Historia ya Huruma ya Mungu kwa jicho la Mababa Watakatifu

IBADA ya Huruma ya Mungu imepata msukumo na kuhamasishwa katika Kanisa Katoliki katika Karne ya 20 kutokana na ufunuo binafsi aliopewa sista Maria Faustina Kowalska mwaka 1935.
Lakini pia ndani ya Kanisa, Ibada ya Huruma ya Mungu ina historia pana yenye kukita mizizi na kuimarika miongoni mwa Kanisa na waamini.
Mwito kwa Ibada ya Huruma ya Mungu imepata kutolewa na kusisitizwa kwa nyakati tofauti ndani ya Kanisa kupitia mababa watakatifu watatu ambao ni; Papa Yohane XXIII, Papa Yohane Paulo II na Papa Fransisko (Baba Mtakatifu wa sasa). Mababa hawa wametoa mchango mkubwa katika ibada hii ya Huruma ya Mungu kila mmoja kadiri ya nafasi na nyakati yake.

Mchango wa Papa Yohane XXIII
Moja ya mambo ambayo Kanisa linamkumbuka baba huyu ni Mtaguso wa pili wa Vatikano. Katika hotuba yake ya ufunguzi mnamo Oktoba 11, 1962, Papa Yohane XXIII alitoa muongozo wa Mtaguso kuwa ni ufunguo wa huruma na mtazamo mpya wa maisha ya kikristu (aggiornamento).
Akifafanua lengo la kuitisha Mtaguso wa Pili wa Vatikano, Papa Yohane XXIII alisema; “Lengo la Mtaguso ni kutoa muongozo na kufundisha kwa ufasaha ‘hazina azizi za mafundisho ya Kikristu’ (sacred deposit of the Christian doctrine)...”
Aliongeza kwa kusema; “Hapo zamani, Kanisa lililaani vikali (condemned with utmost severity) makosa na uzushi wa kimafundisho katika vipindi mbalimbali...Lakini leo, Kanisa halina budi kuelekeza kwa upole na huruma badala ya kulaani (the church must prefer ‘the balm of mercy to the arm of severity) katika kuelezea kwa kina undani wa mafundisho yake badala ya kulaani wanaoyapotosha...”
Bila shaka ndio maana wakati fulani Papa Yohane XXIII alifahamika kama “Mwalimu wa Huruma na Ukweli” kwani alifahamu fika kuwa yote mawili yanahitajika.

Paenetentiam Agere (Msamaha wa dhambi):
Mnamo Julai Mosi, 1962, Baba Mtakatifu Yohane XXIII alitoa barua ya kichungaji iitwayo “Paenitentiam Agere” ama Msamaha wa dhambi ikiwa ni barua yake ya saba ya kichungaji.
Barua hii iliyofafanua juu ya zawadi ya huruma ya Mungu na umuhimu wa kila mmoja wetu kutambua hitaji la zawadi hiyo katika maisha yake na hivyo kuja kuipokea katika sakramenti ya upatanisho na kufanya kwa dhati kitubio cha ndani (rohoni) na nje.
Baba Mtakatifu Yohane XXIII aliipendekeza njia hii bora kabisa kama namna muafaka ya maandalizi ya Mtaguso Mkuu wa Pili kusudi “mbegu bora ya Mtaguso iweze kuenea/kutawanyika mbali zaidi katika kila pande/pembe ya Kanisa na wala isipotee bure bali ikute ‘mioyo iliyo tayari na iliyoandaliwa, iliyo amini na kweli.”
Papa Yohane XXIII aliamini kuwa, Mtaguso ungezaa matunda mengi na yenye kudumu iwapo tu ‘udongo utakuwa umetiwa rutuba ya huruma ya Mungu’ (only if the soil of receptivity had been fertilised with God’s mercy).
Ndio maana pengine baadhi ya watu hufikiri kuwa baadhi ya maazimio ya Mtaguso wa pili wa Vatikano hayafanyiwi kazi au kuzingatiwa ipasavyo kama ilivyotegemewa kutokana na kutozingatiwa kwa wito wa Yohane XXIII juu ya uongofu, upatanisho/kitubio na huruma ya Mungu.

Mchango wa Papa Yohane Paulo II
Baba Mtakatifu Yohane Paulo II naye ana mchango mkubwa sana katika Ibada ya Huruma ya Mungu ndani ya Kanisa Katoliki.
Kati ya majukumu makubwa aliyokuwa nayo ni kutekeleza kwa ufasaha na ufanisi maazimio ya Mtaguso wa pili wa Vatikano ambao yeye mwenyewe alishiriki kama askofu. Bila shaka kama Papa alikusudia kueneza ‘balm of mercy’ aliyokusudia Yohane XXIII katika ulimwengu wa sasa.
Wakati wa uongozi wa Papa Yohane XXIII, Shajara ya Sista Maria Faustina ilikuwa kati ya orodha ya vitabu vilivyolaaniwa kutokana na tafsiri ya kiitaliano iliyokosewa ambayo ilionesha kana kwamba msamaha wa dhambi unaweza kuwepo kupitia mazoezi ya kiroho peke yake pasipo sakramenti ya Kitubio (Huruma ya Mungu).
Lakini Yohane Paulo II alipokuwa Askofu Mkuu wa Kraków alimuagiza Padri Ignacy Rozycki ayachunguze kwa ufasaha na umakini mkubwa maandishi ya Sr Maria Faustina ili athibitishe kama yanaendana na Teolojia na mafundisho ya Kanisa.
Alipochaguliwa kuwa Baba Mtakatifu, aliufanya uongozi wake kuwa katika mtazamo wa huruma ya Mungu. Mnamo mwaka 1981 alisema; “Tangu mwanzo wa utume wangu katika kiti cha Mtume Petro - Roma, ninaufikiria ujumbe wa huruma ya Mungu kuwa kazi yangu/jukumu langu kubwa...”
Papa Yohane II mnamo mwaka 1997 aliongezea kusema; “Ujumbe wa huruma ya Mungu umekuwa daima karibu nami na mahususi kwangu... Umekuwa pia uzoefu wangu binafsi, ambao nimeambatana nao katika kiti cha Mtume Petro, na ambao kwa namna fulani umekuwa/ umefanya muundo wa upapa wangu.”
Agosti 1992, Yohane Paulo II, aliukabidhi ulimwengu kwa huruma ya Mungu, ili ujumbe wa upendo wenye huruma ufahamike na kujulikana kwa watu wote wa dunia.
Baba Mtakatifu Yohane Paulo II alisisitiza sana kwamba; “ Hakuna kitu ambacho mtu awaye yote uhitaji zaidi kuliko huruma ya Mungu...”
Kwa kupitia barua yake ya kichungaji aliyoipa jina; “Mungu Mwingi wa Huruma” (God is Rich in Mercy) alitoa mwito hasa kwa Kanisa kutolea ushuhuda wa Huruma ya Mungu.
Kwa kupitia andiko lake hilo alisisitiza;”…Kanisa halina budi kutolea ushuhuda huruma ya Mungu inayodhihirika katika Kristu...ikijitambulisha na kukaa katika maisha ya waamini na watu wote wenye mapenzi mema...na kuwaalika wote kuja kuitafuta huruma ya Mungu katika maovu yote na mabaya yote...”
Mnamo mwaka 1993 Baba Mtakatifu Yohane Paulo wa II alimtangaza Sista Maria Faustina kuwa Mwenyeheri na miaka saba (7) baadae (2000), akamtangaza kuwa Mtakatifu.
Sambamba na kumtangaza huko Sista Maria Faustina kuwa Mtakatifu, alitangaza rasmi pia kuwa Jumapili ya pili ya Pasaka kuwa Jumapili ya huruma ya Mungu.
Jambo la kipekee la kustaajabisha na kutafakarisha ambayo tunaweza kuhusianisha maisha binafsi ya kujitoa na kuipa kipaumbele ibada ya huruma ya Mungu aliyoishi sambamba na kuitangaza Injili ya Upendo wenye Huruma ya Mungu Baba Mtakatifu Yohane Paulo wa II ni matukio ya mwisho katika uhai wake kwani Mungu mwenyewe ilimpendeza kumuita kwake usiku wa mkesha wa sherehe ya Huruma ya Mungu mnamo mwaka 2005.
Lakini pia, cha kustaajabisha zaidi na kutafakarisha ni kwamba Baba Yohane Paulo II alitangazwa kuwa Mwenyeheri siku ya Jumapili ya Huruma ya Mungu ya mwaka 2011.
Pia alitangazwa kuwa Mtakatifu Yohane Paulo II siku ya Jumapili ya Huruma ya Mungu ya mwaka 2015.

Mchango wa Papa Fransisko
Ujumbe wa huruma ya Mungu umeendelezwa sasa na Baba Mtakatifu Fransisko. Alipoulizwa, mara tu baada ya kuchaguliwa na Makardinali, kama anakubali kuwa Baba Mtakatifu, alionesha imani yake binafsi katika huruma ya Mungu alipojibu; “Mimi ni mdhambi. Lakini nina imani katika huruma ya Mungu na uvumilivu usio na kikomo/mipaka wa Bwana wetu Yesu Kristu...nakubali.”
Huruma imekuwa sehemu msingi ya historia ya wito wake, akiupokea utume wa upadri kama wito wa ajabu wa huruma ya Mungu.
Kauli mbiu (Motto) yake ikiwa ni; “Miserando Atque Eligendo” (‘by having mercy, by choosing him’) yaani, “kwa huruma kwa kumchagua yeye”. Kauli mbiu yake hiyo inaonesha msisitizo kuwa katika maisha yake yote, na hata katika maisha ya mtu yeyote yule, Mungu hutuita katika huruma na kutukumbatia kwa huruma na upendo.
Papa Fransisko alimsifu Yohane Paulo II kwa kutambua kwa njia ya msaada wa Sr. Maria Faustina kuwa nyakati zetu za ulimwengu wa sasa ni “Kairos” au wakati muafaka wa huruma ya Mungu.
Papa Fransisko alisema kuwa, “Injili nzima, ukristu wote” (whole Gospel, all of Christianity) inajumuishwa katika furaha aliyo nayo Mungu katika kutusamehe sisi...na kuwa huruma ya Mungu ndiyo msukumo wa kweli ambao humuokoa mtu na kuukomboa ulimwengu.
Na kwa namna ya kipekee, Baba Mtakatifu Fransisko alitangaza mnamo Desemba 8, 2015 kuanza kwa Yubilei ya kipekee ya Huruma ya Mungu ambayo inadumu mpaka Novemba 20, 2016 huku akualika Kanisa lote kujinyenyekeza, kuendesha ibada, kuomba msamaha na kutafuta huruma ya Mungu.

“Heri walio na huruma maana watahurumiwa” (Mathayo 5:7).

Comments

Post a Comment

Popular posts from this blog

SALA YA ASUBUHI:SALI HIVI..

Ujio wa Wamisionari wa Kwanza Tanzania Bara (2)

HISTORIA YA SHEREHE YA MOYO MTAKATIFU WA YESU