Huruma ya Mungu imetufikia, kazi kwetu kuikimbilia


MWAKA Mtakatifu wa Yubilei ya Huruma ya Mungu uliotangazwa na Baba Mtakatifu Fransisko huku ukiongozwa na kaulimbiu “Iweni na huruma” umezinduliwa rasmi hapo Desemba 8, 2015 katika Sherehe ya Bikira Maria mkingiwa Dhambi ya Asili, kwa kufungua Lango Kuu ya Yubilei katika Kanisa Kuu la Mtakatifu Petro lililoko mjini Vatikani.
Baba Mtakatifu, wakili wa Kristo, Mrithi wa Mtume Petro na Kiongozi wa Kanisa zima, katika Waraka wake wa kichungaji, “Misericodiae Vultus”, “Uso wa huruma” anawaalika waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema kutangaza huruma ya Mungu kwa njia ya ushuhuda wa imani tendaji kutoka katika moyo na akili ya mwanadamu, kwa kuonesha huruma na mapendo.

Manaa ya Mwaka wa Yubilei

Kwa maana ya jumla mwaka wa Yubilei “ni mwaka wa msamaha wa dhambi na maondoleo ya adhabu zake, ni mwaka wa mapatano kati ya maadui, ni mwaka wa uongofu wa ndani, ni wakati wa kupokea Sakramenti ya Upatanisho kwa uzito wa hali ya juu kabisa;
Ni mwaka wa kuimarisha mafungamano ya kidugu na kijamii, ni mwaka wa kuyakumbatia maisha kwa matumaini makubwa, ni mwaka wa kuzingatia haki na kukuza upendo, ni mwaka wa kujidhatiti katika kumtumikia Mungu na jirani kwa furaha na hivyo kujenga amani ya kudumu kati yetu na ndugu zetu wote”.
Hii inatokana na ukweli kwamba, Kanisa daima ni mtumishi wa upendo. Yubilei ya Huruma ya Mungu uwe ni mwaka unaowahamasisha waamini kutubu na kumwongokea Mungu; sanjari na kuwa tayari kujipatanisha na Mungu pamoja na jirani zao, ili kuchuchumia rehema na baraka zinazotolewa na Mama Kanisa katika maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu.

Kufungua Lango katika Kanisa Kuu; Lango hilo linamaanisha nini? 

Lango hilo lililosheheni uzito wa fasihi, linamaanisha mpito kuelekea mwaka wa pekee wa uinjilishaji na sala. Baba Mtakatifu Fransisko amelisukuma lango hilo ikiwa ni ishara rasmi ya kuuzindua mwaka wa Yubilei.
Lango hilo hufunguliwa ili kuashiria na kualika dhana ya msamaha, ambao ni lengo kuu la Mwaka huo Mtakatifu wa Yubilei. Kadiri ya hati ya “Mondo Vaticano”, yaani ulimwengu wa Vatikani, historia ya lango hili Kuu ina chimbuko lake tangu zamani za mwanzo wa Ukristo ambapo wadhambi walifanya toba na wakapekwa malipizi ya hadhara kabla ya kupewa mandoleo ya dhambi.
Watubu, hawakuruhusiwa kuingia Kanisani kabla ya kumaliza toba yao. Baada ya kukamilisha mambo yote, ndipo wakaruhusiwa kuingia Kanisani kwa ibada maalumu.
Ndivyo hata nyakati zetu hizi, mahajuji wanaingia ndani ya Kanisa Kuu kupitia lango Kuu kama ishara ya toba yao na kuiambata tena imani kwa moyo mmoja. Hivyo tendo la kufungua malango na kuyapitia malango hayo kuna maanisha kipindi maalumu kilichotengwa kwa ajili ya wanadamu kutakasa roho zao.
Kwa karne nyingi, lango hilo la Jubilei Kuu halikufunguliwa kwa funguo, bali kwa nyundo, kwa sababu malango ya haki na huruma hufunguka kwa nguvu ya sala na toba. Lakini katika mwaka Mtakatifu wa Yubilei Kuu ya miaka 2000 tangu kuzaliwa kwake Kristo, Mtakatifu Yohane Paulo II, hakutumia funguo wala nyundo, bali alilisukuma lango hilo kwa nguvu na kulifungua.
Lango hilo linabeba dhamira ya dhambi na huruma ya Mungu kadiri inavyoonekana katika kipande cha 15 cha shaba zinazopamba lango hilo.  Kuna picha pia za matukio ya agano la kale na Jipya, pamoja na kuanguka kwa mwanadamu, picha ya kupashwa habari Bikira Maria na picha ile ya Mwana Mpotevu na Baba mwenye huruma. Tafakari ya picha hizo ndiyo inayotusindikiza katika hija yetu ya Mwaka huo Mtakatifu.
Lakini kubwa na la muhimu zaidi ni kuwa sote kwa pamoja tunaalikwa kufungua milango ya mioyo yetu na akili zetu, ili tuweze kutoa msamaha na kupokea msamaha. Malango ya mioyo yetu na akili zetu, yatafunguka kwa nguvu ya sala na toba.
Mama Kanisa anatumia nyundo, funguo za kila aina na nguvu takatifu ili kutusaidia kufungua malango ya mioyo yetu. Kuna nyundo ya Maandiko Matakatifu, nyundo ya Sakramenti za Kanisa na Visakramenti; nyundo ya Mafundisho mbalimbali ya Kanisa na funguo za baraka  na neema mbalimbali. Funguka, upokee huruma ya Mungu

Huruma ya Mungu hutuweka Huru

Kuishi kwa kutumiani huruma ya Mungu hutupa nafasi ya kufungua milango ya upeo na hutufanya tuweze kuona mbali na kuwa huru dhidi ya wasiwasi, mashaka, woga na kutenda dhambi.
Hakuna sababu za kuwa na hofu au woga katika kuomba msamaha kwa dhambi zetu , kwa kuwa Mungu wetu ni Mungu Mkuu mwenye kuziona dhambi zetu na hutusamehe kila tunapoomba kusamehewa.
Binadamu anapaswa kutambua kwamba, Mungu ni mkuu kuliko dhambi zetu. Tunapokutana na Kristo katika Sakramenti ya Kitubio tunapaswa kubadilika kiroho. Ni wakati wa kuanza kuona kile tulichokosea, kuuona ukweli.
Matendo mema na huruma kwa wengine daima huonyesha ukweli; ukweli wenye kuwa na matumaini. Na hivyo matumaini hayo kwa Mkristo inakuwa ni fadhila , ambayo ni zawadi kuu kutoka kwa Mungu,  zawadi yenye kuturuhusu kuona  zaidi ya matatizo na mateso hasa  zaidi sana yanayotokana dhambi zetu. 
Ni Matumaini yenye kuturuhusu  sisi kuona uzuri wa Mungu. Pia kwa wale wenye kuwa na fadhila hii ya matumaini huwa huru na nguvu za kuona mbele zaidi ya mabaya ya  nyakati, iwe kwa ajili ya afya yao au kwa ajili ya familia yao.

Mwanzo mpya wa maisha ya kiroho

Hiki ni kipindi kikuu cha msamaha. Kwa kufungua Malango yote ya Yubilei sehemu mbalimbali za dunia waamini tunaalikwa kuwa chemchemi ya furaha licha ya shida na magumu tunayokutana nayo katika maisha kwani Mungu yuko kati yetu.
Tunaalikwa kufanya tafakari ya kina kuhusu matendo ya huruma kiroho na kimwili, fadhila ambazo zinaendelea kutoweka pole pole katika uso wa dunia. Waamini tunaalikwa kwa namna ya pekee, kujiaminisha mikononi mwa Mwenyezi Mungu, kama mwanzo mpya katika hija ya maisha yao ya kiroho, wakati huu wa maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa Yubilei ya Huruma ya Mungu.
Huruma ya Mungu ni Yesu mwenyewe, Msamaria mwema aliyejitaabisha kumganga mwanadamu katika maisha yake ya kiroho kwa kumwondolea dhambi pamoja na kumpatia mahitaji yake ya msingi.
Yesu alihubiri na kushuhudia huruma ya Mungu kati ya watu wake inayopita dhambi na mapungufu ya binadamu, mwaliko kwetu kukimbilia huruma ya Mungu katika hija ya maisha yetu.

Mwaliko wa kuwa mashuhuda wa huruma ya Mungu

Pia waamini tunaalikwa kuwa vyombo na mashuhuda wa matendo ya huruma kwa maskini na wote waliosahaulika katika jamii.
Huu ni mwaliko kwetu kufanya tafakari ya kina kuhusu maana ya huruma ya Mungu, tayari kuishuhudia imani kwa jirani zetu na ulimwengu wote.

Injili ya uhai
Pia huu ni wakati wa kutoa kipaumbele cha pekee kwa Injili ya Uhai, kwa kuthamini maisha kama zawadi kubwa kutoka kwa Mwenyezi Mungu inayopaswa kulindwa na kuendelezwa.
Uchu wa mali na utajiri visiwe ni sababu ya kudhalilisha utu na heshima ya binadamu. Wafanyabiashara, wanasiasa na wadau mbali mbali wanaojikita katika biashara chafu ya silaha wanahamasishwa kuwa mstari wa mbele kushuhudia huruma ya Mungu katika maisha yao.
Huruma ya Mungu iwaguse watu wa mataifa kutoka katika kila dini, kabila, lugha na jamaa. Huruma ya Mungu ikimwilishwa katika ustadi mkubwa, inakuwa kweli ni chachu ya ujenzi wa ulimwengu ulio bora zaidi.

Comments

Popular posts from this blog

SALA YA ASUBUHI:SALI HIVI..

Ujio wa Wamisionari wa Kwanza Tanzania Bara (2)

HISTORIA YA SHEREHE YA MOYO MTAKATIFU WA YESU