Huruma ni jina na utambulisho wa Mungu

Fahamu yaliyomo kwenye kitabu kiitwacho ‘Jina la Mungu ni huruma’    

PAPA Fransisko ameeleza kuwa Huruma ndilo jina na utambulisho wa Mwenyezi Mungu. Ameeleza hayo katika mahojiano maalum na Andrea Tornielli, mwandishi wa habari za gazeti la ‘La Stampa’ na mhariri mkuu wa tovuti ya ‘Vatican insider’ katika kitabu ambacho kimezinduliwa na Kardinali Pietro Parolin, Katibu mkuu wa Vatikani “Jina la Mungu ni huruma”.
Kitabu hicho kimegawanyika katika sura tisa ambazo ni majibu ya maswali 40 aliyoulizwa Papa Fransisko kama sehemu ya maandalizi ya maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa Yubilei ya Huruma ya Mungu.
Katika mahojiano hayo Papa amefanya rejea katika Maandiko Matakatifu, Mafundisho ya Mababa wa Kanisa pamoja na watangulizi wake, yaani Papa mstaafu Benedikto XVI, Mtakatifu Yohane Paulo II, Mtakatifu Yohane XXIII na Mwenyeheri Paulo VI. Kitabu hiki kimechapishwa katika lugha tano na nakala ya kwanza ikawasilishwa kwa Papa Fransisko hivi karibuni.

Katika sura ya kwanza, Baba Mtakatifu anafafanua sababu msingi zilizomfanya kuitisha maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa Yubilei ya Huruma ya Mungu: kwanza kabisa ni sala, tafakari na mafundisho ya viongozi wa Kanisa waliotangulia, kwa kuona kwamba Kanisa ni sawa na hospitali iliyoko kwenye uwanja wa vita, linapaswa kuwa karibu zaidi na waamini wake ili kuwaonjesha huruma na upendo wa Mungu.
Kanisa lilikuwa linahitaji muda wa mageuzi katika maisha na utume wake, kwani watu wengi kwa sasa wamepoteza dhana ya dhambi pamoja na kuhisi kwamba hakuna uwezekano wa kusamahewa dhambi zao.

Sura ya Pili, Baba Mtakatifu anazungumzia kuhusu zawadi na umuhimu wa maungamo. Anakiri kwamba, muumini anaweza kuomba huruma ya Mungu moja kwa moja bila kupitia kwa viongozi wa Kanisa waliopewa dhamana na kuwaondolea watu dhambi zao.
Lakini Mama Kanisa kwa busara yake, anataka watoto wake kuonesha moyo wa toba kwa kumwendea Padri anayemwakilisha Kristo Yesu katika kiti cha maungamo.
Hii ndiyo njia sahihi ya kuweza kupata huruma ya Mungu ambayo kimsingi ina mwelekeo pia wa kijamii, tayari kuponya madonda, mipasuko na kinzani za kijamii. Waamini wanakwenda kwenye kiti cha huruma ya Mungu si kwa kutaka kuhukumiwa, bali kukutana na hatimaye kuambata huruma ya Mungu inayoendelea kuusimamisha ulimwengu.

Sura ya tatu, Papa anawaalika waamini kujitambua kwamba wao ni wadhambi, wanapaswa kutubu na kumwongokea Mungu ili aweze kuwaonjesha huruma na upendo wake usiokuwa na kifani.

Hii ni neema ambayo waamini wanapaswa kuiomba kutoka kwa Mwenyezi Mungu kwa kutambua kwamba, huruma ya Mungu ni kubwa zaidi kuliko hata dhambi zinazotendwa na mwanadamu na kwamba msamaha wake ni dawa makini dhidi ya dhambi.
Mwenyezi Mungu kama ilivyokuwa kwa Baba mwenye huruma daima anawasubiri watoto wake kukimbilia huruma, kwa njia ya toba. Kitendo cha muumini kukimbilia kiti cha huruma ya Mungu kinaonesha toba ya ndani, sala inayopaswa kujikita katika unyenyekevu wa moyo badala ya litania ya maneno mengi.

Sura ya nne, Baba Mtakatifu anasema kuwa hata Khalifa wa Mtakatifu Petro anahitaji kuonja huruma ya Mungu katika maisha yake, kama ilivyokuwa kwa Mtakatifu Petro pale alipotambua mapungufu yake akaangua kilio.
Ameeleza kuwa muungamishaji asiwe ni mtu mwenye kiburi, bali aoneshe unyenyekevu na ukweli wa maisha kwa kutambua kwamba hata yeye pia ni mdhambi anahitaji huruma ya Mungu.

Sura ya tano, Baba Mtakatifu Fransisko anasema kuwa Kanisa linalaani dhambi, lakini linamkumbatia mdhambi anayetambua dhambi zake, tayari kutubu na kumwongokea Mwenyezi Mungu.
Kanisa halina budi kusamehe bila kuchoka kama anavyofundisha Yesu mwenyewe kwa wafuasi wake. Mwenyezi Mungu yuko radhi kumpokea muumini anayeonesha moyo wa toba na wongofu wa ndani, tayari kukumbatia huruma ya Mungu. Kanisa lipo ili kuwawezesha waamini kukutana na huruma ya Mungu katika maisha yao.

Sura ya sita, Papa anawaonya waamini wanaodhani kwamba wanaweza kujiondolea wenyewe dhambi zao kwani tabia kama hii inamchukiza Mwenyezi Mungu na kwamba, ni “ugonjwa wa kiroho” unaopaswa kupewa tiba muafaka.
Waamini waoneshe nia ya kutaka kutubu na kumwongokea Mungu katika maisha yao, hapa watapata tiba kamili bila kujiaminisha kwamba wanajiweza kwa kila jambo.
Binadamu ni mavumbi mbele ya Mungu, kumbe anapaswa kujinyenyekesha, kutubu na kuomba msamaha na huruma ya Mungu.
Onyo hili, anasema Papa, si tu kwa waamini walei hata kwa Wakleri na Watawa ambao wanadhani kwamba kutokana na maisha na utume wao hawana sababu ya kukimbilia huruma ya Mungu.
Kwa waamini hata wale ambao jamii inawaona kuwa wamekengeuka kiasi hata cha kupoteza dira na mwelekeo wa maisha kama wale wanaoshabikia ushoga na mifumo ya utamaduni wa kifo, wanapaswa kuangaliwa kwa jicho la huruma kama Katekisimu Mpya ya Kanisa Katoliki inavyofundisha.
Huruma ya Mungu si dhana ya kufikirika inayoelea kwenye ombwe, anasema Papa, bali ni sifa kuu ya Mungu na mafundisho ya Kanisa. Yesu alikuja ulimwenguni ili kumkomboa mwanadamu kutoka katika dhambi na mauti kwa kumjalia maisha ya uzima wa milele.
Ni mganga wa kweli anayewatafuta wagonjwa na wala si wenye haki ambao hawahitaji kutubu na kumwongokea Mungu.

Katika Sura ya Saba, Baba Mtakatifu anasema kuwa mdhambi anaweza kuvumiliwa lakini fisadi na mla rushwa, hawa ni watu hatari kwani wanatenda dhambi lakini si wepesi kuungama dhambi zao tayari kujipatanisha na Mungu.
Mafisadi na wala rushwa ni watu wanaowatesa na kudhalilisha wananchi wengine; ni wanafiki. Katika maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu Huruma ya Mungu, Papa Fransisko anawaalika mafisadi na wala rushwa kutubu na kumwongokea Mungu, ili kuanza ukurasa mpya wa maisha yao. Wamwombe Mungu neema ya kuona aibu kwa dhambi walizotenda.

Katika  sura  ya  nane, Baba Mtakatifu anawakumbusha walimwengu kwamba Mwenyezi Mungu anawapenda upeo na anataka kuwaonjesha huruma yake isiyokuwa na mipaka. Mwenyezi Mungu kwanza kabisa anaonesha uso wa binadamu na pili uso wa Kimungu.
Yesu anamwangalia mwanadamu kutoka katika undani wa maisha yake na wala si kama mpiga picha anayeangalia mambo ya nje.


Sura ya tisa ambayo ni hitimisho la maswali 40 ambayo Papa Fransisko amejitahidi kuyajibu kwa ufasaha, inajikita katika matendo ya huruma: kiroho na kimwili; mambo msingi yanayomwezesha muumini kuonja huruma na upendo wa Mungu katika maisha yake.

Comments

Popular posts from this blog

SALA YA ASUBUHI:SALI HIVI..

Ujio wa Wamisionari wa Kwanza Tanzania Bara (2)

HISTORIA YA SHEREHE YA MOYO MTAKATIFU WA YESU