watakatifu wengine pia wamegusia hayo; hivyo kama ni ‘lawama’ au pongezi kuhusu mafundisho ya aina hiyo hata wao wanastahili. Mtakatifu Yohana Paulo wa Pili anasisitiza kuwa ni wajibu wetu katika uumbaji na majukumu yetu kwa viumbe, asili na muumba ni sehemu ya muhimu kwetu kama wakristo na imani yetu.
Baba Mtakatifu Benedikto wa 16 naye pia kazi zake zimehusishwa kwa kurejelewa. Labda kwa taarifa tu, ijulikane pia kuwa wapo watu wengine mbalimbali waliorejelewa katika kazi hii. Hawa ni pamoja na watakatifu Fransisko, Bonaventura, na Tomasi wa Akwino. Wamo pia wanafalsafa kama vile Pd. Teilhard de Chardin na Romano Guardini.
Jambo la kutia moyo ni kwamba baadhi ya watu na vyombo vya habari vilikiri kuwa walau kwa mara ya kwanza suala hili limesemewa kwa uwazi na hakika kabisa. Mara zote mijadala inayohusu masuala haya hugubikwa na unafiki, maslahi binafsi na yanayogongana hivi kwamba mpaka sasa hakuna anayetaka ukweli hasa ujulikane.

Swali: Katika andiko hili kila tunapoambiwa kuhusu ‘kuona’ kabla hatujaamua na kutenda, ni nini hasa tunatarajia ‘tukione’ humu ndani?

Sura ya kwanza inaanza kwa kutuonesha hali halisi; inafanya hivyo kwa kutueleza ni nini kinatokea ‘nyumbani mwetu’ duniani. Sura hii inaorodhesha mambo kadhaa ikiwa ni pamoja na uchafuzi wa mazingira na mabadiliko ya hali ya hewa, uchafu, takataka na utamaduni-potezi (matumizi pindukia na yasiyo ya lazima);
hali ya hewa kama mali ya wote, masuala ya maji na ukosefu wake, upoteaji wa bayoanuai, kuporomoka kwa ubora wa maisha ya mwanadamu na kuparaganyika kwa misingi ya jamii, kutokuwepo kwa usawa, hatua dhaifu dhidi ya haya yote na kuwepo kwa mitazamo kinzani tofauti juu ya nini cha kufanya kukabiliana na hali hiyo.
Ni katika sura hii ndimo tunaoneshwa athari kubwa za kuegemea zaidi kwenye ‘uchumi-ukaa’ katika dunia na maisha ya mwanadamu; pamoja na mambo mengine aina hii ya uchumi na michakato inayoendana inachangia katika kuongezeka kwa joto la tufe (dunia) letu hili, magonjwa na kadhia nyingine nyingi tu.
Aidha athari za kijamii na kimazingira zinazotokana na uchimbaji wa madini zinazungumziwa pia. Katika sura hii Baba Mtakatifu pia anasifia juhudi zinazofanywa na asasi mbalimbali zinazojihusisha na mazingira lakini pia anakosoa baadhi ya mitazamo iliyomo humo kama vile mtazamo hasi juu ya ongezeko la idadi ya watu.
Shida ya hoja hii ni kwamba husababisha watu kutokukubaliana na haja ya kupunguza ‘ulaji-pindukia’ kwa kuwa tu inadhaniwa kuwa kuongezeka kwa idadi ya watu ndio chanzo cha mapungufu yote hayo.  La hasha!

Swali: Je katika maelezo yote haya nini nafasi ya neno la Mungu?

Kwa kuwa masuala yahusuyo hali ya hewa na mazingira yanahusisha uumbaji, basi hata neno la Mungu ndani ya ensikliko hii litahusianisha uumbaji. Katika ensikliko hii, kama zilivyo nyingine zote, usingetegemea kukosa sehemu inayohusianisha Habari Njema (neno la Mungu) na masuala yanayozungumziwa humo ndani; hii ndio injili yake yaani injili ya uumbaji.
Sura ya pili imejikita katika kutufikishia Injili ya uumbaji. Humu tunapatiwa mwanga kama unavyotolewa na imani, tunapata busara za simulizi za kibiblia, tunaoneshwa fumbo la ulimwengu, ujumbe kwa kila kiumbe ndani ya utangamano wa uumbaji, ushirika wa wote na hatma ya jumla ya vitu vyote. 
Hapana shaka Biblia haitoi ruhusa ya mitazamo potofu ya kibinadamu juu ya viumbe wengine. Mitazamo hii potofu inapelekea hata kusafirisha nyara na wanyama walio hatarini kutoweka; hata kuruhusu biashara ya binadamu vile vile.

Swali: Je waweza kuongelea juu ya nafasi ya teknolojia katika kadhia yote hii?

Sura ya tatu kama zilivyo zile zilizoitangulia inajikita katika kuelezea hali halisi na hapa inajikita katika kuelezea nafasi ya teknolojia katika madhila yote haya. Pamoja na kuelezea ubunifu na uzalishaji, pia sura inazungumzia juu ya utandawazi wa mtazamo wa mfumo-kiteknolojia.
Pia inatanabaisha madhara na mkanganyiko wa mitazamo ya kisasa juu ya nafasi ya binadamu katika mambo yote haya. Inaelezea pia shida ya mitazamo inayotegemea msimamo wa mtu binafsi. Katika yote haya zinajadiliwa hoja za kuhakikisha ajira zinapatikana na kulindwa na mwisho zinaainishwa teknolojia mbali mbali za kibaiolojia.
Sura hii inatazama mizizi ya ‘shida’ hizi kutoka katika dhana pacha zinazovuma na kutawala sasa: kwamba teknolojia inaendesha kila kitu (technocratic paradigm) na pia kuwa mwanadamu ndiye kila kitu (anthropocentrism). Dhana hizi zimesababisha wengi kuona kuwa asili ipo tu kwa ajili ya kutumika na kwamba haina thamani yoyote kitasaufi (kiroho);
maana yake ndio kusema kimakosa kuwa raslimali za dunia na maendeleo ya kiuchumi na kiteknolojia pekee yanaweza kutokomeza njaa na umaskini duniani.  Hapana shaka mtazamo huu potofu umepelekea kutojaliwa mazingira, kutothamini uhai wa mwanadamu na hasa kwa wale walio na thamani ‘ndogo’ au wasio na ‘faida’ kama vile mimba, masikini na hata walemavu pia.
Tabia hii ya ‘ulaji’ na itikadi za kiuchumi zinazosukumwa na haja ya kutengeneza faida zimepelekea kwenye tamaa ya kushinda na kutawala inayosababisha kuendekeza tabia na mwelekeo wa ‘kutupilia mbali’ asili na ubinadamu.  Labda tabia ovu ya matumizi ya madawa ya kuongeza nguvu kwa wanariadha hivi karibuni yaweza kuwa ni moja ya utamaduni huo mpya.

Swali: Je sura ya nne inapozungumzia juu ya ekolojia-jumuishi inamaanisha kitu gani hasa?

Katika sura hii Baba Mtakatifu anaongelea juu ya ekolojia-jumuishi. Hapa anaziongelea ekolojia za kimazingira, kiuchumi na hata kijamii kabla ya kugusia utamaduni wa kiekolojia na ekolojia ya kila siku.
Japo kubwa la msingi hapa ni ile kanuni ya manufaa ya wote (common good) na kwa sababu hiyo lipo pendekezo la kuwepo kwa haki miongoni mwa vizazi vyote juu ya masuala ya matumizi ya kimazingira.
Kubwa la msingi hapa ni ile haja ya kukubali ukweli kuwa athari za uharibifu wa mazingira hasa juu ya ekolojia ya utamaduni zinaanza kuonekana wazi wazi miongoni mwa jamii mbalimbali na hasa wenyeji wa asili ya maeneo husika.

Swali; Je ni nini kinapendekezwa kifanyike kukabiliana na kadhia hii?

Kwa kufuata mtindo wa ona-amua-tenda, sura hii ya tano inaainisha nini na namna ya hatua zinazopaswa kuchukuliwa kukabili tatizo na changamoto zinazotokana na kadhia hizi. Humu hatua mbalimbali zimeorodheshwa na kuainishwa.
Si jambo rahisi lakini inaonesha umuhimu wa kubadilisha matumizi toka nishati-makaa kuelekea nishati-rejeshi na pengine ijumuishe pia motisha ya ruzuku kutoka Serikali.
Sura hii inaendelea kusisitiza haja ya kuwepo makubaliano na sheria za kimataifa juu ya kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi, bayoanuai na bahari. Pia inatahadharisha matumizi mabaya ya vocha-ukaa (carbon credits).
Labda tuseme kwa ufupi tu kuwa sura hii inakazia juu ya majadiliano juu ya mazingira, majadiliano juu ya sera mpya za kieneo, kitaifa, kikanda na kimataifa juu ya mambo haya, majadiliano na uwazi katika kutoa maamuzi yahusuyo mambo yanayosababisha na kutokana na kadhia hizi.
Katika kukidhi haja na mahitaji ya kiutu, siasa na uchumi vinapaswa kutiliwa maanani pamoja na dini vilevile. Hapana shaka umuhimu wa dini kujadiliana na sayansi umesistizwa pia.

Swali: Ni ipi nafasi ya elimu ya mazingira na tasaufi (kiroho) katika juhudi zote hizi zinazopendekezwa?

Ensikliko inasisitiza haja ya kubadilisha mitindo yetu ya maisha na kuwa na mitindo mipya kwani mitindo iliyopo ndio imechangia aina hii ya ‘ulaji’ uliopelekea kadhia zinazotukumba. Walaji wanapaswa kufanya ulaji wenye kiasi, unaozuia upotevu wa vitu na mali.
Watu wanapaswa waelimishwe juu ya ‘agano’ kati ya utu na mazingira. Pamoja na kuwepo kwa upendo wa kiraia na kisiasa, mahusiano kati ya viumbe yanapaswa pia kusisitizwa. Ama kwa hakika hata nafasi ya viumbe wengine nao si budi ijaliwe pia kwani lengo la kuwepo kwao si kwa ajili ya mwanadamu tu bali ni zaidi ya hapo.
Kwa namna ya pekee kabisa tunakumbushwa kufikiria masuala ya kimazingira zaidi ya jua, yaani tusiishie kufikiria kuwa jua ndio chanzo na mwisho wa maisha hapa duniani.

Swali: Je kuna jingine lolote unaloweza kuwaambia wasomaji wetu?
Yapo mengi ya kusema kwani matatizo yanayoendana hayapungui vilevile. Labda niliseme hili moja hapa kuwa, Makamu wa Raisi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania aliyemaliza muda wake Dkt Mohamed Gharib Bilal, wakati wa uzinduzi wa chuo kikuu kishiriki cha Marian kule Bagamoyo alituambia kuwa wakati mmoja alipomtembelea Baba Mtakatifu Fransisko, papa alimwambia haya kuhusu uharibifu wa mazingira:
kwamba Mungu husamehe, mwanadamu husahau, lakini katu mazingira hayasahau na wala hayasamehi! Hivyo basi kila ‘ovu’ tuliongezalo kwenye mazingira linasababisha madhara makubwa kabisa, kwa namna yoyote ile tutalilipia tu!

Swali: Ni nini wito wako juu ya yote haya?



Kwa kutumia maneno ya Julius Kambarage Nyerere, tuchukue hatua sasa wakati ndio huu na sio vinginevyo. Hivi karibuni taasisi za Umoja wa Mataifa zimetoa angalizo kuwa kwa takwimu zilivyo sasa baadae mwakani duniani zitafikia rekodi ambayo haijafikiwa kabla na mbaya zaidi hiyo zitavuka viwango vinavyoweza kuzuilika tena! Ndo maana tunasema wakati ndio huu tukiukosa baasi tena!

Comments

Popular posts from this blog

SALA YA ASUBUHI:SALI HIVI..

Ujio wa Wamisionari wa Kwanza Tanzania Bara (2)

HISTORIA YA SHEREHE YA MOYO MTAKATIFU WA YESU